Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Sebastian Simon Kapufi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mpanda Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa pongezi kwa wale wote waliopata bahati ya kujengewa barabara kwa kiwango cha lami katika maeneo yao nikiamini kwa kuwa wamepata wataunga mkono suala la kuhakikisha wale ambao hawajapata nao wanapata. Awamu ya Nne ililenga kufungua mikoa ya pembezoni, sambamba na kuiunganisha mikoa hiyo. Naamini wazo hilo bado ni la msingi kwa Awamu hii ya Tano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu Kitaifa unalenga kudhibiti uzito wa magari na matumizi sahihi ya mizani. Ushauri wangu, ili kulinda barabara zetu yawezakana adhabu ya fine imezoeleka, wakati umefika wa kuangalia adhabu yenye mguso kuepuka kujirudiarudia kwa suala hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la hifadhi ya barabara ni jambo la msingi. Suala hili liendelee kuangaliwa katika mipango ya muda mrefu ili kuepuka bomoabomoa na uwepo wa majengo yenye mandhari mbaya pembezoni mwa barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Mpanda – Ugalla – Kaliua – Ulyankulu - Kahama (kilomita 457), naomba iangaliwe kwa jicho la pekee kwani mara barabara hii itakapojengwa itakuwa kwanza ni njia ya mkato/fupi lakini itakuwa ni ufumbuzi wa ziada iwapo barabara ya Mpanda
– Inyonga – Koga - Tabora itapata shida ya kujifunga au vinginevyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza kasi ya ujenzi wa barabara ya Ifukutwa - Vikonge (kilomita 35). Rai yangu ili ujenzi huu uwe na tija, tuone uwezekano wa upatikanaji wa fedha ili kipande kuelekea Uvinza kiweze kufanyiwa kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Daraja la Kavuu na barabara unganishi. Kilomita 10 za barabara unganishi naomba ziendelee kufanyiwa kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia malalamiko ya wakazi waliopisha ujenzi na upanuzi wa Uwanja wa Ndege Mpanda kuhusu fidia yaendelee kufanyiwa kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa kasi ya ujenzi wa barabara ya Tabora – Ipole - Koga - Mpanda kilomita 373 iongezeke kama kweli fedha ya ujenzi huo zipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho pamoja na ujenzi wa reli ya kati, napongeza matengenezo yote yanayoendelea katika reli ya Mpanda. Niombe ratiba ya treni hiyo ya abiria iendeshwe kwa kufuata ratiba sambamba na uongezaji wa mabehewa likiwemo behewa la daraja la kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kunga mkono hoja kwa asilimia mia.