Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kasulu Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. AUGUSTINE V. HOLLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, nishukuru kwa kunipa nafasi hii angalau niweze kuchangia kidogo kwenye Hotuba ya Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, niungane na wenzangu kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, lakini pia na Waziri Mkuu pamoja na Baraza lake la Mawaziri kwa kazi nzuri ambayo wanaendelea nayo na kasi ya hapa kazi tu ambayo sifa zake zimetamalaki Tanzania nzima lakini pia na nje ya nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, binafsi nilishukuru sana kuona kwamba barabara ya Kidahwe - Nyakanazi imewekwa kwenye kipaumbele, Malagalasi hydropower ipo na Kiwanda cha Sukari - Kigoma Sugar nacho pia kimepewa kipaumbele. Najua haya yatakuwa ni chachu ya maendeleo katika Mkoa wetu wa Kigoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuzungumzia suala la umeme wa REA. Naomba Waziri mwenye dhamana husika, Mzee wangu Mheshimiwa Profesa Muhongo, lakini pia Naibu Waziri wake, suala la umeme wa REA katika Jimbo langu la Kasulu Vijijini bado utekelezaji wake siyo mzuri, ni wa kusuasua. Nashukuru sana Naibu Waziri alifika Jimboni kwangu pale tukaweka mikakati mizuri lakini napenda kumkumbusha tu kwamba, bado utekelezaji siyo mzuri na aweze kusukuma kuhakikisha kwamba umeme wa REA unafika kwenye Jimbo langu la Kasulu Vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, upande wa mapato, nipende kuipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa namna ambavyo imeendelea kuongeza kukusanya mapato kila mwezi. Napenda kuwakumbusha kwamba mpakani kule bado zipo fedha zinapotea. Jimbo langu limepakana na nchi ya Burundi, kule wako watu ambao bado wanaingia pasipo kutozwa ushuru formally. Pia fedha zingine zinaishia kwa wajanja wachache ambao ni Maafisa. Kwa hiyo, ni bora sasa, Wizara husika ikaenda kuweka pale utaratibu wa namna ya kukusanya fedha zile ambazo zitakuja kusaidia Halmashauri yetu lakini pia na nchi nzima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimdokeze Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI, Mzee wangu Mheshimiwa Simbachawene kwamba pale Kasulu bado kuna majipu, nakuomba sana utue mahali pale. Ripoti ya CAG mwaka jana ilionyesha upotevu wa shilingi bilioni 5.9, lakini mpaka leo hakuna kitu ambacho kimefanyika kushughulikia watu ambao walihusika na upotevu ule. Watumishi walikuwepo lakini pia na viongozi wa halmashauri walikuwepo. Kwa hiyo, ni vyema Mheshimiwa ukatua pale kwa ajili ya kushughulikia watu hawa ili fedha zile ziweze kuja kuwasaidia wananchi wa Jimbo la Kasulu Vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kilimo. Mheshimiwa Mwigulu, wananchi wanakusubiri sana Jimbo la Kasulu Vijijini uende ukamalize tatizo au mgogoro wa pori la Kagerankanda. Wananchi kwa muda mrefu sana hawana maeneo ya kutosha kwa ajili ya kilimo kwa sababu tu ya uwepo wa hifadhi ya pori la Kagerankanda ambalo kimsingi ukiangalia uhitaji wake sio mkubwa. Nadhani mipaka ile ilichorwa zamani wakati ambapo uhitaji wa ardhi haukuwa mkubwa. Kwa sasa kimsingi hatuwezi kuendelea kufuga miti ile ilhali watu wanakufa na njaa. Kwa hiyo, nikusihi sana Mheshimiwa Waziri uweze kufika pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia Bunge lililopita Mheshimiwa Waziri ulisema kwamba, Wabunge tuje hapa tuseme ni lini tunahitaji mbolea za ruzuku ziweze kufika Jimboni kwetu. Naomba niseme kwamba Jimbo la Kasulu Vijijini tunahitaji tupokee mbolea ya ruzuku mwezi wa nane kila mwaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo, nipende kusisitiza tu kwamba, Watanzania wa Jimbo la Kasulu Vijijini wanayo imani kubwa sana na Serikali ya Awamu ya Tano na wana imani kubwa sana na kasi ambayo inakwenda nayo. Niwatie nguvu sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, hizi mbwembwe ambazo unaziona hapa, watu kugomea kuchangia na kususia vikao vya Bunge, hizi sarakasi tu wanajaribu kupanda kichuguu wakati mvua imenyesha, ni suala la kisikitisha sana. Nadhani hata Watanzania wanashuhudia nini kinatokea. Watu ambao waliwachagua kwa ajili ya kuja kimsingi kuwasilisha matatizo yao na kuyashughulikia wakisusia vikao mahsusi ambavyo vingeenda kutatua matatizo yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda niwashauri ndugu zangu Wapinzani lakini pia na uongozi wa Bunge hebu tumshauri Mheshimiwa Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni akae chini atafakari aone kama nafasi ya kuwa Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni bado inamfaa, ajipime vizuri. Kwa sababu ukiangalia namna ambavyo anaendesha kambi hii ni kinyume kabisa na matarajio ya Watanzania ambao wanahitaji maendeleo kwa nchi yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge wa Upinzani napenda kuwashauri kitu kimoja, nimesikia wakiitwa majina mengi sana ambayo mengine siyo mazuri kuyataja, lakini suala la kuja kujipanga kugomea mipango madhubuti ya kwenda kutatua matatizo ya wananchi, kujipanga kuchafua Serikali ambayo inakwenda kwa kasi ya ajabu, kujipanga kukwamisha maendeleo kwa namna yoyote siyo tabia ya kibinadamu ni tabia ya kinyama kabisa ambayo inafaa kulaaniwa na watu wote wanaopenda maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, najua wako watu ambao wakati mwingine wanalazimishwa kufikiria kinyume na vile ambavyo wanaamini kwa sababu tu labda kiongozi amesema, wanalazimika kufuata vile ambavyo wameelekezwa. Tabia hii wako wanyama ambao kiongozi akitangulia bila kujua anaelekea wapi, anaelekea shimoni, anaelekea mtoni au kiongozi wa wanyama wale anaelekea kwenye miiba, anaelekea kuliwa na mamba, wao huunga mkono na kumfuata nyuma, wanyama hawa wanaitwa nyumbu. (Makofi)
KUHUSU UTARATIBU
MWENYEKITI: Kuhusu utaratibu.....
MHE. AUGUSTINE V. HOLLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru tu sana na nisingependa muongeaji anifanye nikaenda mbali zaidi kwa sababu kama ni kuminya demokrasia wao ni vinara na hayo yamejidhihirisha wazi, hata kupitia kwenye Kamati za LAAC na PAC ambapo wajumbe wako wa Upinzani na wa CCM lakiniā¦
MHE. AUGUSTINE V. HOLLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na nina imani muda wangu umeulinda vizuri maana wanajaribu kunitoa kwenye mstari ili nisiseme kile ambacho nataka kukisema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niseme tu kwamba hapa ni Bungeni na kila mtu kaja kwa kura ambazo amepewa na wananchi na kila mtu anao uhuru wa kusema. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikumbushe tu jambo moja kwamba wako watu ambao wakati mwingine wanajaribu kukuondoa kwenye kile ambacho unahitaji kuzungumza, labda niachane nayo hayo. Tuko hapa mbali na kuzungumza namna ya kuleta maendeleo ya kiuchumi ya nchi yetu lakini pia lazima tuweke sawa ili kuhakikisha kwamba tunalinda misingi ya demokrasia na kuikuza vizuri na hatimaye nchi yetu iwe katika nafasi nzuri sana katika nyanja ya demokrasia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mengi nimeyazungumza hapa lakini itoshe kusema kwamba naunga mkono hoja vizuri kwa asilimia 100 na Serikali ya Awamu ya Tano iendelee kuchapa kazi vizuri na wana CHADEMA wakubali wajumbe wa PAC na LAAC watoke CUF bila kinyongo chochote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.