Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mpanda Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze na neno la shukrani. Nashukuru kwa maana ya hotuba ya Mheshimiwa Waziri, taarifa ya kamati nikiamini vyote vimesheheni mambo ambayo macho yanapenda kuona na masikio kusikia. Nikianza na nukuu kama ambavyo wenzetu wa kamati waliitoa ya Mahatma Gandhi, wao waliitoa kwa kingereza lakini mimi nitaitoa kwa tafsiri ya Kiswahili changu mwenyewe kwa maana ya afya ndio utajiri halisi na si vipande vya dhahabu na fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa misingi hiyo nakwenda kuisemea Hospitali yetu ya Manispaa ya Mpanda. Hospitali ya Manispaa ya Mpanda ilianza mwaka 1957 ikiwa kituo cha afya. Leo hii inafanya kazi kama Hospitali ya Manispaa, na kwa misingi hiyo watu wote ndani ya mkoa wanaitegemea hospitali ile, na ndiyo maana sisiti kuishukuru Serikali yangu kwa sababu najua tuko mbioni kutengeneza hospitali ya mkoa na fedha zimekuwa zikitengwa na hivi karibuni tumetengewa shilingi bilioni moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini, Serikali itaendelea kutuangalia kwa jicho la huruma nikiamini sisi tuko pembezoni na tukikosa huduma muhimu za afya tunakuwa pembezoni zaidi. Kwa hiyo, hilo nilikuwa napenda kuliweka katika sura hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hospitali yetu hiyo hiyo, mara ya mwisho alikuja Naibu Waziri. Katika kuitembelea hospitali, alipokwenda kwenye chumba cha upasuaji, nasikitika kusema alikifananisha chumba kile na machinjio; yaani kwa maana kwamba vifaa vilivyomo mle havifanani na vifaa vya chumba cha upasuaji, kwa huduma zote, kama vile utoaji hewa na vinginevyo. Kwa hiyo, mahali ambapo tunakusudia tuokoe maisha ya watu ukifananisha na machinjio Mheshimiwa Waziri unaona kabisa kwamba watu wale wanatakiwa kuangaliwa kwa jicho la huruma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, najua pia kuna changamoto ya upungufu wa dawa. Ni kweli mara ya mwisho alikuja Mheshimiwa Waziri Mkuu akatusaidia tukaanzishiwa duka la MSD, hilo nashukuru maana usiposhukuru kwa kidogo hata kwa kikubwa unaweza usishukuru. Hata hivyo pamoja na uwepo wa duka hilo bado tuna tatizo kubwa la uhaba wa madawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nakumbuka Mheshimiwa Waziri wetu mara ya mwisho aligusia habari ya kuiangalia mikoa ya pembezoni kwa maana ya kupeleka madaktari bingwa. Nilikuwa naomba wazo hilo muhimu, wazo hilo la uokoaji liendelee kuwa katika kichwa chako Mheshimiwa Waziri. Nafahamu tuna ukosefu wa magari na katika hili uungwana tu kama binadamu naomba niwapongeze wale wote waliobahatika kupata ambulance. Hata hivyo wakati nikiwapongeza hao Mheshimiwa Waziri maana yake na mimi natoa shukrani in advance kwa maana najua mgao unafuata na sisi tutafikiriwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, najua Mkoa wangu wa Katavi napata aibu kuhusu suala la mimba za utotoni nikiwa mwakilishi wa wananchi. Tunapozungumzia habari za mimba za utotoni, na kwamba Mpanda ndio wa kwanza katika nchi hii sisi wawakilishi wa wananchi tunayo kazi nzuri kubwa ya kufanya. Nilikuwa naomba hiyo kazi kubwa ya kufanya, kwa maana ya kuwafikia vijana katika kuendelea kutoa elimu katika suala hili na tatizo la mimba za utotoni nahitaji msaada kutoka katika ofisi yako Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeshazungumzia habari ya ujenzi wa hospitali ya mkoa ambayo inahitaji msisitizo na msukumo. Tunacho chuo cha afya, miundombinu yote ya kile chuo ambacho kilikuwa cha zamani imeshafufuliwa, kila kitu kipo katika hatua za mwisho. Rai yangu na ombi langu kwako, Serikali ifanye jitihada kuhakikisha chuo kile kinaanza. Najua ni chuo kwa ajili ya matabibu, lakini ningeomba tukibahatika pia katika chuo hicho hicho tukawa tunatoa na wauguzi tafsiri yake ni nini? Kwanza habari ya mahitaji ya wataalamu hawa itakuwa ni ndoto katika hospitali yetu, nilikuwa naomba hilo tusaidiwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nipongeze, kwenye kitabu chako Mheshimiwa Waziri umeongelea habari ya huduma ya matabibu bingwa. Nafahamu kwa kupitia huduma ya matabibu bingwa kwa Taasisi ya Jakaya Kikwete na kwa MOI, huu ni mwarobaini wa kutusaidia Watanzania kwenda nje ya nchi, mimi hilo nalipongeza sana. Hata hivyo, pamoja na kulipongeza basi maeneo hayo yapewe fedha, na hapa si suala tu la kusema fedha zimetengwa ila ionekane fedha zikipelekwa, nilikuwa naomba kutoa rai hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo niendelee tena kutoa pongezi kwa kupunguza rufaa nje ya nchi. Suala hili ni la msingi, najua ni kwa maana ya kupunguza rufaa ya nje ya nchi kama vile kwa masuala ya kupandikiza figo. Tumeona pale ukizungumzia nje ya nchi ni shilingi milioni 80 lakini kwa shughuli hiyo kufanywa ndani ya nchi inakuwa ni shilingi milioni 20, huu ni msaada mkubwa kwa wananchi wetu. Naamini nchi ya uchumi wa viwanda bila kuwekeza kwenye afya ya watu, rasilimali watu, nguvu kazi ndoto ya uchumi wa viwanda itakuwa mashakani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende kwenye ushauri, lakini wakati nikienda kwenye ushauri kuna suala la dharura...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.