Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

Hon. Azzan Mussa Zungu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ilala

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

3

Ministries

nil

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

MHE. AZZA H. HAMAD: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema na hatimae niko ndani ya ukumbi huu wa Bunge nikiwa na afya ya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuunga mkono bajeti ya Wizara ya Afya kwa asilimia mia moja. Kwa nini naunga mkono bajeti ya Wizara ya Afya? Nitumie fursa hii kuipongeza Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mheshimiwa John Pombe Joseph Magufuli, Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu na Baraza lote la Mawaziri bila kuwasahau Mheshimiwa Ummy na Naibu wake Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla. Mmefanya kazi kubwa ambayo inaonekana kwa muda mfupi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa muda mfupi mmeweza kugawa ambulance 67 katika baadhi ya Halmashauri zetu. Kwa muda mfupi mmeweza kutoa vitanda 20 vya kulalia wagonjwa, vitanda vitano vya kujifungulia, magodoro yake na mashuka 50 kwa kila Halmashauri zetu. Kwa hilo, nawapongeza sana na nawatia moyo pigeni kazi tupo pamoja na ninyi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nirudi katika Mkoa wangu wa Shinyanga, niwasemee wanawake wa Mkoa wa Shinyanga walionileta ndani ya ukumbi huu. Najua Wizara ya Afya hamjengi miundombinu katika hospitali zetu, lakini ndugu yangu Mheshimiwa Ummy wewe ni ndugu yangu sana, kwa hili naomba unisamehe. Pamoja na yote unayoyafanya na pamoja na jitihada zote za ambulance, sijui vitanda na nini kama hamtokaa sawa na TAMISEMI hakuna ambacho kitawezekana. Hivyo vitanda vitakuwa havina pahala pa kuviweka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hilo kwa sababu gani? Miaka mitano iliyopita kila nikisimama ndani ya bajeti hii huwa nasema ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga na suala hili halijawahi kuchukuliwa hata siku moja. Najua siyo la Wizara ya Afya lakini kwa sababu Mheshimiwa Simbachawene yupo hapa na sikupata nafasi kusema TAMISEMI naomba niliseme. Hamtutendei haki Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, tumeanzisha ujenzi kwa nguvu zetu wenyewe, lakini hakuna fedha ambayo tunapewa kutoka Serikalini. Tukipewa fedha tunapewa fedha kidogo, tutamaliza lini ujenzi wa hospitali hii? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeanzisha ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, toka tumeanza kila mwaka tunapewa shilingi bilioni moja, ujenzi huu utakamilika lini? Ndiyo maana ninasema Mheshimiwa Ummy na Mheshimiwa Kigwangalla pamoja na jitihada zote bila kukaa sawasawa na TAMISEMI yote mnayoyafanya hayatakuwa na maana yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaomba pamoja na kwamba ni Wizara ya Afya nitaomba TAMISEMI watujibu ni kwa nini Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga kila mwaka hatupewi pesa kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga inahudumia wagonjwa wengi zaidi kwa sababu Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga na Manispaa ya Shinyanga hatuna Hospitali za Wilaya. Kwa hiyo, inabeba mzigo mkubwa ambao haikustahili kuubeba. Hospitali hii ya Mkoa wa Shinyanga pamoja na kuhudumia wagonjwa wote hao x-ray machine ni mbovu, hazifanyi kazi, kila zikitengenezwa zinaharibika. Kuna kampuni inaitwa Phillips wala hawaonekani kwenda kutengeneza mashine hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapata taabu kidogo, kwa sababu nikienda Hospitali ya Kahama hawana x-ray machine, Hospitali ya Wilaya ya Kishapu hawana x-ray machine na nikienda Mkoani x-ray machine ni mbovu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanawake hawa na wananchi wote wa Mkoa wa Shinyanga wanakwenda kupata wapi huduma za x-ray? Namuomba Mheshimiwa Waziri wa Afya akija atuambie wanaiangaliaje Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga kwa kuiletea x-ray machine mpya kwa sababu hii ni ya muda mrefu na imekwishachoka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hospitali ya Mkoa wa Shinyanga haina vifaa vya upasuaji, ninaiomba Wizara ya Afya, kwa sababu hospitali hii inabeba Mkoa mzima na uzito mnauona, tunaomba Wizara ya Afya mtuletee vifaa vya upasuaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hospitali ya Mkoa wa Shinyanga inaitwa Hospitali ya Rufaa, inapaswa kuwa na Madaktari Bingwa 21, mpaka hivi ninavyoongea ina Madaktari Bingwa watatu tu. Sasa madaktari hawa wanafanya kazi kwa kiasi gani? Ninakuomba sana Waziri utakaposimama utuambie, ni lini mtatuongezea Madaktari Bingwa katika hospitali ya Mkoa wa Shinyanga, kwa sababu hawa waliopo hawatoshelezi hata kidogo. Kinachonisikitisha zaidi katika hawa watatu hakuna hata Daktari Bingwa wa Wanawake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee kuhusu vya vituo vya afya, Mkoa wa Shinyanga tuna vituo vya afya 21, katika vituo hivi ni vituo vitano tu ambavyo vinatoa huduma ya upasuaji. Katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri ukurasa wa 76 nimeona amesema kwa mwaka huu wa fedha wataboresha vituo 150 vya afya kwa kuwa na majengo ya upasuaji. Nikupongeze Mheshimiwa Waziri na watendaji wako wote kwa jambo hili kubwa ambalo mnakwenda kulifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yangu kubwa sasa ni lini utekelezaji huu utaanza? Tunaposema tunakwenda kupunguza vifo vya mama na mtoto ni kupeleka huduma ya upasuaji kwenye vituo vyetu vya afya. Bila kuwa na huduma ya upasuaji kwenye vituo vyetu vya afya vifo vya mama na mtoto vitazidi kuongezeka. Ninakuomba Waziri utuambie hivi vituo 150 ambavyo umevisema kwenye hotuba yako ni lini utekelezaji wake utaanza? Niwashukuru sana lakini niwaombe Serikali iangalie kila mwaka ijaribu kuboresha vituo vyetu vya afya tulivyonavyo ili viweze kutoa huduma zinazostahili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mgawanyo wa watumishi. Nasikitika kusema kwamba mgawanyo wa watumishi hauko sawasawa. Ukienda maeneo ya mijini watumishi unawakuta wako wengi, unakuta labda hospitali inahitaji watumishi labda 30 lakini wapo 50, kwa nini? Hamtutendei haki tunaoishi maeneo ya vijijini. Ninaiomba Wizara na wanaohusika mtuangalie hata tunaotoka maeneo ya vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwa nini watumishi wengi wanakwenda maeneo ya mjini na maeneo ya vijijini tunakosa watumishi. Naomba hili mliangalie kwa makini ili na sisi wananchi wetu waweze kupata huduma zinazostahili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa niongelee kuhusu maendeleo ya jamii. Katika Mkoa wa Shinyanga kuna vituo vya wazee viwili, kituo cha Kolandoto na Usaanda. Bajeti iliyokwisha nakumbuka kuna fedha zilitengwa kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya wazee ingawa hazikuainishwa zinakwenda kujengwa wapi, naomba Waziri akija aniambie, kile Kituo cha Kolandoto ambacho hali yake ni mbaya sana, majengo karibu yanadondoka, Wizara inafikiria nini kuboresha majengo haya ya wazee ambao kwa kweli yanasikitisha na yanatia huruma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba mtuambie maendeleo ya jamii vituo hivi vya wazee mnafikiria lini na fedha zake zipo wapi kwa ajili ya kuwaweka wazee wetu katika mazingira mazuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kusema haya yote nirudi kwenye Mfuko wa Wanawake katika Halmashauri zetu. Fedha zinazotoka maendeleo ya jamii kwenda katika Halmashauri zetu sielewi kidogo ni kwa nini usimamizi wake unakuwa mgumu na mbaya. Kuna fedha zinazotoka Wizarani na kuna fedha zinazotoka Halmashauri, ninawaomba Wizara Halmashauri isipotoa fedha zake za asilimia kumi ya mapato ya ndani msiwape fedha za Wizarani. Kwa sababu mnapokuwa mnawapa fedha kutoka Wizarani ndipo wanapokuwa na jeuri ya kutokutoa ile asilimia kumi ya mapato ya ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na naunga mkono hoja, Waheshimiwa Mawaziri pigeni kazi, Mwenyezi Mungu atawabariki.