Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

Hon. Kiteto Zawadi Koshuma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

MHE. KITETO Z. KOSHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata nafasi ya kuchangia kwa maandishi Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuchangia vifo vya mama na mtoto katika Mkoa wa Mwanza ambavyo ni asilimia 21 kitaifa. Idadi hii ni kubwa sana. Vifo vya uzazi kwa asilimia 37 hutokana na kutokwa damu nyingi wakati wa kujifungua, hivyo kama mama asipowahishwa hospitali hupoteza maisha, na hii husababishwa na vituo vya afya kuwa mbali. Vilevile asilimia 21 ya vifo vya wajawazito hutokana na kuchelewa kufanya maamuzi ya njia ya kujifungua hususan upasuaji wa kupanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Mwanza pia una upungufu wa vituo vya afya vinavyotoa huduma ya upasuaji. Hivyo, tunaiomba Serikali ituongezee vituo vya afya vyenye huduma za upasuaji hususan Wilaya za Ukerewe, Sengerema na Magu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake. Mfuko huu utengewe fedha ili kusaidia Halmashauri kuwakopesha akina mama kwa kujumuisha na asilimia tano ya mapato ya ndani ya Halmashauri. Kwa kufanya hivyo, akina mama watakuwa wamewezeshwa kiuchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua fursa hii kuzipongeza Halmashauri za Mkoa wa Mwanza ambazo zimefanikiwa kutenga na kupeleka fedha kwenye vikundi vya akina mama zikiwemo Halmashauri za Ilemela, Sengerema, Mwanza Jiji, Kwimba, Misungwi na Buchosa. Niiombe Wizara
husika kufuatilia Halmashauri ambazo hazikutoa fedha hizo kama vile Halmashauri za Ukerewe na Magu na kuzitaka Halmashauri hizo kupeleka fedha hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia niongelee suala la Benki ya Wanawake. Benki hii ilianzishwa ili kusaidia akina mama kukopesheka kwa riba nafuu, lakini benki hii haitengewi fedha za kutosha kama alivyoahidi Mheshimiwa Waziri Ummy wakati akihutubia kwenye maadhimisho ya sita ya wanawake duniani 2016, kwamba Wizara itatenga shilingi bilioni mbili kila mwaka lakini katika mwaka huu imetengwa shilingi milioni 69 tu. Naiomba Serikali itenge fedha ya kutosha ili benki hii iweze kukopesha kwa riba ndogo ya asilimia 10 mpaka 12 na pia kuongeza matawi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia Serikali iangalie suala la CT scan katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando kwani inategemewa na mikoa ya jirani kama Kagera na Mara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni mimba za utotoni; hizi pia zinachangia vifo vya mama na mtoto. Niiombe Serikali ilete marekebisho ya Sheria ya Ndoa ili kusaidia watoto wanaoolewa na umri mdogo na hivyo kupelekea mimba za utotoni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja.