Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

Hon. Ester Alexander Mahawe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

MHE. ESTER A. MAHAWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi hii na mimi niweze kutoa mawazo yangu katika Bunge lako Tukufu. Kwanza kabisa naomba nitoe shukrani zangu za dhati na pongezi nyingi sana kwa Mheshimiwa Ummy pamoja na Mheshimiwa Kigwangalla. Amezungumza mwenzangu Mheshimiwa Mama Martha Umbulla muda si mrefu ya kwamba juzi tu tuna kama siku mbili, tatu alitoka katika Mkoa wetu wa Manyara kwa sababu ya Hospitali ya Haydom, kwa kweli tunamshukuru sana Mheshimiwa Ummy lakini kubwa zaidi nimshukuru pia na Mheshimiwa Waziri Mkuu ambaye alisema atamtuma Waziri wake kwenda kuangalia jinsi gani Hospitali ya Haydom inaweza ikawa Hospitali ya Rufaa ya Kikanda kwa sababu hospitali hii inahudumia watu wengi sana, inahudumia Mikoa siyo chini ya mitano, ina Wabunge wanaoweza kuisema humu ndani siyo chini ya 20, kwa hiyo hili siyo jambo dogo. (Makofi)

Nimuombe sana sada yangu Mheshimiwa Ummy kwamba ikiwezekana kwa vile ile hospitali iko kijijini, kuna umbali wa zaidi ya kilometa 900 kutoka Haydom mpaka Muhimbili, kuna umbali wa zaidi ya kilometa 400 kutoka Haydom mpaka KCMC, kuna umbali wa zaidi ya kilometa 200 kutoka Haydom mpaka Hospitali ya Mkoa wa Manyara, tunakuomba sana Mheshimiwa Ummy kwa hili acha legacy. Watu wa Haydom, watu wa Mkoa wa Manyara, Arusha kupitia Wilaya yake ya Karatu, Meatu, Simiyu upande mkubwa sana wa Simiyu hawatakusahau, Singida ndiyo usiseme hata Dodoma.

Tunakuomba sana Mheshimiwa Waziri Ummy hospitali hii iweze sasa kufikiriwa kuwa Hospitali ya Kikanda ili kwa ukanda huu tuwe tumepata hospitali ya rufaa ya kuweza kumaliza matatizo ya wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Baada ya pongezi hiso naomba sasa nijielekeze katika pongezi hizo, nisisahau kumshukuru Rais wangu ametoa vitanda kwa kila Halmashauri. Kwa kweli Mheshimiwa Rais Mungu ambariki sana jamani kazi inafanyika, tunaona kwa macho ya nyama, Mungu ambariki sana Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Wilaya yetu ya Babati tuna changamoto mbalimbali, ninaomba tu niongelee kwa uchache hospitali yetu ya Mkoa wa Babati haina theatre inayoeleweka, haina x-ray inayoeleweka, haina haya ultra- sound inayoeleweka, haina wataalam wa radiology, tunaomba sana Mheshimiwa Ummy, tunajua kazi inafanyika, tunajua mnajitahidi sana, lakini penye changamoto lazima tuseme, tunaomba muikumbuke hospitali hii ya Mkoa wa Manyara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tuna Hospitali ya Mrara ambayo inatoa huduma kama Hospitali ya Wilaya pale, tunakuomba sana Mheshimiwa Ummy changamoto nilizozitaja zilizoko katika Hospitali ya Mkoa zipo na kwenye hospitali ya Mrara, tunaomba uikumbuke hospitali hii. (Makofi)

Mheshimiwa Waziri, pia nisisahau kuishukuru Wizara yako Mheshimiwa Ummy umepeleka vifaa vya kutosha na wataalam wa kutosha katika Kituo cha Afya cha Magugu hili lazima tukupongeze sana. Kwa kweli, tunakushukuru sana, tumeona juhudi zenu na pale kwa kweli sasa neno upungufu hakuna, ahsanteni sana kwa hili mlilolifanya pale Magugu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ninaishukuru Serikali kwa sababu sasa inafanya sana kazi nzuri kupitia PPP, tayari imepeleka ruzuku katika Hospitali ya Dareda, hii ni Hospitali ya Mission ambayo inahudumia wananchi wengi sana wa Wilaya ya Babati Mji na Babati Vijijini Halmashauri zote hizi zinasaidiwa sana na hospitali hii ya Dareda, kwa kweli naishukuru Serikali imepeleka ruzuku pale ya kutosha lakini pia inasaidia kulipa watumishi wa kada hii ya afya wa hospitali ile. Kwa kweli kwa ujumla wake, niiombe Serikali iendelee kutoa ushirikiano kwa hospitali hizi za makanisa ambazo kwa kweli ni hospitali teule katika maeneo yetu, zinafanya kazi nzuri sana kutoa huduma kwa wananchi. Hivyo, niipongeze Serikali kwa kukubali kufanya kazi kupitia PPP na hizi hospitali za makanisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika Wilaya yetu ya Babati tuna mapungufu, tuna vituo saba na mahitaji yetu ni vituo 25, tuna zahanati 32 mahitaji ni zahanati 102; tunaomba sana haya mapungufu yatazamwe kwa jicho la kipekee sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashauri kwamba badala ya kuhangaika kuja kuweka labda Hospitali ya Wilaya pale Babati, ningeshauri zile fedha ambazo zilipaswa kuelekezwa kwenye ujenzi wa hospitali, vituo hivi vikiboreshwa vinaweza vikachukua nafasi kubwa sana ya kumaliza tatizo kiasi kwamba hata umuhimu wa kuwa na hospitali ya Wilaya pale unaweza usiwe wa lazima sana. Hivyo, naomba Kituo cha Bashnet, Hospitali ya Dareda pamoja na Kituo cha Mrara hozpitali hizi zikiboreshwa ukweli ni kwamba taabu itakuwa imekwisha maana wananchi hawa watakapokuwa wanahitaji huduma yoyote ya rufaa wataelekea Haydom ambako siyo mbali. Naomba tuboreshe kwanza huku chini ili tuweze kusaidia wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo kubwa pia la hospitali zetu katika Mkoa mzima wa Manyara hatuna ambulance. Kwa mfano, Wilaya ya Simanjiro imesemwa tayari kwamba tuna ambulance moja ambayo ni mbovu kila wakati ipo garage. Tunaomba jiografia ya Mkoa wa Manyara imekaa kidogo ni tatizo. Kwa mfano, Wilaya ya Simanjiro kutoka kata moja kwenda kata nyingine unakuta siyo chini ya kilometa 50 mpaka 80, kwa hiyo tunapokuwa na ambulance ambayo kwa kweli haipo vizuri tunapata shida.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nisisahau pia kuishukuru Serikali, tayari pale Simanjiro tunapanua wodi sasa, huduma ya mama na mtoto inakwenda kupatikana vizuri sana pale Orkesment, ninaishukuru sana Serikali kwa kuliona hili. Pia nisisahau kuishukuru hospitali ya Orkesment ya KKKT, hospitali teule iliyoko pale Simanjiro inaendelea kutoa huduma nzuri kwa wananchi wetu. Niiombe tu Serikali kama nilivyosema kwa sababu gharama kwa kiwango fulani ni kubwa katika hospitali hizi ambazo zina muundo wa hospitali binafsi, ninaomba ile Urban Orkesment itakapokuwa imeboreshwa vizuri na kuwekwa vifaa vyote vinavyotakikana, kwa kweli wananchi wetu watapata huduma bora ya afya pasipokuwa na tatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nizungumze suala sasa la afya ya mama na mtoto - uzazi salama. Uzazi salama ni kitu muhimu sana, kama takwimu zinavyoonesha kwamba akina mama wasiopungua 30 wanakufa kila iitwapo leo. Hii idadi siyo ndogo, tunaomba katika vituo hivi vya afya huduma hii iboreshwe, katika zahanati zetu huduma hizi ziboreshwe. Kwa mfano, katika Wilaya ya Simanjiro, kata ya Ngorika pana umbali wa kilometa 60 kutoka Ngorika mpaka Orkesment. Nilikuwa naomba ikiwezekana ile zahanati iliyoko pale iweze kupandishwa hadhi kidogo, iweze kukaa vizuri ili wale wananchi wa Ngorika waweze kupata huduma pale Ngorika maana kutoka Ngorika mpaka Orkesment mtu anatembea kilometa 60 kwa kweli huu umbali ni mrefu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tulivyosema jiografia ya Simanjiro ni zaidi ya square kilometer 17,000 hiyo Wilaya ni kubwa sana na sehemu kubwa ni pori, kwa hiyo tunaomba msaada wenu sana Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, naomba nizungumzie suala la ndoa za utotoni; vifo vingi vimekuwa vikitokea kupitia ndoa hizi za utotoni. Ninaomba sana ikiwezekana Mheshimiwa Waziri sasa alete marekebisho ya sheria hii huku ndani. Ninawaomba wakina baba mlioko humu ndani, ninawaomba sana akina mama watoto wetu wanateketea. Hii biashara ya kusema kwamba kigezo cha mtoto wa kike kuolewa ni baada ya kuvunja ungo hii siyo sahihi. Siku hizi watoto kwa ajili ya hizi chips, corie na kadhalika wanavunja ungo wana miaka 10, wana miaka 11, wana miaka tisa, hivi kweli mtoto huyo ame-qualify kuwa mke wa mtu?

Jamani akina baba tunaomba mtusaide, hawa ni watoto wenu kama siyo wa kwako ni wa mjomba wako, kama siyo wa mjomba wako ni wa kaka yako, kama siyo wa kaka yako ni wa shangazi yako. Ninaomba katika hili tuungane jamani, tuweke itikadi zetu pambeni, tunafahamu mambo mengine ya kidini yapo humu na imani za watu tunaziheshimu, lakini ili kuokoa nafsi hizi za watoto wa kike tunaomba basi tushirikiane kwa pamoja ili kwamba watoto wetu waweze kupona. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante naomba niunge hoja kwa asilimia mia moja.