Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

Hon. Suzana Chogisasi Mgonukulima

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

MHE. SUZANA C. MGONOKULIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa kunipa nafasi hii niweze kuchangia jioni ya leo kwenye Bajeti ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa naomba nianze na kundi la walemavu. Ninarudia tena kusema Mheshimiwa Ummy - Waziri wa Afya, matatizo wanayoyapata wanawake wenye ulemavu wakati wa kujifungua bado yako pale pale. Niliongea mwaka wa jana katika Bunge hili lakini wakati nikiwa field huko kwenye majimbo nimekuta wauguzi wengi wanawanyanyapaa sana wanawake wenye ulemavu wakati wa kujifungua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo basi, kwa dhamana ya nafasi yako, hili ulichukue na ulifanyie kazi, wale watakaobainika wanaendeleza vitendo vya kuwanyanyapaa wanawake wenye ulemavu wakati wa kujifungua wachukuliwe hatua za kinidhamu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2011 mpaka mwaka 2012 Hospitali ya Mkoa wa Iringa ilipata hadhi ya kuwa Hospitali ya Rufaa. Tatizo ambalo linaikumba hospitali ile ni ukosefu wa madaktari bingwa. Hitaji la madaktari ni 24, hadi sasa hivi hospitali yetu ile ya rufaa ina madaktari watano, hivyo kusababisha kazi ya kiutendaji ya kuokoa maisha ya wananchi wa Mkoa wa Iringa kuwa ngumu sana. Mheshimiwa Waziri, naomba hili ulichukue kwenye mgawo wako wa madaktari hao wanaopata ajira, basi Madaktari Bingwa uwapeleke kwenye Mkoa wetu wa Iringa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuja kwenye Mfuko wa Bima. Afya kwa wazee wetu wa Taifa hili imekuwa ni tatizo. Serikali imejikita kuwasaidia wazee hawa huduma ya magonjwa ya homa, tumbo, lakini si pale wanapopata magonjwa yale ya moyo, ini, figo, vipimo hivi lazima walipie. Sasa kama Serikali inataka kusaidia kundi la wazee; hivi vipimo nilivyovisema gharama yake ni kubwa; na Serikali haitaki kuwekeza mkono wake, hii huduma ambayo tunasema tunataka kuwasaidia wazee naona sio sahihi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, basi Wizara ichukue jukumu hili kuhakikisha hawa wazee ambao Serikali imesema itawatibia bure, iwe bure ya magonjwa yote hata hayo niliyoyaainisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya Hospitali ya Mkoa wa Iringa kupata hadhi ya kuwa Hospitali ya Rufaa, Manispaa ya Iringa tulijenga Hospitali ya Wilaya ambayo iko maeneo ya Frelimo na inaitwa Hospitali ya Frelimo. Hospitali hii ina wauguzi wakutosha, madaktari wakutosha, kinachokuja kuleta shida ni upungufu wa vifaa tiba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi ninapozungumza sasa hivi hospitali hiyo yenye wauguzi wa kutosha na madaktari wa kutosha haina vifaa vya uuguzi ambapo tumekosa kupata vipimo vya full blood picture, x-ray, ultra sound ambapo ingekuwa vipimo hivi viko pale, hospitali hii ingepokea msongamano wa wagonjwa ambao wanatakiwa kutibiwa pale ili wasiende kutibiwa kwenye hospitali ya rufaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo ningependa nijikite kwenye unyanyasaji wa watoo wadogo wa kike. Sipo sambamba na wachangiaji waliosema, mtoto wa miaka chini ya miaka 18 kuozeshwa na kuwa mama wa nyumba ni makosa makubwa sana kiafya. Kwanza nyonga zake zenyewe hazijakomaa kuweza kuendeleza mambo ya mipango mingine ya kiutu uzima na hivyo tunawafanyia hayo matendo kiunyama kwa sababu tendo la ndoa kwa mtoto wa miaka chini ya 18 hana hisia nalo kwenye akili yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naomba Wizara hii kama sheria inakingana, kuwa haiwezekani kutungwa sheria hiyo, basi tutalazimisha Wizara ya Elimu iweke kiwango cha elimu ya mtoto wa kike ni Kidato cha 12, ili kama itaonekena kuna mzazi yeyote yule ana binti yake ameolewa chini ya miaka 18 aweze kuchukuliwa hatua za kisheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii tutakuwa tumewakwamua kundi la watoto wa kike ambao kwa tamaa za wazazi wao… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. SUZANA C. MGONOKULIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja ya Kambi ya Upinzani