Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

Hon. Tunza Issa Malapo

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Awali ya yote naunga mkono hoja ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Afya napenda kuzungumzia Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Ligula. Hospitali ile imepandishwa kuwa ya Rufaa ya Mkoa lakini jambo la kusikitisha sana tena naomba mnisikilize na Mheshimiwa Kigwangalla nilikufuata nikakuuliza lakini haukunipa majibu. Hatuna mtaalam wa x-ray wa uhakika, vijana wetu wanapopata matatizo ya kuvunjika miguu na kadhalika, ni kama sawa mtu anaendelezwa kwenda kutiwa kilema, kwa sababu karibu watu wengi wanaofungwa mikopa (P.O.P) pale wanaopata tiba za mifupa hakika tiba zile siyo za uhakika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kusikitisha zaidi inabidi watoke kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa waende Ndanda ama Nyangao bila Rufaa kwa sababu zile ki-rank ni ndogo kuliko hii ya Rufaa ya Mkoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba mtuangalie, mmeipandisha hadhi sawa tunashukuru, lakini tukienda kwenye wodi ya wazazi vitanda ni vichache mno, mtu ametoka kwenye uchungu wa kujifungua anaambiwa alale kitandani watu watatu. Nina uhakika ninachokizungumza, nilikaa pale wiki mbili namuuguza wifi yangu hali iko hivyo, haijalishi huyu mtu kajifungua kwa operation, ama kajifungua kawaida. Kwa hiyo, tunaposema hali ni mbaya ninamaanisha hali ni mbaya kwa sababu ni kitu ambacho nakijua nanime- experience. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu duka la MSD la Kanda ya Kusini linaenda kujengwa Ruangwa kwenye Jimbo la Waziri Mkuu, sina shida na hilo. Shida yangu kubwa iko wapi, kama kweli mnakujua Ruangwa, Ruangwa ni ndani barabara ile ya kilometa 45 kutoka Nanganga kwenda Ruangwa ni ya vumbi na kipindi cha masika hakufikiki. Barabara ile na Jimbo la Ruangwa lipo ndani haliunganiki zaidi na Wilaya zingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini duka hili lisikae Masasi ambako ni centre mtu wa Tunduru analikuta, mtu wa Mtwara analikuta, mtu wa Lindi na anayetoka Newala analikuta, kwa nini lisikae pale mkaamua kwenda kulipeleka kule? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kama mnaona kabisa ni lazima liende likakae Jimboni kwa Waziri Mkuu, mtengeneze zile kilometa 45 za barabara ili kusudi watu wanapoenda kuchukua madawa wasihangaike. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu dawa za watu wenye ulemavu wa ngozi. Siku ya maadhimisho ya wanawake nilienda shule ya msingi Masasi ambayo inatoa elimu jumuishi. Nimewakuta watoto pale takribani 39 wenye ulemavu wa ngozi, wana ari ya kujifunza lakini yale mafuta hawapati.

Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri ninakuomba muwafikirie watoto wale ili nao wapate haki yao ya elimu. Pia kuna watoto wenye uoni hafifu na ambao hawaoni kabisa lakini vifaa vya kujifunzia vya kutosha hakuna, hivyo wanashindwa kupata haki yao ya elimu vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Afya nafikiri mna jukumu la kuhakikisha watoto wale wanapata haki yao ya elimu vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Wilaya ya Mangaka ambayo inahudumia Nanyumbu. Hospitali ile imepandishwa hadhi kuwa ya Wilaya lakini haina x-ray. Kwa hiyo, naomba katika mpango wako Mheshimiwa Waziri, basi ufanye kila linalowezekana ili x-ray ile ipatikane iweze kuwahudumia watu wa Nanyumbu na majirani zao. Tunasema afya kwanza ili twende kwenye mambo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba ya Waziri ukurasa wa 76 amezungumzia suala la kuhakikisha wodi za watoto wachanga zinaanzishwa katika hospitali zote za rufaa. Namuomba Mheshimiwa Waziri suala hili lisiwe kwenye makaratasi na maneno… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)