Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Geita
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niwe mchangiaji katika mjadala unaoendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa, napenda kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa Hotuba yake nzuri iliyosheheni matatizo ya Watanzania ambayo tumekuwa tukilia kwa siku nyingi. Tunakutia moyo tunasema endelea na moyo huo, Watanzania wanaona. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze pia Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anayoendelea kuifanya ya kutumbua majipu na Watanzania wanaona. Napenda kumshauri kama atapata taarifa hizi aangalie hata kwenye Vyama vya Upinzani na kwenyewe kuna majipu ambayo yanatakiwa yatumbuliwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka Bunge la Kumi na Moja Mheshimiwa Lusinde alichangia hapa akasema Chama cha Upinzani kikishindwa zaidi ya mara tatu kinageuka kuwa chama cha kigaidi. Nakubaliana na Mheshimiwa Lusinde kwamba hawa ndugu zetu wanakoelekea sasa ni kutengeneza ugaidi kwenye nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivyo kwa sababu sina hakika kama mawazo aliyoyasoma Mheshimiwa Kiongozi wa Kambi ya Upinzani ni ya Wabunge wote. Kama ni ya Wabunge wote, Wabunge wote wa Kambi ya Upinzani mtakubaliana na mimi ile hoja yangu ya bhangi tuitafutie muda tuijadili. Niliwaambia humu kuna wateja, sababu ya kuwabanabana wanavuta bila kipimo, wanakuja humu wana stata zimezidi kipimo. Sina hakika kama haya mawazo ni ya watu wote ama ni ya mtu mmoja aliyevuta bila kipimo. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini unaona hata hali halisi ya Kambi ya Upinzani ilivyokaa, ndugu zangu watu wa Upinzani, hebu tumieni akili zenu mlizotumia kuwaomba watu kura kule mkaletwa humu ndani. Mnadanganywa mnatoka kwenye mada, mtu anasimama hapa anasema eti kwa sababu Kiongozi wa Kambi ya Upinzani amesema bado anafikiria naomba kuchangia hiyo ndiyo hoja yangu, hayo ndiyo yamekutoa kwenye Jimbo kukuleta humu Bungeni? Watu wako wana njaa, wana shida ya maji, umeme, madawati, Mawaziri hawa hapa wewe unazungumza suala la Kiongozi wa Upinzani, ana nini humu ndani? (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana tukubaliane na hii hali kwamba yale maneno ya Mheshimiwa Lusinde yanaenda yanatimia. Ukiangalia hata Wapinzani waliobaki humu ndani sasa hivi ni wale waliokosa tu nafasi, ni wana CCM walioingilia dirisha la pili, wanajiandaa kurudi humu ndani. Tukubaliane na hii hali, hawa wenzetu hawana hoja, walikuja na hoja ya CUF ya Zanzibar wamepigwa bao.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Wewe kaa chini. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, walikuja na hoja ya Zanzibar, hoja ya Zanzibar tumewashinda…
MWENYEKITI: Mheshimiwa Musukuma keti. Haya taarifa....
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na namshukuru mkomavu wa kisiasa ambaye pia anajua kuzisoma Kanuni vizuri. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea kuwasifu baadhi ya viongozi wa upinzani, Waheshimiwa Wabunge kama Mheshimiwa Profesa J, unaonesha uvumilivu wa hali ya juu. Wewe kwa sababu ni kioo cha jamii ningeomba uachane na mawazo ya kufundishwa ukipata nafasi changia, wasanii wanakutegemea humu ndani, usitegemee mawazo ya kuambiwa na wenzio hawa wazoefu hutarudi. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa niende kwenye hoja yangu ya msingi. Nataka kuchangia baadhi ya mambo ambayo Mheshimiwa Waziri Mkuu ameandika humu ndani kuhusiana na matatizo yaliyoko kwenye Majimbo yetu. Kwanza ni kuhusiana na suala la TV. Naipongeza Serikali na uongozi wa Bunge, Jimbo langu halina umeme, tulikuwa tunatumia generator kuangalia Bunge na toka mmezuia Bunge vijana sasa wanashinda mashambani. Endeleeni na mpango huu na ikiwezekana vipindi vya Bunge vioneshwe hata saa sita wakati wa kupumzika ili hata usiku kuwe na kazi zingine za kufanya wakati ambao watu wana nafasi. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niishauri Serikali, kumekuwa na kasi ya kutumbua majipu watendaji wa Serikali, tunaipongeza sana Serikali, lakini hatutumbui vyanzo vinavyosababisha wafanyakazi wetu wa Serikali wanakuwa wezi. Nataka kutoa mfano, kuna mkandarasi anaitwa JASCO ambaye amesababisha Mkuu wa Mkoa wa Bariadi akasimamishwa na Mkurugenzi na Mhandisi wakafukuzwa lakini yeye akaachwa palepale kwa kuiba shilingi bilioni 19. Sasa amehamia Geita ana mkataba wa shilingi bilioni tano kwa kilometa tatu, ana mkataba wa shilingi bilioni sita kwa kilometa mbili, ana mkataba wa shilingi bilioni kumi na nne kwa kilometa thelathini na nane na bado anafanya kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri watu kama hawa kwenye kasi ya wakati wa Waziri Magufuli alikuwa anazifuta hizi kampuni. Tutamaliza watumishi wetu kuwaacha wafanyabiashara wenye uwezo wanawashawishi watendaji wetu kwa pesa, wanawapa mikataba ambayo ni mibovu. Tunawajua kabisa wamefanya hayo Bariadi leo amehamia Geita na tunawaacha wanaendelea kufanya kazi. Je, tunasubiri tena kwenda kufukuza Mkuu wa Mkoa na Wakurugenzi? Kwa hiyo, nashauri kwamba tuchukue hatua kabla mambo hayajawa mabaya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilizungumza kipindi kilichopita kuhusiana na suala la ulinzi kwenye Jimbo langu. Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba utuonee huruma. Ukiangalia kwenye taarifa Jimbo langu nadhani sasa hivi Tanzania ndiyo tunaongoza kwa kukatwa mapanga. Nilisema kila mwezi wastani wa watu wanne wanakatwa mapanga. Leo tunavyozungumza nurse kavamiwa hospitali kakatwa mapanga. Kwa mwezi wanakatwa mapanga siyo chini ya watu wane.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo lililopo kwa wananchi wa Jimbo langu, kutoka kilipo kituo kikuu cha Polisi Geita ambako kuna usafiri ni zaidi ya kilometa hamsini. Unapopiga simu Geita gari kufika kwenye eneo la tukio inachukua zaidi ya saa moja kulingana na hali ya miundombinu. Pengine kuna njia gani mtufundishe na sisi ambao ni Wabunge wageni tuweze kuwaona Mawaziri mtupe Kanda Maalum. Wakati Rorya watu walikuwa wanaibiwa ng’ombe mkatoa Kanda Maalum na gari, sasa kwetu binadamu wanauawa wanne kwa mwezi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilizungumza humu Mheshimiwa Masauni akasema mwezi mmoja tuangalie tunapata magari sijaona mpaka leo. Mheshimiwa Waziri Mkuu labda mnataka mpaka msikie na Mbunge amekatwa mikono ndiyo mlete helikopta? Naomba mlipe kipaumbele Jimbo langu kwani kwa hali ilivyo sasa tunahitaji kupata gari kwa dharura ambalo litafanya doria kukamata wakata mapanga, pengine wahame basi hata warudi Mikoa ya Kusini huko na ninyi muweze kupambana nao huko. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapiga kelele sana kuhusu suala la maeneo ya kuchimba Geita. Nimeona humu amesema ameongeza ruzuku, Mheshimiwa Waziri Mkuu imekuwa ni porojo. Ndugu yangu Mheshimiwa Kalemani nataka nikwambie uliahidi mara ya tatu juzi akiwepo Waziri Mkuu kwamba tarehe 16 utaachia magwangala hujaachia. Sasa nakusubiri ukivuka feri labda upae na helikopta hutapita pale Geita, tutakusubiri, tutahakikisha tunakupeleka kwenye magwangala wewe ukawe ni mmoja wa waathirika kama wale vijana wanaopigwa mabomu bila sababu kwa kusikiliza kauli yako.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Kitu kizuri huwa hakina mjadala na ndiyo maana umeona wenzetu wale wamekimbia. Hotuba ya Waziri Mkuu inajitosheleza tunachotakiwa sisi ni kuisimamia na tuko tayari kuisimamia na ndiyo maana hata Wapinzani wanakwambia wanakwenda kujipanga. Hakuna cha kujipanga, hiyo ni dalili ya kukwambia Mzee uko safi, endelea na spidi hiyo hiyo na ikiwezekana geukia na upinzani utumbue majipu maana hata kwao kuna ufisadi mkubwa tu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka, Mheshimiwa Sabodo walionesha kwenye TV, aliwasaidia shilingi milioni mia mbili na kiwanja Mwenge, mkasema mnajenga Chuo cha Viongozi wa Vyama vya Upinzani, kiko wapi hata tofali hazipo na hela ziko wapi? Kwa hiyo, tuangalie hata kwenye Vyama vya Upinzani. Kama mnataka kuiga siasa ya kweli ya kuwasaidia Watanzania, hii ndiyo mlikuwa mnaililia miaka yote kasi ya jet, nendeni mkajifunze kwa Magufuli na kwa Waziri Mkuu na timu nzima ya Mawaziri, sasa hivi tuko vizuri, mjiandae 2020 kurudi CCM.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.