Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CHADEMA
Constituent
Tunduma
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa
Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii. Nichukue fursa hii kwanza kuwashukuru sana watumishi wa Wizara hii nikianza na Katibu Mkuu wa Wizara pia madaktari pamoja na wauguzi wote nchi nzima kwa kazi kubwa wanayoifanya katika mazingira magumu ambayo wanayo. Ninawapongeza sana kwa moyo wao na kwa kazi kubwa wanayoifanya na uzalendo wanaouchukua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze moja kwa moja kuhusu suala la wazee; nimesikitika sana kuona kwamba suala la wazee katika nchi hii inaonyesha kabisa ni suala ambalo siyo kipaumbele cha Taifa hili, ukijaribu kuangalia hata kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri kuna mistari karibu mitano tu inayozungumzia suala la wazee na halieleweki ni namna gani Serikali imeweka mikakati ya kuhakikisha kwamba inatatua tatizo la wazee kukosa huduma muhimu kama za afya na huduma zingine zinazohitajika kwa wazee hawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la wazee ni suala muhimu sana. Humu ndani ya Bunge kuna wazee ambao sasa hivi siyo muda mrefu na wao watastaafu na watakwenda kuungana na wazee walioko mitaani. Pia na sisi vijana tunajua kabisa kwamba siyo muda mrefu tutakuwa wazee na baadae tutakwenda kuungana na wazee wengine walioko mitaani huko. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Taifa lolote ambalo halitawathamini wazee Taifa hilo ni lazima litakuwa na mapungufu makubwa na haliwezi kupata baraka za Mwenyezi Mungu. Ni lazima wazee hawa tuhakikishe kwamba tunawaheshimu na tunawatengenezea mazingira mazuri, ninaamini kabisa wazee hawa wamelitumikia Taifa hili kwa nguvu zao zote, kwa jasho na damu na mpaka sasa hivi wameishiwa nguvu zao wanahitaji msaada wa Serikali, lakini Serikali haijaweza kuonesha mpango thabiti kabisa wa namna gani wanaweza kuwahudumia wazee hawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kuangalia kwenye takwimu za wazee, Serikali imetambua wazee karibuni 346,889, wazee hawa ni kati ya wazee asilimia 60 waliotambuliwa, lakini wazee waliopata vitambulisho, wanaopata matibabu na huduma zingine ni wazee 74,590 tu na wazee 272,299 bado hawajatambuliwa na hawapati huduma zozote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekaa inasema kwamba inataka kuwahudumia wazee, hatuhitaji huduma za kwenye makaratasi, tunahitaji huduma ambazo wazee watakwenda kuzipata na wazee hawa waweze kupata vibali haraka iwezekanavyo ili waweze kupata huduma na waweze kunufaika na Taifa ambalo wamelipigania kwa muda mrefu.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni kuhusiana na vifo vya mama na mtoto. Suala hili katika Taifa hili limeonekana ni jambo la kawaida tu. Tunakuja humu katika Bunge tunazungumza, bajeti zinatengwa na bajeti zinazotengwa ni kidogo sana, lakini fedha hizi haziendi kwa wakati na fedha hazipatikani kabisa. Akina mama wanaendelea kupoteza maisha, watoto wanaendelea kupoteza maisha, Taifa limetulia wanaona kama ni jambo la kawaida wanazungumza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii Taifa hili takwimu zinaonyesha kati ya vizazi 100,000 vifo ni 556 na hivi vifo ni kati ya akina mama wanaokwenda kwenye vituo vya afya na hospitali asilimia 64, asilimia 36 ambao hawajagusa kabisa katika vituo vya afya na hospitali hawa hawatambuliki kabisa ni wangapi wanaopoteza maisha. Kwa hiyo, tuna janga kubwa katika suala hili, tunaona Serikali haijaweka mkazo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Waziri anakuja kujaribu kutoa ufafanuzi wa mwisho atueleze Serikali ina mkakati gani, hatuoni vipaumbele muhimu ambavyo Seriakli inavichukua. Leo tunanunua ndege lakini watu wanapoteza maisha, Serikali haiangalii namna gani inaweza kuwahudumia wananchi hawa, Serikali inawakumbuka Watanzania hawa wakati wa uchaguzi, lakini baada ya kupata madaraka inawasahau na wananchi wanaendelea kufa, hakuna mkakati wowote ambao unaonekana kwamba ni wa kuwaokoa watoto pamoja na akina mama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nataka kujua, kwa nini Serikali hii haitaki kuona kwamba ni muhimu hospitali zetu zote za mikoa zikapata CT Scan, nataka hospitali zote za mikoa ziweze kupatiwa CT Scan.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna MRI, hospitali zetu zote za Mikoa zinatakiwa kupata MRI pamoja na CT Scan, kinachoonekana sasa hivi ni kwamba huduma hizi zinapatikana baadhi ya maeneo tu na zimekuwa na gharama kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, leo mgonjwa anakwenda kupima mgongo, anakwenda kupima kichwa kwenye MRI atatumia zaidi yashilingi 700,000 na kwenye CT Scan anatumia zaidi ya shilingi 200,000 mpaka 150,000 gharama ni kubwa, Serikali haijaonesha thabiti kuweka ruzuku katika matibabu haya, inaonyesha kabisa kwamba Serikali inafanya biashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Serikali itueleze ni namna gani inaweza ikahakikisha kwamba inapunguza gharama ya vipimo hivi ili Watanzania waweze kupata vipimo vizuri na waweze kutibiwa sawa sawa. Kwa hiyo, jambo hili tunataka wahakikishe kwamba linafanyika haraka iwezekanavyo.
Mheshimiwa Mwenyekiri, pia kuna suala la kuhakikisha kwamba hospitali zote za Wilaya na hospitali zote za kanda ambazo zingeweza kujengwa katika nchi hii, ukichukua gharama za ndege moja ya Bombadier inaweza ikajenga hospitali ambazo zina hadhi ya Ocean Road karibu kanda zote katika nchi hii, leo hiki siyo kipaumbele cha Serikali, wananchi wanakufa kwa cancer, wananchi wanakufa kwa magonjwa haya na tumesikia takwimu hapa inaonesha kwamba miaka inayokuja kati ya miaka 2020 kutakuwa na vifo vingi sana vya watu ambao wanaweza wakapoteza maisha kwa ajili ya cancer.
Serikali ijaribu kuangalia ni namna gani wanaweza wakapunguza matumizi kwenye maeneo ambayo hayastahili na wakapeleka kuokoa maisha na roho za Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tunajaribu kuendelea kushauri kuhakikisha kwamba mambo haya yanafanyika haraka iwezekanavyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuokoa vifo vya akina mama na watoto, tumeangalia ni namna gani Serikali ilivyojipanga. Hiki ambacho kimeoneshwa hapa kwamba kinaweza kikasababisha upungufu wa vifo vya akina mama na watoto, tumeona siyo sababu sahihi. Sababu sahihi zilizopo ziko takwimu mbalimbali ambazo zinaonesha, ukiangalia katika nchi hii, hospitali za Wilaya zilihitajika 139, leo kuna hospitali 119, kuna upungufu wa hospitali 20 katika Wilaya zetu nchi nzima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia vituo vya afya vilihitajika 4,420 leo kuna vituo 507, kuna upungufu wa vituo 3,913. Kwa hiyo, vituo karibuni 3,913 havipo mpaka sasa hivi katika nchi hii. Ukiangalia zahanati zilizokuwa zinahitajika ni 13,545 leo kuna zahanati 4,470, kuna upungufu wa zahanati 8,075.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huwezi kupunguza vifo vya mama na mtoto kama hatutasogeza huduma hizi kwa wananchi katika vijiji vyote nchi nzima na Wilaya zote tuweze kujenga hospitali za Wilaya ziweze kukamilika. Hivyo, tunafikiri ni vizuri Serikali ikajaribu kuangalia vipaumbele hivi muhimu kwa ajili ya kupunguza vifo vya akina mama na watoto katika nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo tunajiuliza sana kama Watanzania, sijui kama Tanzania imekuwa ni nchi ya majaribio ya dawa za malaria. Kila zikifika ndani ya mwaka mmoja tunapata matangazo kwamba dawa hii haifai kwa matumizi ya binadamu inatakiwa iachwe na inaletwa dawa nyingine. Sasa tunataka wakati Mheshimiwa Waziri anakuja kuzungumza hapa atueleze ni kwanini Tanzania imekuwa kama ni nchi ya majaribio ya dawa ya malaria, atueleze wakati wanatangaza kwamba dawa hii haihitajiki na haifai kwa matumizi ya binadamu ni Watanzania wangapi wanakuwa wameathirika na nini ambacho kinaendelea ili kuokoa athari ambazo zimewapata Watanzania hawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na dawa moja ambayo ilikuwa inatumika hapo nyuma, dawa ya chloroquine, dawa hii imefanya kazi kwa kipindi kirefu sana, ilikuwa inaokoa sana vifo vya akina mama kwa sababu pia walikuwa wanatoa kama chanjo kuhakikisha kwamba akina mama hawapati malaria kama kinga, leo dawa ile imefutika na hatuelewi ni utafiti gani ambao ulifanyika, Watanzania wanataka kujua utafiti uliosababisha dawa ya chloroquine ikaonekana kwamba haifai. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna jambo lingine la upungufu wa madaktari katika nchi hii. Imeonesha kwamba katika nchi hii kuna upungufu mkubwa sana wa madaktari, nataka kukuhakikishia kwamba nchi hii imesomesha madaktari wengi sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda katika nchi za Kusini na Kati mwa Afrika, wanaofanya kazi karibuni asilimia 20 na 30 ni Watanzania wanafanya kazi katika hospitali zile. Ukienda katika nchi za Botswana, Congo, Mozambique na maeneo mengine, wanofanya kazi za kuwatibu wale watu ni Watanzania na hawa Watanzania wanaofanya kazi kule wametumia fedha kubwa kabisa ya Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuweza kumfundisha daktari mmoja haipungui karibu shilingi milioni 10. Madaktari hawa wametumia resources za nchi, lakini leo wanafanya kazi katika nchi zile, juzi tumesikia Mheshimiwa Rais pamoja na Wizara wameamua kuwachukua madaktari wetu kuwapeleka Kenya, jambo ambalo limekuwa ni jambo la kusikitisha na kushangaza wakati tuna upungufu mkubwa wa madaktari nchini. Ahsante.