Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
ACT
Constituent
Kigoma Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. KABWE Z. R. ZITTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nitoe shukrani zangu za dhati kwa Mamlaka ya Bandari Tanzania kwa kuendelea kuamini katika maendeleo ya Mkoa wa Kigoma na hususan Mji wa Kigoma kwa kuwekeza katika upanuzi wa Bandari ya Kigoma na ujenzi wa Bandari ndogo za Kibirizi na Ujiji. Pia nawashukuru sana kwa kumaliza kazi Bandari ya Kagunga baada ya kuhangaika nayo kwa muda mrefu sana tangu mwaka 2009.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona zabuni za Bandari ya Kigoma - Ofisi ya Mkoa na pia taarifa ya kazi ya upembuzi yakinifu kwa upanuzi wa Bandari ya Kigoma. Nimeona zabuni ya Bandari ndogo ya Kibirizi na naamini kuwa zabuni kwa ajili ya Ujiji itakuwa imetoka ili kuwezesha gati kujengwa eneo la Ujiji na kuwezesha ndoto yetu ya kurejesha hadhi ya Ujiji katika maendeleo ya nchi yetu. Miradi hii itaingiza fedha kwenye mzunguko wa uchumi wa mji wetu, kutoa ajira kwa wananchi wetu na kupanua shughuli za uchumi za Manispaa ya Kigoma-Ujiji. Nampongeza Mkurugenzi Mkuu wa TPA kwa kuendeleza miradi hii na hii ni ishara ya imani yake kwa ukuaji na maendeleo ya mji wetu na Mkoa wetu wa Kigoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile napenda kumpongeza Meneja wa TANROADS wa Mkoa wa Kigoma kwa juhudi kubwa za kutekeleza miradi ya barabara katika mkoa wetu licha ya changamoto kubwa za fedha. Ujenzi wa mzunguko wa Mwanga Sokoni, taa za barabarani za umeme wa jua kuelekea njia panda ya Mwandiga na kuanza kuandaa zabuni kwa ajili ya barabara ya Bangwe – Ujiji ni juhudi ambazo zinatuunga mkono katika juhudi zetu za kufanya mabadiliko makubwa katika Mji wa Kigoma Ujiji. Namwomba Waziri wa Ujenzi ahakikishe kuwa barabara ya Kasulu katika Manispaa ya Kigoma-Ujiji ambayo inaunganisha Mji wa Ujiji na barabara kuu ya Kigoma - Nyakanazi, inajengwa sasa katika orodha ya ahadi za Rais. Barabara hii yenye urefu wa kilometa 7.5 ni barabara ya kimkakati kwani itaongeza barabara mbadala ya kuingia Kigoma badala ya sasa ambapo kuna njia moja tu ambayo ni hatari kiulinzi na usalama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na shukrani hizo hapo juu bado watu wa Kigoma wanalia na barabara yao kuu inayounganisha mkoa kuanzia Nyakanazi mkoani Kagera mpaka Kigoma Mjini. Eneo la barabara kuanzia Manyovu – Kasulu - Kibondo halina mradi wa ujenzi kwani bado mapitio ya usanifu yanafanywa. Kigoma ni mkoa pekee nchini ambao bado haujaunganishwa na mikoa mingine kwa barabara ya lami moja kwa moja bila maeneo ya vumbi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua kuwa barabara ya Kigoma – Tabora - Singida (Manyoni) – Dodoma sehemu zake muhimu zote sasa zina fedha za wafadhili ikiwemo Nyahua – Chaya – Urambo - Kaliua na Uvinza - Malagarasi lakini kuna kilomita 41 kati ya Kazilambwa (Tabora) na Chagu mkoani Kigoma hazina fedha wala mradi. Serikali itazame upya vipaumbele vyake kwani haitakuwa na maana mtu asafiri kwa lami kutoka Kigoma - Dar es Salaam lakini kuwe na kilometa 41 vumbi. Serikali itafute fedha mahali kwingine na kuongeza kipande hiki katika miradi ya kuunganisha Mikoa ya Kigoma na Tabora na Mashariki mwa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, juhudi za ujenzi wa reli ya kati ni za kimaendeleo na hazina budi kupongezwa na kila mpenda maendeleo. Reli ina faida kubwa kwa nchi na kiongozi yeyote anayefanya maamuzi muhimu kama haya hana budi kupongezwa kwa dhati. Hata hivyo, Serikali ni lazima ifungue masikio kusikiliza maoni mbadala katika utekelezaji wa miradi mikubwa kama hii ambayo inatumia fedha nyingi na tumeamua kutumia fedha za ndani. Uamuzi wa kutumia fedha za ndani ni uamuzi mchungu kwani maana yake badala ya kuwekeza kwenye miradi ya kilimo ili kuongeza uzalishaji wa chakula na bidhaa za kuuza nje, tumeamua kujenga reli. Badala ya kuongeza vyuo vikuu na vyuo vya ufundi ili kuongeza maarifa na wataalam katika nchi yetu tumeamua kujenga reli. Badala ya kuwekeza kwenye kumaliza kabisa tatizo la mtindio wa ubongo (stuntedness) ambalo ni tatizo kubwa sana kwa nchi yetu kwa sasa kwani Watanzania 34 katika 100 wametindiwa ubongo tumeamua kujenga reli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kupanga ni kuchagua. Mmeamua kwa niaba yetu kutumia rasilimali fedha zetu kidogo kujenga reli (na kununua ndege) na haya mengine yasubiri kwanza. Uongozi ni uamuzi. Mmeamua, hatuna namna. Hata hivyo, tusikilizeni sisi wawakilishi wa wananchi, mawazo yetu ni kusaidia kupunguza maumivu ya maamuzi yenu bila kuathiri utekelezaji wa miradi husika. Mimi binafsi naunga mkono uwekezaji kwenye reli lakini siungi mkono namna uwekezaji huu unavyofanywa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiwa mwaka wa tatu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam nilichagua kusoma kozi elective iitwayo Transport Economics lakini nilipoingia darasani chini ya Dkt. Natu Mwamba tulijikuta watatu tu darasani. Hatukutosha na kozi ile haikutolewa mwaka ule. Nilichagua kozi ile kwanza kwa sababu ya mwalimu aliyekuwa anafundisha hiyo kozi, wanafunzi tulimpenda sana. Pili, nimelelewa kwenye uchumi wa usafiri, Mji wa Kigoma (bandari, reli na mipaka ya Kongo na Burundi).
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kukosa kozi ile ikabidi nisome mwenyewe na mtu aliyebadilisha kabisa mwono wangu anaitwa Ndugu Ali Karavina, alikuwa Mbunge wa Urambo. Ndugu Karavina na wenzake waliandika kuhusu ‘Uchumi wa Jiografia’ ukijikita kwenye faida za ujenzi wa reli ya kati. Reli ya kati ni reli kutoka Dar es Salaam (bandarini) mpaka Kigoma (bandarini) na Tabora - Mwanza, Ruvu - Tanga na Kaliua - Mpanda ni matawi ya reli ya kati sio reli ya kati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika andiko lao ‘Uchumi wa Jiografia Tanzania‘, Ndugu Ali Karavina na wenzake walishauri reli ya kati kwa kigezo cha takwimu za mizigo na ndio maana walisema kwanza ijengwe Dar es Salaam - Kigoma kabla ya popote kutokana na mapato yatakayotokana na eneo hilo, ndio matawi yajengwe. Leo kwa mshangao mkubwa Serikali ya Awamu ya Tano imekuja na tafsiri yake ya reli ya kati kwamba ni Dar es Salaam – Isaka - Mwanza. Mimi ni Mtanzania, sina tatizo kabisa na Mwanza kwani siku ikifika nitataka kura za watu wa Mwanza lakini mimi ni mzalendo nataka kuona kuwa maamuzi ya kutumia rasilimali za nchi yanakuwa na faida kwa nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutumie shehena za mizigo inayopita Bandari ya Dar es Salaam kujenga hoja kwamba Serikali imekengeuka na kufanya maamuzi ama kwa faida za kisiasa, maslahi ya kikanda au urafiki tu wa viongozi na kupiga teke maamuzi kwa vigezo vya faida za kiuchumi. Mwaka 2015/2016, Bandari ya Dar es Salaam ilipitisha mizigo jumla ya tani milioni tano kwenda nchi tunazopakana nazo. Katika mizigo hii, 34% ya mizigo ilikuwa ya Zambia, 34% ya DRC, 12% Rwanda, 6% Burundi na 2.6% Uganda. Lango la mizigo ya DRC na Burundi ni Bandari ya Kigoma (kimsingi kama reli inafanya kazi). Hivyo, Bandari ya Kigoma inaweza kupitisha 40% ya mizigo yote inayopita Bandari ya Dar es Salaam kwenda nchi jirani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lango la mizigo ya Uganda na Rwanda yaweza kuwa Isaka na Mwanza ambayo ni takribani 15% ya mizigo yote kutoka Bandari ya Dar es Salaam. Ikumbukwe kuwa hiyo mizigo ya Rwanda na Uganda ina ushindani wa bandari ya Mombasa (ambapo wanajenga reli kwenda huko) ilhali mizigo ya Kongo DRC na Burundi haina ushindani huo na hakuna reli wala mradi wa reli unaojengwa. Sasa, Serikali itueleze sayansi gani ya uchumi waliyotumia kutumia mabillioni ya fedha za ndani kupeleka reli mahali penye mzigo wa 15% ya mizigo yote na kuacha mahali penye mzigo wa 40% ya mizigo yote?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaweza kujenga hoja kuwa Bandari ya Mwanza itakua lakini ukitazama takwimu za reli utaona kuwa bandari inayokua kwa kasi hivi sasa kwa idadi ya mizigo inayohudumia ni Bandari ya Kigoma. Mwaka 2015/2016, Bandari ya Kigoma ilikua kwa 12% wakati Bandari ya Mwanza ilikua kwa -41.3%. Hizi sio takwimu zangu, ni takwimu za taarifa hali ya uchumi inayotolewa na Serikali yenyewe. Mkurugenzi wa Bandari (TPA), Mhandisi Kakoko ana ushuhuda wa juzi tu msafirishaji Azam Dewji kapata kazi ya kupeleka Kongo DRC tani 120,000 ya udongo ulaya (saruji) kwa mwaka na mzigo huu utapita Bandari ya Kigoma kwa urahisi na wepesi wa kufikisha eneo la mteja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi, Serikali inatumia nini kufanya maamuzi? Ujasiri wa kutopeleka SGR Kigoma kwanza kwa ajili ya faida za kiuchumi unatokana na nini? Serikali inajua nini ambacho sisi wengine hatujui? Njia sahihi yenye faida kwa nchi kwa reli ya kati ni Kigoma-Dar es Salaam na tawi la Uvinza Msongati, Burundi ili kwenda kubeba mzigo wa madini ya Nikeli. Awamu za Serikali hazina mashiko kiuchumi na ni lazima kubadilisha njia na kupeleka reli mahali penye mzigo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili kwenye reli ni hatua za ujenzi. Hivi sasa kazi ya Dar es Salaam-Morogoro imeanza, kilometa 205 kwa thamani ya dola za Marekani bilioni 1.2 (shilingi trilion 2.5). Kipande hiki cha reli kitabeba nini kutoka Morogoro kwenda Dar es Salaam na Dar es Salaam kwenda Morogoro? Mwaka 2016/2017 tumepanga bajeti ya shilingi trilioni moja lakini mwaka 2017/2018 tunapanga shilingi bilioni 900. Hivyo itachukua bajeti tatu kujenga kipande cha reli kutoka Dar es Salaam mpaka Morogoro cha kilometa 205. Hii reli itafika lini huko mtakapotaka ifike na muda huo uwe na uvumilivu wa kiuchumi? Serikali haioni kwamba ingekuwa na faida zaidi kama reli hii awamu hii ingefika Makutupora Dodoma, kilometa 500 halafu TPA wakajenga dry port hapo ili reli ianze kuzalisha mapato kwa kusafirisha mizigo mpaka Dodoma? Rwanda, Uganda, Burundi na DRC wachukulie mizigo yao Dodoma. Najua swali litakuwa ni fedha za kufika Dodoma. Ni lazima Serikali ianze kufikiria nje ya boksi la fedha za ndani na mikopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Ethiopia ilijenga bwawa la kuzalisha umeme 10,000 MW. Benki ya Dunia walikataa kuwapa fedha na China walikataa kuwapa fedha. Serikali ya Ethiopia ikawaambia wananchi wake wajenge kwa kuuza bond kwa wananchi na hasa wananchi wao waishio nje ya nchi hiyo (Diaspora). Serikali iuze railways bond kwa wananchi wa ndani na nje ili ku-finance kipande cha Morogoro – Makutupora sasa hivi. Serikali ilete Muswada Bungeni wa kuiweka bond hiyo kisheria kwa miaka 15 na kupanga/kutenga fedha kwenye bajeti kulipia riba ya bond hiyo mpaka iive ambapo tayari uchumi utakuwa umekua na kumudu malipo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iwafanye Watanzania washiriki katika ndoto yake ya kujenga reli kwa njia hii. Tufikishe reli hii Dodoma na kuwepo na dry port Dodoma kwanza ndiyo tutaweza kupunguza gharama na kuanza kupata mapato kutoka katika mradi, mapato ambayo yataanza kulipia madeni au kulipa ujenzi wa kuelekea Tabora na Kigoma na baadaye Mwanza, Uvinza, Musongati na Kaliua na Mpanda. Hayo ndiyo mawazo yangu, mnaweza kuyachukua ama kuyaacha, lakini nashukuru Mungu nimesema na watoto wetu watakuja kufukua historia na kutuhukumu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho kwenye reli ni uchumi kufaidika wakati wa ujenzi. Miradi mikubwa kama hii huwa ina mikataba inaitwa Offsets Agreeements. Hizi offsets hutumika kwenye miradi mikubwa ya kijeshi na miradi ya kiraia. Tusirudie makosa ya Bomba la Gesi la Mtwara ambapo kila kitu kilitoka China. Serikali izungumze na wakandarasi ili vitu ambavyo vinaweza kutengenezwa hapa nchini viwanda vianzishe kutengeneza vitu hivyo, lazima tutumie miradi hii kutekeleza ajenda yetu ya viwanda. Serikali inaweza kutuambia viwanda vingapi vya ugavi kwenye bidhaa za ujenzi wa reli vitajengwa? Nashauri hili lifanyike kama halijafanyika. Haya ndio mambo ya local content na Serikali lazima kila mwaka ituambie ni makampuni mangapi ya Watanzania yamefaidika na ujenzi wa reli na kwa kufanya kazi gani. Wajerumani walibebesha babu zetu mataruma ya reli, Waturuki walibebesha watu wetu ujuzi na fedha tunayolipa sehemu ibakie humu nchini kukuza uchumi wa nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ni hili la ndege. Leo nimetua uwanja wa ndege wa Dodoma nikitokea Jimboni Kigoma kwa kutumia ndege za ATCL. Hii ni hatua ya maendeleo kwa sababu sikuweza kufanya hivi mwaka jana tu. Ningeendesha zaidi kilomita 800 na kufika nimechoka. Hatua hii siyo ya kubeza bali ya kuungwa mkono. Hata hivyo, suala la manunuzi ya ndege za ATCL linahitaji uwazi mkubwa kutoka Serikalini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana tumetenga fedha za ndani shilingi bilioni 500 kununua ndege na mwaka huu pia kiasi kama hicho. Tumeambiwa kuwa tayari tumelipa 30% ya dola za Marekani milioni 224 kununua Boeng 787 -8 Dreamliner. Jumla ya fedha za ndege kwa miaka miwili ni trilioni moja. Ni maamuzi, hatuna chakula Ghala la Taifa tunanunua ndege. Watoto wanakosa mikopo ya elimu ya juu, tunanunua ndege. Ni maamuzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna habari kuwa ndege tuliyonunua ni sehemu ya ndege za Boeng zilizokataliwa na mashirika mengine duniani kwa sababu ya ubora wake. Ndege hizi zinaitwa Terrible Teens Dreamliner ambazo zilikuwa 12 na zilikosa soko kwa sababu ni nzito na hazina viwango. Wenzetu Ethiopia wamenunua pia ndege hizi lakini kwa punguzo kubwa la bei kwa sababu ndege hazikuwa na soko. Hata hivyo, katika tovuti ya Boeng, Bwana Van Rex Gallard, Vice President, Latin America, Africa & Caribbean Sales, Boeing Commercial Airplanes(http://www.boeing.com/commercial/ customers/air-tanzania/air-Tanzania-787-oder. page) amesema kuwa tumenunua ndege hizi kwa USD milioni 224. Naomba maelezo ya Serikali kuhusu suala hili ili Watanzania wajue kama fedha zao zinatumika vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha na naomba kupata majibu sahihi kuhusu masuala niliyoeleza.