Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CHADEMA
Constituent
Bukoba Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. WILFRED M. LWAKATARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
Kwanza kabisa nitumie fursa hii kuwapa pole wananchi wa Mkoa wa Kagera na hususan Bukoba Town ambao majuzi usiku wa kuamkia tarehe 30 Aprili waliweza kupata tena mshutuko wa tetemeko ambalo tunamshukuru Mungu kwamba tetemeko hilo halikuweza kuleta athari kubwa zaidi ya kuongeza nyufa katika nyumba ambazo zilikwishapata nyufa pamoja na kuangusha kuta ambazo watu waliambiwa waanze kujenga wenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichoweza kuwaombia ni kwamba nawaomba wawe watulivu na kuondoa hofu huku wakisubiri ripoti ya wataalam ambao tumeahidiwa kwamba watakwenda huko na hasa baada ya hoja yangu humu ndani ya Bunge na Mheshimiwa Waziri Muhongo kuweka kalenda kwamba timu hiyo itakwenda kule tarehe 17 kuweza kuwasilisha ripoti, pamoja na hayo amefanya uugwana ametanguliza advance party ya kufanya maandalizi na kuwaondoa watu hofu katika Mji wa Bukoba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tetemeko ambalo lilitupiga mnamo tarehe 9 Oktoba, 2016 liliacha athari kubwa. Naomba Mheshimiwa Waziri wa Afya na Naibu wake watambue kabisa kwamba zahanati nne pamoja na vituo vya afya viwili vilisambaratishwa kabisa. Baada ya Mheshimiwa Rais kutembelea Mkoa wetu na mji wetu na akavunja ile Kamati akitumia usemi kwamba hata kamati za harusi huwa zikakuwa na mwisho wake, jukumu la kuendelea kupokea michango na kuendeleza kazi zilizokuwa zinaendelea liliachwa kwenye kitengo cha maafa husika ambacho kiko chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati huo shughuli nzima za Kamati ya Maafa zinasitishwa tayari vituo hivi kamati ilikuwa imeitengea shilingi milioni 380 kwa ajili ya ukarabati, tayari kwa zahanati za Buhembe pamoja na Rwamishenye tayari matofali yalishasombwa na kuwekwa pale, lakini tangu Rais alivyotoa maagizo yake na Kamati ile ikasitishwa kazi yake na shughuli zikarudishwa kwenye kitengo husika, ni kwamba zaidi ya matofali hakuna ambacho kimeendelea hadi hivi sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, zahanati hizo pamoja na kituo cha afya bado viko katika hali ile ile, nitaomba Mheshimiwa Waziri aliangalile hili ili wananchi wa Bukoba Mjini waweze kutendewa haki na Serikali yao. Jamani hatujiombei maafa hili naomba litambulike, ni tatizo tu la kuwa katika mkondo wa majanga ya Kimataifa ndiyo kitu kinachotuletea matatizo. (Makofi)
Kwa hiyo, tutaomba kabisa Mheshimiwa Waziri unapohitimisha ulijue hilo na kama unatenga mafungu yaende yakasaidie kwa kazi ambayo haikuweza kukamilika mtusaidie wananchi wa Bukoba. (Makofi)
Mheshimwa Mwenyekiti, pili natambua kabisa ni utaratibu na sera ya Serikali na hasa na mwenzangu alizungumza hii ni Ilani la Chama cha Mapinduzi kwamba kila Wilaya inapaswa kuwa na hospitali ambayo ni ya ngazi ya Wilaya.
Katika Mji wa Bukoba tayari hospitali hii ilishaanza kujengwa jengo kubwa la ghorofa moja, lakini jengo hilo limeendelea kutumika kama OPD kwa sababu hospitali hii ya Manispaa haina theatre, haina pharmacy, haina jengo la utawala wala haina majengo ya madaktari; yaani ni jengo hilo moja tu. Huko nyuma kipindi cha mwaka mmoja uliopita katika bajeti, tulielekezwa kuwasilisha maombi maalum ambayo tuliahidiwa kupewa shilingi bilioni mbili kwa ajili ya kuendelea kuimarisha hospitali hii ya Wilaya. Nasikitika kuzungumza kwamba mpaka dakika hii fedha hizo hazijawahi kuletwa.(Makofi)
Mheshimwa Mwenyekiti, mwaka huu nimeona kabisa katika mafungu ambayo yananuiwa kuelekezwa huko ni bilioni mbili tena. Naomba safari hii Serikali itutimizie haki hiyo ituletee fedha hizo na ikiwezekana iongeze fungu ili jamani wananchi wa Bukoba Mjini muwaangalie kwa jicho la huruma kabisa. (Makofi)
Mheshimwa Mwenyekiti, jambo la tatu, Mkoa wa Kagera na Hospitali yetu ya Mkoa kwa utaratibu unaoeleweka ndani ya Wizara ile ni Hospitali ya Rufaa. Nitaomba Mheshimiwa Waziri utusaidie na Watanzania wote wajue kupitia hili, hivi hospitali inapoitwa Hospitali ya Rufaa tunaomba kujua ipaswa kuwa na sifa zipi? Maneno tu ya kuita Hospitali ya Rufaa isiwe ni kigezo ya kuwa rufaa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka huko nyuma hata Serikali iliwahi kuingia kwenye mtego huo kila taasisi ikawa inageuzwa Chuo Kikuu, lakini baadaye Serikali ilikuja kujitafakari zaidi ikaondoa utaratibu huo.
Mheshimwa Mwenyekiti, nafikiri suala hili la Hospitali ya Rufaa inabidi tulitendee haki sawa na huduma inayopaswa kutolewa kama hospitali za rufaa. Sidhani kama suluhisho la timu kuifunga timu nyingine ni kupanua magoli, nafikiri suluhisho huwa ni kufundisha soko ndiyo unapata magoli kupanua magoli sidhani kama ndiyo solution ya kujua kama timu inaweza kucheza mpira. (Makofi/Kicheko)
Mheshimwa Mwenyekiti, ninaomba wakati wa maafa ya tetemeko yalipotokea kupitia kwa Mkuu wa Mkoa kwa niaba ya kamati ya maafa na wananchi wa Mkoa wa Kagera, aliomba at least CT-Scan kwa sababu wakati wa athari za tetemeko wagonjwa wengi waliopata athari ilibidi wapelekwe Bugando, Mwanza, kwa sababu ya kukosa baadhi ya vipimo. Tunaomba hiyo ahadi tuliyoahidiwa kwamba Hospitali ya Mkoa italetewa CT-Scan kwa njia ya dharura, nitaomba Mheshimiwa Waziri wakati unahitimisha hotuba yako usingoje tuende kwenye mafungu kuzibiana mishahara, hii ahadi ya CT-Scan mnatuletea?
Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi umeona tena tetemeko lingine, hivi mnataka tuwe wageni wa nani kama Serikali inatuahidi, haitekelezi kile ambacho imekuwa imetuahidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba wakati unahitimisha hotuba yako hili suala ulizungumzie ili wananchi wa Kagera na Mji wa Bukoba kwa ujumla waweze kupata hope na Serikali yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa lisemwalo lipo kama halipo linakuja. Mheshimiwa Waziri akina mama wanaojifungua wameanza kuwa na wasiwasi kwa baadhi ya matukio yanayotokea bila Wizara au Mamlaka husika kutoa taarifa za haraka au kutoa statements.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Temeke inasemekana kuna mama mmoja alijifungua mapacha halafu pacha mmoja akayeyuka kinamna namna, mambo haya yamewahi kuwa reported kwamba kuna vitendo vya kuiba watoto. Kuna wafanyakzi wanafanya deal la kuiba watoto wanaozaliwa. Tutaomba kupitia kwako hebu waondoe akina mama wasiwasi wanaojifungua, warudishe imani na hospitali zetu, waache kujifungulia vichochoroni kwa sababu ya kukwepa kwamba wataibiwa watoto. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia.