Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchukua fursa hii kwanza kumpongeza Waziri mwenye dhamana ya Ujenzi kwa hotuba nzuri na mtandao mzima wa barabara ambao wananchi wana imani kubwa kwamba Serikali ya Awamu ya Tano inatekeleza mambo mbalimbali kwa ajili ya sekta ya miundombinu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna baadhi ya maeneo nataka nichangie katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri katika baadhi ya maeneo ambayo Wabunge hasa Mheshimiwa Mary Muro, Mheshimiwa Hasna Mwilima, Mheshimiwa Ester Bulaya na sasa hivi Mheshimiwa Julius Kalanga katika suala zima la upelekaji wa fedha za miundombinu ya barabara katika halmashauri zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli wakati mbalimbali kwamba maeneo mengine yamekuwa na changamoto kubwa na ndiyo maana Serikali kwa kipindi kirefu sasa imeamua kubadilisha utaratibu wake wa upelekaji wa fedha kuelekeza fedha nyingi katika Halmashauri zetu. Japokuwa bado hazijatosheleza angalau hali si haba, ndiyo maana hata ukiangalia kitakwimu katika Bajeti yetu ya Mwaka 2010/2011 shilingi bilioni 84 tu ndiyo zilikuwa zimetengwa kwa bajeti ya barabara lakini bajeti yetu ambayo tumeipitisha juzi hapa tumetenga karibu shilingi bilioni 272. Lengo kubwa ni kuziwezesha Halmashauri mbalimbali japo tuweze kuzifungua barabara zile ziweze kupitika vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, najua kwamba changamoto ya mtandao wa barabara za Serikali za Mitaa ni mkubwa hizi fedha hazitoshi, lakini Serikali lazima tutaendelea kuangalia jinsi gani tunatafuta rasilimali fedha kuhakikisha kwamba tunaboresha. Ndiyo maana wakati mwingine tunashirikiana hasa kwa kutafuta funds kutoka hata kwa wenzetu wa World Bank ndiyo maana Halmashauri nyingi sana za Miji hivi sasa mitandao ya barabara imebadilika, ni kwa ajili ya juhudi hizo kubwa sana zinazofanyika, lengo kubwa ni kufungua barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika upelekaji wa fedha, naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba kwa sababu mwaka wa fedha haujakwisha, kwa zile bajeti ambazo zimetengwa katika mwaka huu wa 2016/2017, Wizara ya Fedha itakuwa inafanya harakati za kutosha kuhakikisha kwamba barabara hizi tutaziwezesha ili kazi zetu za barabara ziweze kuendelea vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na hoja ya Mheshimiwa Hussein Bashe ambayo ilikuwa ikizungumzia suala zima la Wakala wa Barabara ambao unaanzishwa sasa hivi vijijini, hoja yake ni kwamba changamoto kubwa ni fedha na jinsi gani tutaanzisha wakala ambapo sasa mgawanyo wa fedha hauko sawasawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ni jambo la kisheria, kwa sababu kwa sheria yetu tuliyonayo ni kwamba asilimia 30 ya fedha hizi zinaenda katika bajeti ya barabara za Halmashauri na asilimia 70 inaenda kwa ajili ya TANROADS, ndiyo maana tumekusudia kuanzisha Wakala lakini jambo hili liko katika hatua za mwisho, ilikuwa ni mapendekezo ya Wabunge humu ndani ya Bunge, basi kama kutakuwa na mawazo mengine tofauti tutatafakari. Lengo kubwa ni kwamba wananchi wetu katika maeneo yao barabara ziweze kupitika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mawazo haya kama michango ya Waheshimiwa Wabunge yote tunayachukua kwa pamoja, jukumu kubwa la Serikali inaangalia jinsi gani itafanya kuhakikisha kwamba barabara zetu zinapitika katika maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na hoja ya Mheshimiwa Ahmed Shabiby, alikuwa akizungumzia suala zima la barabara yake pale Mjini ambapo kulikuwa na ahadi ya kilometa tano na Mheshimiwa Shabiby anasema kweli na ndiyo maana siku ya Alhamisi Mheshimiwa Shabiby anakumbuka tulikuwa Jimboni kwake. Ahadi ya Serikali ni kuhakikisha kwamba barabara ile ya kilometa tano ujenzi unakamilika na ndiyo maana juzi nilivyofika pale Gairo ujenzi wa barabara ile sasa unaendelea. Ni imani yangu kwamba Serikali katika kipindi hiki cha miaka mitano, itafanya kila liwezekanalo ule mtandao ambao ni ahadi ya Serikali, ahadi ya Mheshimiwa Rais aliyoitoa ya ujenzi wa kilometa tano uweze kukamilika katika eneo la Gairo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Balozi Adadi Rajab alizungumzia suala zima la ahadi ya Mheshimiwa Rais ya kilometa tatu pale Mjini Muheza. Naomba nikuhakikishie Mheshimiwa Balozi Adadi Rajab kwamba ile ahadi ya Mheshimiwa Rais ndiyo hivi sasa Ofisi ya Waziri Mkuu ilikuwa inachukua ahadi mbalimbali. Imani yangu ni ndani ya kipindi hiki cha miaka mitano ahadi ile iweze kutekelezeka kwa sababu commitment ya Serikali ni kuhakikisha kwamba ahadi zote hasa za ujenzi wa miundombinu ya barabara ndani ya kipindi cha miaka mitano hii tuweze kuzikamilisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na hoja ya Mbunge, Mheshimiwa Vedasto Ngombale ambaye amechangia nadhani kwa maandishi, Mheshimiwa Bwege naye alizungumzia ile barabara ya kwenda Kilwa Kivinje na mwaka huu kulikuwa na commitment ya shilingi milioni 800 ambayo ipo katika bajeti ya mwaka huu wa 2016/2017. Kwa vile jua halijachwa bado ni imani yangu kwamba zile fedha zitapatikana kwa kipindi hiki kwa kuwa ipo katika mpango huu wa bajeti, bahati nzuri Mheshimiwa Bwege ni kwamba tayari tumeshaingizwa katika bajeti, hivi sasa naamini Wizara ya Fedha, fedha hii ikishatiririka basi tutatoa maelekezo Wakandarasi waingie site haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua kipindi hiki cha mvua hali ni mbaya na nilipokuja kule kwenu nimeona kwamba hali ya barabara ile siyo nzuri zaidi ndiyo maana commitment ya Serikali mwaka huu ilitenga shilingi milioni 800 hizi tutahakikisha kwamba zikishapatikana basi ujenzi utekelezwe katika ubora unaokusudiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na hoja ya dada yangu, Mheshimiwa Bonnah, kuhusu suala la ujenzi wa barabara chini ya Mradi wa DMDP ambao hata wewe unakuhusu katika Jimbo lako la Ilala. Mradi huu utakuwa na takribani shilingi zisizopungua bilioni 600 na nusu na kuendelea, ambapo mchakato wake kweli ilibidi uanze tokea zamani lakini kuna mambo mbalimbali yalikuwa yamekwamisha. Hata hivyo, hivi sasa tupo katika hatua nzuri, Mbunge wa Temeke na Mbunge wa Mbagala, ni mashahidi, mwezi mmoja na nusu uliopita tumekwenda kuangalia ukaguzi wa ujenzi wa barabara hizi hasa utengenezaji wa daraja lile kubwa la Twangoma ambalo lina urefu wa karibu mita 800.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi mchakato huu katika maeneo mengine umekwama ni kwa sababu ya lile jedwali la tathmini. Imani yetu ni kwamba kulikuwa na mchakato hapa, inaonekana hali siyo nzuri sana katika ufanyaji wa tathmini. Jambo lile likikaa vizuri kwa sababu sasa hivi Wakandarasi wameshapatikana, ni imani yangu kwamba ujenzi wa barabara hii sasa utaanza mara moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikuhakikishie, katika Jimbo lako la Ilala nitasimamia kwa karibu zaidi na maeneo yote ya Jiji la Dar es Salaam kuhakikisha barabara zile tunazijenga. Kwa sababu barabara zile ndiyo zitakuja kufungua Mji wa Dar es Salaam nyingine ni feeder roads zinaunganisha katika barabara kuu yetu ya DART, zingine ni barabara ambazo zinapita katika mitaa yetu ya Jiji la Dar es Salaam. Sasa hivi ukiangalia hata mvua ikinyesha mitaro yetu imekuwa ni tatizo, mradi ule unakwenda kutengeneza mitaro, unatengeneza barabara halafu unafanya settlement katika maeneo mengine. Kwa hiyo, naomba niseme kwamba Serikali imeweka commitment katika maeneo haya kuhakikisha mradi huu wa DMDP ambao Wabunge wa Jiji la Dar es Salaam lengo letu ni kuufungua mji ule vizuri, tutakwenda kulifanya hili kwa kadri iwezekanavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kikubwa zaidi naomba niwahamasishe Waheshimiwa Wabunge hasa kwa fedha tunazozipeleka katika Halmashauri zetu, tuzisimamie vizuri, kwa sababu imani yangu kubwa katika maeneo mengine hali huwa inakuwa siyo shwari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja ya Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi. Ahsante sana.