Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

Hon. Maria Ndilla Kangoye

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

MHE. MARIA N. KANGOYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nami nianze kwa kuunga mkono hoja na sina mashaka na Serikali yangu ya Awamu ya Tano kwa kazi nzuri inayofanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja kwa moja nianze na suala zima la udhibiti wa UKIMWI. Napenda kuipongeza Wizara kwa juhudi nzuri inazofanya kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya afya. Hata hivyo, kumekuwa na tatizo kubwa la watoto wanaozaliwa na maambukizi ya VVU. Kwa mujibu wa Kanuni ya Maadili, watoto hawa hawapaswi kupimwa bila idhini ya wazazi. Mara nyingi wazazi hawa wamekuwa hawawapi taarifa ya status zao watoto hawa na tatizo linakuja pale ambapo watoto hawa wanaingia katika mahusiano katika umri mdogo wakiwa shuleni ama mitaani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, takwimu zinaonesha kwamba lipo ongezeko kubwa la watoto kujihusisha na ngono katika umri mdogo. Napenda kutumia fursa hii kuiomba Serikali ije na programu nzuri ambayo itawawezesha watoto hawa kuweza kujitambua na kufahamu ni namna gani ya kuweza kujilinda wao pamoja na wengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia kuhusu tatizo la hedhi isiyo salama. Kumekuwa na tatizo kubwa sana la hedhi zisizo salama ambalo limekuwa likiwaandama sana wasichana na wanawake ambao wako vijijini lakini na wale ambao hawana uwezo wa kupata taulo salama. Changamoto hii imesababisha matatizo mengi yakiwemo magonjwa mbalimbali yanayotokana na kutumia zana ambazo sio salama kipindi hicho cha hedhi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kama mdau mmojawapo wa hedhi salama na napenda ku-declare interest kwamba ni mzalishaji wa taulo ambazo zinatumika zaidi ya mara moja na mara nyingi nimekuwa nikijitolea kutoa bure sehemu mbalimbali ikiwemo mashuleni na magereza. Napenda kuiomba Serikali yangu kuungana na sisi wadau ili pale inapowezekana iweze kutoa pedi hizi kwa makundi mbalimbali yakiwemo ya wafungwa wanawake, wanawake wasio na uwezo lakini pia kwa watoto wa kike ili kuweza kupunguza tatizo la utoro wa shuleni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba moja kwa moja nijielekeze katika Mkoa wangu wa Mwanza. Kwanza napenda nianze kwa kumkumbusha Waziri ahadi ambazo ametuahidi, ipo ile ahadi ya kutuongezea OC katika Hospitali ya Sengerema ambapo OC inayokuja kwa ajili ya vitanda ni ndgo mno kulingana na hali halisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumkumbusha pia Mheshimiwa Waziri ahadi yake ya vitanda katika Kituo cha Afya cha Malya. Alimuahidi Mbunge wangu wa Sumve na sisi tunasubiri ahadi hiyo itimie kwa sababu akina mama wanahangaika sana, wanajifungulia chini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Wilaya ya Magu nitaongelea Kituo cha Afya cha Kisesa, ni kituo ambacho kinahudumia takribani kata tano na tarafa nzima ya Sanjo. Kituo hiki kina uhitaji mkubwa wa x-ray na chumba tayari kimeshaandaliwa vizuri kwa ajili ya mashine hiyo. Hivyo basi, tunaiomba Wizara itushike mkono tuweze kupata mashine hiyo ili wananchi wa Tarafa ya Sanjo wasipate tabu kwenda maeneo ya mbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Ilemela haina Hospitali ya Wilaya. Kwa juhudi ya Halmashauri imeweza kuanza kujenga jengo la OPD. Tunaishukuru Wizara kwa kuweza kuchangia shilingi milioni 300 kwa ajili ya jengo hilo ambalo lina thamani ya zaidi ya shilingi milioni 600. Hata hivyo, bado safari ni ndefu, hospitali nzima gharama yake ni shilingi bilioni 25, hiyo ni kwa ajili ya majengo pamoja na vifaa. Tunaomba sana Wizara ituangalie ili wananchi wa Ilemela wapungukiwe na matatizo ya kwenda katika misongamano ya wagonjwa katika Hospitali ya Bugando pamoja na Sekou Toure.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naunga mkono hoja.