Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ushetu
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ELIAS J. KWANDIKWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuunga mkono hoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Ushetu lina vituo vya tiba 27 na linahudumia wananchi zaidi ya 300,000 kulingana na sensa ya mwaka 2012 na lina ukubwa kilometa za mraba 5,311. Kati ya vituo hivyo vya tiba kuna vituo vya afya vitatu vya Mbika, Ukune na Bulungwa. Kati ya vituo hivyo vituo viwili vya Mbika-Ushetu na Bulungwa vina huduma ya upasuaji, vituo hivi vinahudumia watu wengi sana kwa kuwa watu wa Jimbo la Ushetu wanahudumiwa na Hospitali ya Wilaya ya Kahama ambayo imezidiwa sana kwani inahudumia Halmashauri nyingi ikiwemo Halmashauri za Ushetu, Ulyankulu, Kaliva, Uyui, Bukene, Mbogwe, Msalala na maeneo ya jirani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo niiombe Serikali ifikirie kupandisha Kituo cha Afya cha Mbika-Ushetu kuwa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ili kusaidia mzigo mkubwa unaobebwa na Hospitali ya Wilaya ya Kahama. Hivyo kuanzishwa au kupandishwa hadhi kituo cha afya kutasaidia mambo mengi ikiwa ni pamoja na kupunguza vifo kutokana na wananchi kusafiri umbali mrefu kwenda Hospitali ya Wilaya kwa kata za Ushetu, Uyogo, Nyamilagano, Ulowa, Ubagwe pamoja na wananchi wa majimbo ya Kaliua, Ulyankulu, Uyui ambao hutibiwa Kahama Mjini kupitia maeneo ya Ushetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii itaondoa dhana kwa wananchi kuona kwamba wametengwa. Vilevile itaboresha huduma za afya Jimboni Ushetu pamoja na kupunguza mrundikano katika Hospitali ya Wilaya ya Kahama na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali itusaidie kupata ambulance ili kuokoa maisha ya wananchi wa Jimbo la Ushetu. Sisi kama Jimbo au Halmashauri tunajitahidi kujenga ili kupata zahanati nyingi katika harakati za kutekeleza sera ya kuwa na zahanati kila kijiji. Kwa sasa tunayo majengo 48 yanayoendelea kujengwa kwa nguvu za wananchi na Halmashauri yao. Majengo hayo ni zahanati 44 na nyumba za watumishi nne. Tunaomba tusaidiwe gari ya kubeba wagonjwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu gari ya chanjo, Halmashauri ya Ushetu haina gari ya chanjo, tunaiomba Serikali itusaidie gari ya chanjo katika Halmashauri ya Ushetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mko hoja.