Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

Hon. Devotha Methew Minja

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia Wizara hii muhimu kwa maisha ya Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimefuatilia sana hotuba zote tatu ikiwemo ya Waziri, hotuba ya Kamati na hotuba ya Kambi ya Upinzani. Katika hotuba zote hizi, kila hotuba iligusa kuwapongeza madaktari kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya kwa Watanzania. Tunafahamu kazi yao ni ngumu kazi ya kutetea uhai wa wanadamu siyo kazi rahisi. Kazi ya kuahirisha kifo siyo kazi rahisi ni kazi ambayo kwa kweli inatoka moyoni katika kuhudumia watu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshuhudia madaktari wakifanyakazi katika mazingira magumu, tumeshuhudia wengine hata waki- risk kwenye kazi zao magonjwa, kupata maambukizi, lakini madaktari hawa hawakati tamaa wanaendelea kuwahudumia Watanzania. Kwa kweli, niwapongeze sana madaktari kwa kazi ngumu wanayoifanya. (Makofi)

Pamoja na kazi hii sasa wanayoifanya lakini kuna mambo ambayo tukiyaangalia yanakatisha tamaa. Daktari anafanya afanyavyo kuhudumia wagonjwa walio wengi, lakini inatokea viongozi kama DC, RC anamtumbua hadharani Daktari - DMO akishasikiliza malalamiko ya wananchi kwenye mkutano wa hadhara, anasema kuwanzia leo hana kazi. Nafikiri ifike mahali tuwape moyo watu hawa ambao wanajitoa kwa ajili ya Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, madaktari wana madai yao ya msingi, kwa zaidi ya mwaka mmoja hivi sasa Daktari Bigwa kwenye zile call allowance kwa maana mgonjwa kazidiwa saa nane saa tisa ya usiku analipwa shilingi 25,000 na dakitari wa kawaida analipwa shilingi 15,000. Madaktari hawa kwa zaidi ya mwaka hospitali nyingi hawajalipwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niende kwa Mkoa wa Morogoro. Hospitali ya Mkoa wa Morogoro inahudumia wagonjwa 500 kwa siku na hii ni baada ya hospitali ile kuwa ya rufaa kwa maana inahudumia wagonjwa wanaoshindikana katika Wilaya zake zote. Hospitali hii pamoja na ukubwa kuhudumia wagonjwa 500 ni sawa na wagonjwa 15,000 kwa mwezi, lakini hospitali hii haina x-ray machine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, x-ray machine iliyopo ni ambayo imenunuliwa tangu vita ya pili ya dunia, kwa sababu hospitali ile ilikuwa ya Jeshi. X-ray inagharimu siyo zaidi ya shilingi milioni 100, hospitali hii haina. Wagonjwa wanatoka na drip wanakwenda Mazimbu, wanakwenda hospitali ya Jeshi kwenda kufanya x-ray. Hilo nimelishuhudia mwenyewe na tumefuatilia na tumewahi hata kusema hapa Bungeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa mortuary, hivi leo ndugu yako akipoteza maisha katika Mkoa wa Morogoro utalazimika kumsitiri pasipo hata kusubiri ndugu, kwa sababu mortuary hazifanyi kazi. Kweli kwa hospitali hii ambayo ina hadhi ya kuwa ya rufaa inashindwa kutengeneza tu mortuary kwa ajili ya kuwaifadhi wapendwa wetu ili basi walau waweze kuagwa kwa heshima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee pia suala lingine la Madaktari Bingwa. Tumekuwa na ajali nyingi sana Mkoa wa Morogoro, Daktari Bingwa wa mifupa hakuna, theatre kwa ajili mifupa hakuna, theatre iliyopo ni moja na inategemewa kwa maana ya magonjwa yote, akina mama wanaojifungua ndiyo hiyo hiyo. Watu wenye vidonda ndiyo hiyo watu wa ajali ndiyo hiyo. Nafiki Waziri alitizame kwa namna nyingine suala hili ili kuipa hadhi hospitali ya Mkoa wa Morogoro iweze kuwa na theatre room.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye suala la sakata la madaktari. Serikali ya Awamu ya Nne, kipindi cha nyuma ilikuwa ikihamasisha kwa maana ya ule mpango wa brain bridge kutoka nje, madaktari wetu ambao wamesomeshwa na kwa fedha za Tanzania watoke nje, waje nchini, tena nakumbuka Rais wa Awamu ya Nne, ndiyo ulikuwa mkakati wake wa kuwaomba Watanzania walioko nje warudi hapa nchini watoe huduma kwa Watanzania wenzao. Nakumbuka walikwenda Cuba, Botswana Uingereza na kwingineko na baadhi ya madaktari nafikiri waliitika wito wa Rais wa Awamu ya Nne wakarudi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii cha kushangaza Tanzania ambayo ina upungufu wa madaktari, inawachukua madaktari kwenda kutoa huduma kwa Wakenya. Tumeushangaza ulimwengu kwa hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiangalia daktari mmoja kwa takwimu nimepitia hotuba ya Kambi ya Upinzani kwa vijijini daktari mmoja anahudumia watu zaidi ya 78,000 na nane, kwa mjini anahudumia watu 25,000. Wenzetu Kenya daktari mmoja anahudumia watu 15,000. Leo hii sisi ndiyo wa kupeleka Madaktari Bingwa, madaktari wetu, watoto wetu, waende wakahudumie kuwaponyesha Wakenya wakati wamesomeshwa na kodi za Watanzania! Kuna mahali ambapo tunabidi kukubali kwamba tumefanya makosa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hayo tu, najaribu kuwatizama wale ambao hawakujitokeza kwa maana walikuwa na nia pengine ya kutoa matibatu kwa Watanzania, kuwaajiri madaktari 258 kati ya wale ambao walitahiniwa na kuwaacha wale wazalendo ambao walikuwa na nia ya uzalendo siyo sawa. Nafikiri priority ingekuwa kwa wale ambao walisema wana nia ya kuwatumikia Watanzania zaidi, kubaki nchini na kusaidia Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sera ya Serikali inasema ni kuhakikisha kila kata inakuwa na kituo cha afya, hivi sasa tuna kata zaidi ya 3,900, hospitali ambazo zinamejengwa katika kata hizi ni hospitali 448 ambayo ni sawa na asilimia 11 tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango huu unatekelezeka kwa namna hii? Yako mengi ambayo tunataka kuyajua, flyover ndiyo ni maendeleo, flyover moja ambayo ni shilingi bilioni 100 ni sawa na kujenga hosptali ngapi za Kata? Ni zaidi ya hospitali 250. Priority kwa Watanzania walio wengi ni flyover au ni kupata hospitali ili wapate huduma za afya? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kuhusu suala la upungufu wa vifaa. Ukienda kwenye hospitali kifaa cha kupima wingi wa damu baadhi ya hospitali za private unapata, siyo hospitali za government. Ukienda kupima hospitali za government itakuchukua siku tatu kufahamu wingi wa damu, private ndani ya saa kadhaa unapata jibu, kwa sababu hospitali za government zinazidiwa na wagonjwa, ni kwa nini vifaa hivi muhimu visiwepo kwenye hospitali za government zikaweza kuwasaidia wagonjwa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huwa naliangalia sana suala...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naunga mkono hoja ya Kambi ya Upinzani.