Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chemba
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nimshukuru Mwenyezi Mungu Subhanahu Wataala, kwa kutujalia afya njema leo. Nikushukuru wewe binafsi kwa kunipa nafasi hii. Nimshukuru sana Mheshimiwa Rais na kumpongeza kwa kazi nzuri anayoifanya, amefanya kazi nzuri sana kwa muda mfupi sana na naomba aendelee na moto huohuo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikupongeze sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi nzuri unayoifanya na Waheshimiwa Mawaziri wote. Kwa kweli sasa tunaamini kabisa kwamba Serikali iko kazini. Ahsanteni sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa Spika na Katibu wake Dkt. Kashillilah pamoja na Naibu Spika kwa kufanikisha Bunge kuwa na studio yake. Duniani hakuna ambapo Bunge linaoneshwa toka asubuhi mpaka jioni na vyombo vya habari, jambo hili ni zuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nilishangaa kusikia mtu anasema matangazo kutooneshwa ni kuvunja demokrasia. Hao waliotuletea hiyo demokrasia wenyewe hawaoneshi Bunge toka asubuhi mpaka jioni. Sisi tumechaguliwa na wananchi baada ya kwenda kuwaona na kuwaomba kura, siamini kama tulikaa kwenye televisheni na kuwaambia wananchi tuchagueni, turudi huko tukawatumikie. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya pekee kabisa niipongeze sana Timu ya Yanga Afrika wamefanya vizuri sana. Mimi ni mwanachama wa Simba na-declare interest lakini katika mechi yao ya juzi kule Cairo walicheza mpira mzuri sana, walikuwa wanawakilisha Tanzania. Naomba nimpongeze sana Rais wa Yanga Bwana Yussuf Manji kwa kazi nzuri ya kusajili wachezaji wazuri. Huwezi kuwa na wachezaji wabovu halafu unalalamika tunafungwa…
MHE. JUMA S. NKAMIA: Kama hali ilivyo. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimpongeze sana Bwana Manji kwa kazi nzuri aliyofanya na aendelee kuisaidia Yanga Afrika. Naamini katika mchezo wao na Angola wanaweza kupita. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nije sasa kwenye hoja zangu chache, kwanza nianze na suala la kilimo. Sisi Wilaya ya Chemba tuna mgogoro kidogo, si mgogoro in such, bali ni tamaa za watu wachache na wenzetu wa Kiteto. Tunaishi vizuri sana na watu wa Kiteto lakini wapo baadhi ya watu wanatuvuruga sana. Ni wazi kwamba Tanzania unaweza kwenda mahali popote bila kubaguliwa ili mradi tu ufuate sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, wakulima wetu wa Wilaya ya Chemba wanaokwenda Kiteto wengi wamefukuzwa na juzi juzi wakati mimi na Mheshimiwa Ndugai, bahati mbaya hana nafasi ya kusema humu, Mkuu wa Wilaya ya Kiteto kule akasema mimi na Mheshimiwa Ndugai tutamkoma kwa sababu tunatetea haki za wapiga kura wetu. Mheshimiwa Waziri Mkuu hebu liangalie jambo hili vizuri ili wananchi hawa waweze kuishi kwa amani, walime na waweze kufanya kazi zao bila tatizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo ningependa kushauri ni suala la mfumo wetu wa uendeshaji wa Serikali. Tulipokuja kwenye ule mfumo wa D-by-D nashauri turudi tukaangalie upya tena. Huu ugatuaji wa madaraka umefanya baadhi ya mambo hayaendi vizuri kwangu mimi ninavyoona, kwenye elimu na afya ndiko kwenye matatizo makubwa. Leo Waziri wa Elimu hana mamlaka na shule ya kata, Waziri wa Afya akienda Hospitali ya Wilaya hana mamlaka nayo na Waziri wa Habari akienda kule Sumbawanga akawaambia wawe na Maafisa Habari kila Halmashauri hana mamlaka nayo. Kwa hiyo, naomba jambo hili tuliangalie vizuri kwa kufanya marekebisho kidogo ili tupunguze kidogo nguvu ya TAMISEMI iende kwenye Wizara nyingine kazi ziweze kwenda haraka zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kushauri kidogo kuhusu usafiri Dar-es-Salaam. Njia ya kupunguza tatizo la msongamano ni pamoja na Serikali kuhamia Dodoma. (Makofi)
MHE. JUMA S. NKAMIA: Wewe unaweza kusema aah wewe kwa sababu inawezekana fikra zako zinaishia hapa karibu, huoni mbali. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la msongamano wa magari Dar-es-Salaam na hata huu utaratibu wa DART tunaoanza nao siyo suluhisho. Hakuna miji mikubwa duniani kwa watu waliojipanga vizuri hata London, hakuna foleni kubwa pale mjini kwa sababu wametengeneza utaratibu mzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kuhamia Dodoma imeshindikana basi tuanzishe utaratibu kwamba mtu anayetoka Gongo la Mboto akifika Airport kutengenezwe parking mahali aache gari aingie kwenye public transport. Vivyo hivyo kwa njia ya kutoka Bagamoyo, Mbagala, Tabata, tutapunguza tatizo la msongamano wa magari pale Dar-es-Salaam. Naamini jambo hili likifanyika litakuwa limetusaidia kwa kiwango kikubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia hata mfumo wa mabasi ule ambao mmeutengeneza pale Dar-es-Salaam, njia za mabasi zile ziko katikati. Unapotengeneza bus lane katikati pale halafu ni njia moja basi likiharibika katikati pale ya nyuma yatakwenda wapi kwa sababu iko line moja tu! Hebu angalieni vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo nataka kushauri kidogo, amezungumza hapa Mheshimiwa Kessy kwamba wafute hata michezo watu wasiende nje, hapana, mimi napingana naye kidogo. Kwa mfano, Timu ya Bunge kwenda kucheza kwenye michezo ile ya EALA ndiyo ushirikiano wenyewe wa Afrika Mashariki. Nimwombe Mheshimiwa Keissy aje tufanye mazoezi akifanya vizuri na aende kwenye timu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Malocha amezungumzia suala la watu wengi kutopiga kura katika uchaguzi uliopita. Mimi nikupe tu mfano, Wilaya ya Chemba kijiografia ndiyo wilaya kubwa kuliko wilaya nyingine katika Mkoa wa Dodoma, kutoka Kata moja ya Mpendo mpaka kufika Makao Makuu ya Tarafa ni kilometa 64, kutoka mpakani na Kiteto mpaka kufika mpakani na Singida kilometa 275. Nilishangaa kuna wilaya nyingine zilikuwa na Kata nane (8) ama 12 zimegawanywa yakawa majimbo mawili, hata hiyo population yake siyo hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niungane na Mheshimiwa Malocha, tazameni namna gani baadhi ya Wilaya kama Chemba igawanywe yawe majimbo mawili, tuna kata 26, eneo lake ni kubwa kweli. Kuna wilaya sitaki kuzitaja, lilikuwa na Mbunge mmoja sasa hivi kuna majimbo matatu, ndani ya Tanzania Bara, hebu tuliangalie hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho kabisa nataka kushauri kwenye suala la maji, tuongeze nguvu kwenye mabwawa. Sisi tumehangaika na mradi wa maji wa Ntomoko kule, sasa hivi mradi ule hauwezi kufika vijiji vyote 17, tuangalie utaratibu mwingine lakini tuongeze nguvu kwenye kujenga mabwawa. Mfano, Bwawa la Farkwa pale, Mlongia na Itolo pale katikati likitengenezwa bwawa wananchi hawa wataondokana na matatizo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana wewe binafsi na nirudie kusema Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli chapa kazi. Wenzetu sasa ndiyo basi tena kwa sababu hata mgonjwa akiwa mahtuti unajua huyu kesho sijui kama atafika. Sasa baada ya kuisoma namba hata namba sasa hivi kuisoma inakuwa ni shida. Wakati mwingine tulieni, binadamu mzuri hapigi kelele hovyo. Utalalamika sana, kuonekana kwenye TV si hoja, kwani unatafuta mchumba? Wewe unataka uonekane kwenye TV unatafuta mchumba? Unataka wakuone ili iweje, nenda Jimboni! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa anakuja mtu mzima analalamika hapa ndani ya Bunge, TV hazionekani, wewe unataka ya nini?
MHE. JUMA S. NKAMIA: Ndiyo, mbona zamani hazikuwepo TV hizi ulikuwa wapi wewe? Unakuja humu ndani mtu mzima kabisa, tunakuheshimu sana, unasema TV hizi, sasa hivi watu hawaonekani, waonekane ili iweje, nenda kafanye kazi. Mimi nawashangaa tu, kumbe watu walikuwa hawafanyi kazi wanategemea TV, tuonekane hapa ili iweje? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namalizia, naomba kazi hiyo iendelee. Nakushukuru sana Mheshimiwa Spika, Naibu Spika na Katibu wa Bunge kwa kazi nzuri mliyofanya. Sisi wengine ndiyo tulioanzisha mawazo hayo, yamefanya kazi vizuri hongereni sana. Hawa wanaosubiri televisheni waende. Kwa nini usiende kuomba kazi ya utangazaji kama unataka kuonekana kwenye televisheni? Nenda, nafasi zipo tu, TV ziko nyingi tu utaonekana, utapaka poda usoni, tutakuona.
MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naunga mkono hoja.