Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Flatei Gregory Massay

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbulu Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ili na mimi nichangie hoja hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kabla sijasahau na muda haujakwisha nipongeze hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Kwa kweli imelenga kila mahali na kwa mimi mwenyewe nimekosheka kwa maana ya kwamba imegusa maeneo mengi sana. Pia nimpongeze sana Mheshimiwa John Pombe Magufuli kwanza kwa kasi aliyoanza nayo na pia kwa kazi anayofanya, kwa kweli maarufu sana kwa kutumbua majipu. Sisi wanyonge na maeneo ambayo kimsingi tulikuwa tumesahaulika sasa tunaanza kupata ahueni ya kupata maisha bora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niwapongeze Mawaziri ambao wamekuja kwenye Jimbo letu la Mbulu ambalo lilisahaulika kwa muda mrefu sana. Nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Lukuvi, Waziri wa Ardhi kwa kusaidia kutatua matatizo au mgogoro wa ardhi ulioko katika Bonde la Yaeda Chini kule eneo la Wahadzabe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia nimpongeze Mheshimiwa Ummy Mwalimu pamoja na Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla kwa kuja kuisaidia Hospitali ya Haydom ili iweze kupandishwa kuwa Hospitali ya Kanda ambapo inaweza kuhudumia Mikoa yetu ya Arusha, Manyara, Singida, Simiyu na Meatu. Pamoja na pongezi hizi kwa kweli niwapongeze Mawaziri wote wanaofanya kazi na kwenye kasi hii ya hapa kazi tu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo kwa kweli naomba nizungumzie kwenye sekta ya miundombinu. Tunayo barabara moja kubwa sana kule Nyumbani ya Mbulu - Karatu- Haydom – Singida - Mbuyu wa Mjerumani – Mbulu - Dareda-Dongobesh. Barabara hii ni muhimu sana kwa ajili ya mawasiliano ya Wilaya ya Mbulu Vijijini ili kukutana na Hanang na Katesh. Barabara hii inahitajika sana kwa wananchi wa Jimbo la Mbulu Vijijini, Mbulu Mjini, Katesh, Babati, Mkalama na kwenye Majimbo ya Singida ili kupata mawasiliano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Hospitali ya Haydom kwa sasa ni ya rufaa na ina wataalam wa kutosha barabara hii inahitajika sana ili iweze kufikiwa na watu wetu wa maeneo haya niliyoyazungumzia wapate tiba. Kwa kuwa Mheshimiwa Waziri alinijibu kwenye swali langu nililouliza Bungeni Na.76, kwenye Bunge la Februari kwamba, ataweka kwenye Mpango ili barabara ile itengenezwe kwa kiwango cha lami, naomba kwa kweli azingatie hili ili wananchi wa Mbulu Vijijini na maeneo niliyoyataja waweze kupata mawasiliano. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninalo jambo moja la kushauri Serikali. Kuna taasisi mbili za RITA na NIDA. Ili kubana matumizi, nadhani taasisi hizi mbili zinafanya kazi moja, kwa sababu RITA inasajili vizazi na vifo na NIDA hali kadhalika inafanya kazi hiyohiyo. Ni vyema basi ili kupunguza matumizi ikafanywa kuwa taasisi moja katika hali ya kubana matumizi ili Serikali ipeleke pesa kwenye maeneo mengine kwa ajili ya maendeleo. Huu ni ushauri wangu kwa Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nizungumzie suala la umeme. Suala la umeme ni jambo ambalo limezungumziwa sana na Wabunge wengi. Nimuombe Mheshimiwa Waziri, Mbulu tangu kumekucha yaani imezaliwa 1905 sawa na Nairobi lakini kwa masikitiko yetu Mbulu umeme umepatikana mwanzoni mwa miaka ya 90 kwenye Kata moja ya Haydom lakini mpaka leo haujasogea kijiji hata kimoja. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri kwenye REA III tafadhali angalia sana Mbulu ili mtusaidie Mbulu tuondokane na tatizo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata leo hii ukiwaambia wananchi wa Mbulu waangalie TV wataionea wapi, umeme katika kata 18, kata tatu tu ndiyo zina umeme. Kama Mheshimiwa Joseph Musukuma alivyosema, leo hii hata nikiongea hapa hawawezi kuniona labda wawashe jenereta. Naamini katika mpango wa Serikali na kasi hii, umeme utafika kwenye Vijiji vyetu vya Endadubu, Masieda, Endanyawish, Endanaichan na maeneo mengi ambayo kwa kweli hata nikiyasema leo naona kabisa napoteza wakati lakini nina hakika Mheshimiwa Waziri ananisikia na nimeshampelekea orodha ya Vijiji vya Mbulu ambavyo havijapata umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia nizungumzie suala la mawasiliano. Kama unavyojua mawasiliano yanahitajika sana kwa ajili ya kuwasiliana na wananchi wetu. Sisi kule ni wakulima wa vitunguu swaumu ambavyo vinakwenda hata nje ya nchi kama vile Uarabuni na maeneo mengine mengi. Kule kwetu wamekuja watu kutoka Zanzibar kwa sababu biashara hii inauzika lakini tuna shida ya mitandao ya simu maeneo ya Tumati, Dongobesh, Maretadu na maeneo mengi hasa ya Masieda basi tungeomba Mheshimiwa Waziri aone maeneo haya hasa Kata ya Tumati kutupatia minara michache ili walau tuweze kuwasiliana na watu wetu. Mimi kama Mbunge wa Mbulu Vijijini nikitaka kuwasiliana na wananchi wangu kutoka hapa siwezi mpaka nifike manually niweze kuzungumza na watu wangu kule. Kwa hiyo, naomba sana Waziri wetu wa Ujenzi na Mawasiliano alione hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina jambo la kushauri kuhusiana na suala la michezo. Mimi ni mwanamichezo, napenda ku-declare interest. Mbulu ni Wilaya ambayo ilikuwa inatoa wanamichezo wengi sana hasa maarufu ambao wamevunja historia na kuweka rekodi katika Olympic hasa kwa michezo ya riadha. Ndugu Filbert Bayi anatoka Mbulu, Gidamis Shahanga anatoka Mbulu, John Bura anatoka Mbulu, hawa wote wameweka rekodi ya dunia. Kwa hiyo, nishauri hivi vyama vya michezo viangalie wapi hasa historia ilipo ili viisaidie Tanzania iweze kujulikana Kimataifa kama ulivyokuwa miaka ya 70. Hii inawezekana kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Nape ni rafiki yangu sana najua ananisikiliza katika hili. Kambi nyingi zimewekwa mijini, nature ya Mbulu inafanya vijana wengi waweze kujiingiza katika michezo na waweze hakika kuzinyemelea hizo medali, sasa hivi Tanzania ni vigumu sana kushinda katika jumuiya yoyote hata Olympic kwa sababu tu michezo mingi imewekwa mijini, mtukumbuke na kule. Wananchi na vijana wa Mbulu wamenituma niwaeleze hili ili muweke kambi kule, historia ya akina Filbert Bayi haijavunjwa mpaka leo, rekodi yake ya dunia iko pale. Ni vema tutafute na kuinua vipaji vya kina Filbert Bayi na wengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hotuba nzuri sana ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, nimpongeze rafiki yangu msanii mwenzangu Profesa Jay na wenzake ambao wamebaki humu. Kwa kweli huu unaonekana ni uzalendo wa kutosha. Nawapongeza na Wapinzani wengine ambao wamebaki hapa. Sina sababu ya kusema sana kuhusu upinzani lakini najua dozi wamepata na wanaelewa nini maana ya kubaki na kuendelea kuzungumza, kusikiliza na kuchangia hoja hii.
Naomba tuwe na kitu kimoja tu kinachoitwa uzalendo. Uzalendo hauwezi kuonekana katika vyama vyetu, unaonekana katika mtu kufanya jambo. Ndiyo maana nimekupongeza Profesa Jay kwa sababu najua tulipotoka, tulikuwa tunaimba mimi na wewe unakumbuka (huku akiimba madawa bangi ni saa utajiri kuuchuma mashangingi) mambo kama haya, leo tupo Bungeni. Kaka usitoke hapa, ukitoka mwanangu kule watakuchimbia mbali na mimi Flatei si unajua mwana sarakasi sitoki hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kumkumbusha tu kwamba na yeye aangalie, kwa nini nasema haya? Leo hii tunatakiwa kufanya kitu kinachoitwa maendeleo katika Majimbo yetu, leo hii TV kule haionekani ni vizuri tukashauriana humu ndani, tukitoka hapa nenda Jimboni watakuangalia. Muombe Waziri hapa akifika kule atakusaidia umeme utakwenda na maji yatakwenda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijielekeze kwenye maji. Jimbo langu la Mbulu Vijijini tuna miradi mitatu ya maji ambayo imefadhiliwa na Benki ya Dunia. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri wa Maji nadhani ananisikia, miradi ile ya World Bank imesimama, naomba basi tusaidie iongezee pesa ili miradi ile iweze kutekelezeka wananchi wa Haydom, Bashay na maeneo ya Masieda na Dongobesh waweze kupata maji ili yale maji tuyatumie katika kilimo na kilimo kiweze kuwapatia wananchi wetu faida. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, najua muda wangu nao umeanza kusogea sana. Mwisho, naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Mkuu Majaliwa, ni Waziri wa kwanza kwa miaka 10 iliyopita amefika Jimboni kwangu akiwa Naibu Waziri, hakuwahi kutokea Waziri mwingine mpaka awamu hii imekwisha. Nakushukuru sana umefika kule na sasa basi nawashukuru Mawaziri ambao wanategemea kufika na wengine wameniahidi kufika katika Jimbo la Mbulu. Ni kweli barabara yetu haipitiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi mimi na Mheshimiwa Jitu tulisukumwa na wananchi baada ya mvua kunyesha. Walipojua tunakuja Bungeni wakasema basi tuwatoe hawa kwenye matope ili wafike Bungeni, tulitumia saa tano kutoka kule kuwahi hapa Bungeni kutokana na jinsi miundombinu ilivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sitaki kuendelea sana lakini kubwa zaidi nataka kuonesha tu umuhimu wa kuiona na kurudi Mbulu na Wilaya ile ni kongwe. Haya maeneo matatu niliyoyasema naomba mtusaidie sana Serikali. Kwa nini nasema haya ni kwa sababu naona uchungu. Mimi ni mjukuu nimekuja huku, alikuja Sarwatt, Marmo na Akunaay sasa kumbuka mimi ni mjukuu nimekuja kuwaambieni Mbulu muiangalie kwa jicho la pekee sana. Mbulu ni Wilaya mama imezaa Hanang kwa Mama Nagu, imezaa Babati kwa mtu anayeitwa Jitu, imezaa Babati Mjini kwa mtu anayeitwa Pauline Gekul na imezaa Karatu kwa mtu anayeitwa Willy. Jamani, sasa leo wote hao wana lami wana kila kitu, wana umeme, Mbulu kata tatu, mtuonee huruma jamani, hatuna hata kipande cha kilometa moja cha lami. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema kabisa kwa asilimia mia moja, naunga mkono hoja hii ili Serikali ifike Mbulu ikanifanyie haya. Ahsante sana.