Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

Hon. Esther Nicholus Matiko

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia kwenye Wizara hii muhimu kwa maslahi ya Watanzania na uchumi wa nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuanza kwa kusikitika juu ya kipaumbele kidogo kinachopewa kwa Wizara hii muhimu sana. Mfano bajeti ya Wizara hii imetekelezwa kama asilimia 25.8 tu kwa bajeti za maendeleo kwenye Sekta ya Afya. Pia kwenye Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ni asilimia 5.65 tu ya bajeti ya maendeleo. Hii ni aibu sana kwa kweli kwa nchi. Hivi kwa mwendo huu tutafika kweli?

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti ya maendeleo ni shilingi bilioni 5.8 tu, lakini Serikali inashindwa kutimiza hili. Kwa mwendo huu tutafikia Abuja Declaration ya kutenga angalau asilimia 15 ya bajeti kuu? Imekuwa ni kinyume kabisa! Kwanza katika kutenga; pili, katika kutekeleza hata kile kidogo kilichotengwa. Tanzania ya Viwanda itafikia wapi kama hatuwekezi kwenye afya ambapo tutakuwa tumewekeza kwenye rasilimali watu (Human Capital Investment) na tukifanya hivi tutakuwa na skilled labour?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili litawezekana tu kwa kuwekeza kwenye lishe (nutrition). Nchi yetu kwa sasa ina tatizo kubwa la malnutrition, stunting, wasting, hivi vinapelekea udumavu wa mwili (physical development) na udumavu wa akili (cognitive development). Tukiwa na Taifa la wadumavu daima hatutaweza kufika popote kama Taifa la Tanzania ya viwanda. Ni ndoto!

Mheshimiwa Mwenyekiti, dunia nzima kwa sasa wameamua kuwekeza kwenye lishe ili kuweza kuzalisha rasilimali watu na kukuza uchumi. Tukiwekeza kwenye lishe, tutapunguza vifo vya mama na mtoto, maana mtoto mwenye malnutrition huweza kupata maambukizi ya magonjwa kama vile pneumonia, kuhara, Malaria, utapiamlo na hata kupelekea kifo na ukiangalia idadi ya vifo vya watoto chini ya miaka mitano, bado ni tatizo sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo ni jukumu letu sisi kuwekeza kwenye lishe kwa kufanya yafuatayo:-

(1) Kuhakikisha tuna Maafisa wa Lishe kuanzia ngazi ya Kijiji, Mtaa, Kata na Wilaya ili waweze kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi. Maana zaidi ya asilimia 75 ya Watanzania, cha kushangaza, mikoa yenye idadi kubwa ya watu wenye udumavu ni ile inayolima mazao mbalimbali ila hawana elimu ya lishe bora kwa afya bora;

(2) Kuhakikisha tunakuwa na vipeperushi vinavyotoa elimu juu ya umuhimu wa lishe na ni nini lishe bora ili wananchi wa vijijini na kaya maskini wajue ni jinsi gani wanapata mlo kamili wenye lishe bora?;

(3) Kuweza kutoa ruzuku kwenye viwanda vinavyozalisha chakula ili waweke virutubishi kwenye packages zao;

(4) Kuwekeza, kutoa Supplement Bills hasa kwa akinamama wajawazito wasiokuwa na uwezo wa kupata hivi vidonge vyenye madini ya chuma na vitamins;

(5) Kuweza kuwa na miundombinu imara ya maji, hospitali, zahanati na vituo vya afya; na

(6) Kuepusha mimba za utotoni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nijikite kwenye utatuzi wa huduma ya afya kwenye Jimbo la Tarime Mjini. Kwanza kabisa kwa mwaka wa fedha 2016/2017, Wizara ilituahidi tutapata vituo vinne vya afya, maana kwa sasa hatuna kituo cha afya hata kimoja. Hivyo naomba sana mtupatie hivi vituo vya afya ili kutatua tatizo la huduma za afya Jimboni kwangu, maana sasa ni tegemeo la Hospitali ya Mji ambayo nayo inahudumia Wilaya nzima na hata Wilaya jirani kama Serengeti na Rorya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili ni kuhusu mzigo mkubwa wa Hospitali ya Mji wa Tarime ambayo bado inasomeka kama Hospitali ya Wilaya, lakini basket fund na OC zinakuja kwa kuzingatia idadi ya watu na Mji wa Tarime na siyo Wilaya nzima. Hii inapelekea upungufu wa Watumishi, mfano hili la vyeti feki limeondoka na Madaktari wawili, hivyo tumebaki hoi na inaweza kupelekea vifo vingi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru tumepata Madaktari watatu; wale wa Kenya lakini tumeondokewa na wawili, hivyo tatizo la uhaba lipo pale pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri hatua za haraka zichukuliwe ili tupate hao Madaktari, Manesi na Wahudumu wengine wa Afya. Pili, Hospitali yetu itambulike kwa idadi ya watu wa Wilaya ya Tarime na siyo Mji wa Tarime ili kuwe na uhalisia wa huduma ya afya inayotolewa, maana kule Halmashauri ya Wilaya haina Hospitali. Tunaomba sana.