Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Munde Abdallah Tambwe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. MUNDE A. TAMBWE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa fursa hii na mimi niweze kuchangia hotuba ya Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa ninaipongeza hotuba nzuri ya Waziri Mkuu, lakini nimpongeze Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nimpongeze Waziri Mkuu na nipongeze Baraza zima la Mawaziri kwa kazi nzuri wanayoifanya, kazi yao inatutia moyo sana na inafanya sisi kama wana CCM tutembee kifua mbele. Tunawapongeza sana, tunaomba muendelee kufanya kazi kwa juhudi kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze moja kwa moja kuchangia kuhusu mambo ya Tabora. Naomba nianze na suala zima la tumbaku, maana tumbaku ndiyo Tabora, bila tumbaku Tabora haipo.
Mheshimiwa Naibu Spika, zao hili la tumbaku limekuwa ni zao linalochangia kodi kubwa, pato kubwa la Taifa, lakini wakulima wa tumbaku wanatozwa tozo 19 za tumbaku, hili suala linadhoofisha sana wakulima wa tumbaku. Mkulima wa tumbaku ukimkuta leo hana maendeleo yoyote, tozo ni nyingi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaiomba Serikali yangu, ninamuomba Waziri Mkuu na Serikali ya Awamu ya Tano, kaka yangu Mheshimiwa Mwigulu mziangalie hizi tozo, muweke mkakati maalum wa kupambana na hizi tozo kuzipunguza ili wakulima wa tumbaku waweze kufaidika na kilimo wanacholima, najua Serikali ya Awamu ya Tano ni Serikali ya kusaidia wanyonge. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Tabora tunalima tumbaku kwa asilimia 60 lakini huwezi kuamini hatuna kiwanda cha ku-process tumbaku, hatuna kiwanda cha kutengeneza sigara, inaumiza sana nasema kwa uchungu mkubwa, juzi amekuja mwekezaji wa kujenga kiwanda cha sigara, kiwanda hicho kimewekwa Morogoro, Morogoro hawalimi tumbaku, ajira zetu watapata watu wa Morogoro kule sisi tunaumia, miti inakwisha, watu wetu wanakonda na moto wa tumbaku, hatuna faida yoyote na hiyo tumbaku. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaiomba Serikali ya Awamu ya Tano iliangalie hili suala kwa makini sana, ninamuomba Waziri Mwijage ninamuamini, ana uwezo mkubwa wa kufanya kazi. Tumehangaika naye kutafuta mwekezaji wa tumbaku mara nyingi, lakini Mheshimiwa Waziri Mwijage nikuombe sana hata kama tumekosa kiwanda cha sigara atusaidie tupate hata kiwanda cha ku-process tumbaku hali ya Tabora kwa kweli siyo nzuri, hatuna kiwanda chochote, ajira ni shida. Ninaiomba sana Serikali ya Awamu ya Tano itusaidie, ituonee huruma, tumbaku yote inapatikana Tabora. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumbaku imeliingizia Taifa dola milioni 3 lakini pia inachagia pato la Taifa asilimia 27 ya GDP ya Taifa. Kwa hiyo, tunaomba sana mtuangalie watu wa Tabora.
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie kuhusu suala la hospitali, Tabora Manispaa hatuna hospitali ya Wilaya, tumeliweka hili suala kwenye bajeti toka 2012, tumepata shilingi 150,000,000 tumeanza, lakini tunaiomba Serikali kupitia kwa Waziri Mkuu iangalie jinsi ya kutuwekea hospitali ya Wilaya, pale ni Makao Makuu ya Mkoa population ni kubwa sana, mtu akiumwa malaria moja anaenda hospitali ya Mkoa, msongamano unakuwa mkubwa, matokeo yake tunawalaumu madaktari kila siku lakini kwa kweli msongamano ni mkubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Uyui ambayo iko Tabora Manispaa haina hospitali ya Wilaya, ninaiomba Tabora Manispaa na Uyui tupate pesa za kuweka hospitali za Wilaya ili kupunguza population kubwa ya wagonjwa kwenye hospitali ya Mkoa wa Tabora. Leo siongelei Madaktari Bingwa, Mheshimiwa Ummy aliwahi kuniahidi hapa kwamba analishughulikia suala la Madaktari Bingwa na ninamwamini sana Mheshimiwa Ummy, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, kwa kazi anazozifanya ninaamini atatuletea Madaktari Bingwa ndani ya Mkoa wa Tabora. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee kuhusu kupata Mkoa mpya wa Tabora. Katika Mikoa mikongwe ya nchi hii, Mikoa ya kwanza toka tunapata uhuru ni Mkoa wa Tabora. Kwa kweli Mkoa ule umepanuka jiografia yake ni kubwa, Mheshimiwa Waziri Mkuu amefanya kazi Tabora, anaijua kabisa jiografia ya Mkoa wa Tabora, tunaomba atusaidie kuugawa huu Mkoa, RCC imeshakaa zaidi ya mara tatu, mara nne tukitoa mapendekezo ya kuugawa Mkoa wa Tabora, tunaomba atusaidie sana, tupate Mkoa wa Tabora na Mkoa mpya wa Nzega. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Tabora Manispaa lina population kubwa sana, lina Kata zaidi ya 30 watu ni wengi sana, leo ukiangalia watu wa Jimbo la Pangani ni kama watu 45,000 tu, lakini angalia watu wa Jimbo la Tabora Manisipaa, tuko kwenye 300,000 na kidogo uwajibikaji unakuwa mgumu, kuwafikia wananchi inakuwa kazi sana. Ninamwomba Waziri Simbachawene ni lini sasa atagawa hii Wilaya ya Tabora Manispaa na kuwa Majimbo mawili. Tunamwomba sana atusaidie hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia Wilaya ya Uyui tuliomba Halmashauri ya Wilaya ya Mji Mdogo muda mrefu, tunaiomba Serikali ikija ku-wind up ije na majibu kwa ajili ya Halmashauri ya Wilaya ya Uyui. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu milioni 50 ya kila Kijiji na kila Mtaa. Kwanza nianze kwa kukipogenza Chama changu cha Mapinduzi, viongozi wangu wa Chama cha Mapinduzi kwa kuweka kwenye Ilani yao ya Chama cha Mapinduzi, kwamba kila Mtaa watu wapate milioni 50 na Kijiji ili kusaidia watu wanyonge, watu wa chini, vijana na sisi kina mama. Niwapongeza sana Chama cha Mapinduzi na niseme hiki ni kitu kikubwa sana walichofanya it is not a joke. Kwa hiyo, mimi nawambie tu wale wanaosubiri kukitoa hiki chama madarakini watasubili sana!
MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Watasubiri sana hiki chama kutoka madarakani siyo rahisi, jambo hili ni kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nitoe pongezi zangu za dhati kwa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli. Sikudhani kabisa kwamba bajeti hii ya mara ya kwanza Rais Magufuli na Serikali yake watakuja na mpango wa hizi milioni 50, nilijua wana mambo mengi, wana elimu bure, wana elimu bure kwa vyuo, mimi ninaiita elimu bure kwa vyuo kwa sababu revolving ya vyuo vikuu hatuanza kuiona, pesa zinazoenda kukopesha watoto wetu wa vyuo mimi niseme ni bure tu, Serikali ya Chama cha Mapinduzi inafanya hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Rais na Waziri Mkuu kwa kuanzisha bajeti yao ya kwanza tu kuweka hizi milioni 50. Mimi nilikuwa nadhania kwamba shilingi milioni 50 labda zitakuja 2018, niliwahi kwenda Tabora kwenye kikao cha akina mama wakaniuliza, nikasema jamani tumeingia juzi tu madarakani hebu tumpe Rais na Waziri Mkuu nafasi ya kufanya kazi. Mimi nilidhani labda itakuwa bajeti ya 2017 au 2018 lakini kwa mshangao mkubwa wameleta bajeti hii 2016 big up sana Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nazidi kuipongeza Serikali yangu.
MHE. MUNDE A. TAMBWE: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali hii imekuwa ikituahidi toka 2011 kutuletea maji ya Ziwa Victoria na leo hii nimesoma kwenye randama kuna maji ya Ziwa Victoria yanaonekana lakini sijaona pesa za maji ya Ziwa Victoria. Ninaiomba sana Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi, ikija hapa Wizara ya Maji ituambie imetutengea shilingi ngapi kwa ajili ya Ziwa Victoria na mkandarasi anaanza lini kazi ili tuweze kumjua ni mkandarasi yupi na yupi, tunaiomba sana Serikali ya Chama cha Mapinduzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naendelea kuipongeza Serikali hii, imeleta nidhani kubwa kwenye ofisi za Serikali, imeinua ari ya Watanzania na ari ya wafanyakazi. Leo hii mtu akienda Polisi anahudumiwa, mtu akienda ofisi ya Serikali anahudumiwa, mtu akienda hospitali anahudumiwa, yote hii ni juhudi ya Serikali ya Chama cha Mapinduzi. Mheshimiwa Waziri Mkuu na Mawaziri wako endeleeni kufanya kazi, tuko nyuma yenu tunawapongeza, tunawaunga mkono na tunawasaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi vyama vya siasa haviwezi kutumbuliwa majipu! Naomba niulize kwa sababu kuna vyama hapa ni SACCOS, kuna vyama ni NGO’s kuna vyama vinapata hati chafu. Hivi vyama mwanachama wa chama hicho akiuliza anaitwa msaliti, anafukuzwa. Lakini nimeona Chama cha Mapinduzi kwenye Ilani yake kimeweka milioni 50 kila Mtaa, lakini kuna watu wanaruzuku za Wabunge wao hawajawahi kuweka kwenye Ilani yao hata madawati kumi kila Wilaya. Leo hii wanakuja hapa wanalaumu na kusema kwamba, Serikali ya Chama cha Mapinduzi haifai. Serikali ya Chama cha Mapinduzi inafaa na inawaona wananchi wake.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa!
MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika….
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Munde kuna Taarifa....
MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba unitunzie dakika zangu siwezi kuipokea hiyo taarifa kwa sababu haina msingi wowote. Serikali hii ni ya Chama cha Mapinduzi na Chama cha Mapinduzi ndiyo kimeweka kwenye Ilani yake mambo yote haya yanayoendelea kufanyika, wao kwenye Ilani yao na wao wanapata pesa za walipa kodi za ruzuku wameweka nini kwa ajili ya wananchi wa Watanzania? (Makofi/Vigelegele)
Mheshimiwa Naibu Spika, wao katika pesa za ruzuku ambazo ni za walipa kodi wamefanyia nini wananchi wa Tanzania, hawajawahi hata kujenga choo cha shule kwa ajili ya hela ya ruzuku ya walipa kodi. Pesa hizo wanageuza ni NGOs zao ni SACCOS zao kwa manufaa yao wao binafsi na familia zao, tunataka sasa Serikali ya Chama cha Mapinduzi, sisi ndiyo Wabunge tunatunga sheria, tutunge sheria Waziri Mkuu akatumbue majipu kwenye vyama vya siasa, hivi Vyama siyo kwa ajili ya NGOs. Ahsante sana, nashukuru.