Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CUF
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
HE. RIZIKI S. MNGWALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa fursa na mimi kama ada nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu muumba mbingu na ardhi, aliyetujalia uhai, uzima na afya na akatuwezesha kuwa hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze hapo alipomalizia Mheshimiwa Halima kwa kuzungumzia suala la kunusuru akina mama na vifo wakati wa ujauzito. Mimi nimeogopa kweli labda kwanza nianze kusema naipongeza Kamati ya Bunge husika kwenye Wizara hii kwa ripoti yao hii na naunga mkono hoja hii ya wao walichosema na pia ripoti ya Kambi Rasmi ya Upinzani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukurasa wa 33 Kamati inasema bajeti hii inayoitwa Support to Maternal Mortality Reduction imepungua kutoka shilingi bilioni 13 mpaka shilingi bilioni nane. Mheshimiwa mdogo wangu Ummy ana lile tangazo lake anatoka sana kwenye televisheni “Kama
Halmashauri zinataka kuona kipaumbele cha kunusuru wakina mama watatenga pesa.” Wizara yenyewe inapunguza bajeti, Halmashauri itatenga pesa za kutosha kutosha kutoka wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jamani tuishi yale tunayoyasema, kama kweli tunataka kunusuru akina mama hawa wanaotimiza jukumu la msingi, kweli tuwatengenezee mazingira ya kuwanusuru na tusiwanusuru kwa maneno tu. Hii inauma na haikubaliki, mdogo wangu Mheshimiwa Ummy nakuelewa, nakufahamu na ninakuamini katika utendaji kazi wako, hili lirekebishe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine linaloendana na Halmashauri kubebeshwa mzigo ambao hawauwezi ni haya masuala ya kuhakikisha huduma za msingi kama afya zinatolewa ipasavyo. Ajira zinatangazwa Serikali Kuu, watu wanaomba halafu wanapangiwa kwenye Halmashauri, kisha watu hao wanatakiwa washughulikiwe na Halmashauri. Halmashauri hizi hazina uwezo, mbaya zaidi hii tofauti ya uwezo wa Halmashauri inajenga matabaka ya watendaji wa kada moja katika sehemu mbalimbali za nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nani midwife professional ataenda kukaa Mafia ambako Halmashauri yenyewe hohe- hahe aache kukaa Kinondoni kwenye mabilioni huku? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali Kuu ishughulikie wafanyakazi wa kada hizi nchi nzima. Nurse wa Mafia, nurse wa Kinondoni na nurse wa Ilolangulu huko wote wapate hadhi sawa, kwa maana ya mishahara na stahiki nyingine. Vinginevyo yale maeneo ya pembezoni yataendelea kuwa ya pembezoni na watumishi watatukimbia kila siku. Hili lirekebishwe watu wapate stahiki zinazostahili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mafia in particular jamani ni kisiwa, tena kisiwa kile kilichosahauliwa. Hatuna usafiri wa kuaminika ambao watu wengi wangeweza kutumia wa meli, Hospitali ya Wilaya x-ray hatuielewi na vipimo vingine sijui vitendanishi na vitu gani, mpaka kumpima mama mjamzito kuangalia tu mkojo wake, ile kama sijui kuna vidude gani vingine visivyotakiwa, sukari na vitu vingine hakuna vitu vya kuwezesha kufanya hivyo. Sasa watu hawa wakipata dharura tunawapeleka wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mafia huko hospitali hiyo haijiwezi, majeruhi chungu mzima wanaovunjika, tunawafanya nini? Hata tukimudu kuwatia kwenye ndege, ndege zetu zinazokwenda ni hivi vidogo vya private companies vya eight seaters sijui 13 seaters; kumuingiza mgonjwa mle aliyevunjika mguu au aliyevunjika ni mtihani, angalau maeneo kama haya yangepewa kipaumbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii Serikali inayofanya mambo kwa jumla bila kuangalia specific case kama hizi kwenye masuala kama haya ya afya na mengineyo naona siyo sahihi lazima Serikali ibadilike katika kuweka mipango yake na kutuambia wananchi kwamba kweli wanataka kutupa huduma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilisema kwenye kikao kilichopita tubadilike kwenye budgeting process yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru.