Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

Hon. Richard Phillip Mbogo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nsimbo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kwa kuongeza bajeti tangu iingie madarakani na Mawaziri kufanya kazi kwa bidii na umakini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Chuo cha Maendeleo ya Wananchi, Msanginya kikiwa chini ya Wizara ya Afya kiliingia mkataba na Mkandarasi wa Ujenzi na Ukarabati wa Majengo ya Chuo hicho, lakini mpaka sasa ujenzi umesimama na Mkandarasi hajalipwa kwa kazi za awali. Pia miundombinu mingi bado ni chakavu sana. Hivyo Serikali inaombwa kuangalia na kutatua kero hizo kwa kuongeza bajeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatoa wito kwa Serikali kulipa deni hili na kazi ikamilike ili huduma ziboreshwe na vijana wapate elimu bora na kuwasaidia katika maisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huduma za Bima ya Afya kwa hospitali binafsi nyingi hazijaingia mkataba, hivyo kutowapa fursa wanachama wa NHIF kufaidika na huduma hiyo. Hivyo basi, Serikali itoe mwongozo kwa hospitali zote binafsi kupokea Bima za NHIF. Vilevile namna ya kuhudumia wateja wa NHIF iwe bora zaidi kwa kuwa wateja wa NHIF hupewa Wauguzi wachache na kuathiri muda wa kupata huduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bila kuathiri mila, desturi na imani zetu, Serikali haina budi sasa kuleta Sheria ya Ndoa ya 1971 iboreshwe ili kurekebisha umri wa mtoto kuolewa na kuoa iwe miaka 18. Kwa kuwa miaka ya sasa, elimu kwa watoto angalau idadi kubwa wanafika kidato cha nne, kwa nini tuondoe haki ya watoto kupata elimu ya sekondari ukizingatia kuwa sekondari takriban kila kata zipo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano, nchi haina dini, hivyo imani za watu wachache zisizuiwe haki za watoto kupata elimu na kuondokana na mimba zenye kuhatarisha maisha yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Rufaa katika nchi zipo kikanda ili kusaidia mikoa yote, lakini Kanda ya Magharibi hatujaona katika hotuba ya bajeti. Hivyo, tunashauri Mkoa wa Katavi uwe na Hospitali ya Rufaa kwa Kanda ya Magharibi kukidhi Mikoa ya Katavi, Kigoma, Tabora na Rukwa pia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua Wizara ya Afya haiwajibiki moja kwa moja, lakini kwa kupitia wafadhili mbalimbali na kutimiza sera mbalimbali hususan kupunguza vifo vya mama na mtoto, Halmashauri ya Nsimbo bado tunahitaji gari la wagonjwa kutokana na moja lililopo kuwa halikidhi mahitaji, sababu ya eneo lilivyo la Jimbo la Nsimbo na pia miundombinu mibovu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Taasisi ya Saratani ya Ocean road inahitaji kutanua huduma zake kwenye Hospitali za Rufaa kila kanda na kuwa na watumishi wanaowajibika moja kwa moja ili kusogeza huduma karibu kwa wananchi kwa kuwa ugonjwa wa Saratani umekuwa tatizo kubwa hasa kwa akina mama (cancer ya uzazi).

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtaji wa Benki ya Wanawake bado kuongezwa kwa kiasi cha kukidhi haja za wanawake, nchi nzima, hivyo tunashauri Serikali iongeze mtaji kama tulivyotoa tangu mwaka jana bajeti ya 2016/2017. Vile vile Halmashauri nyingi hazijatumia fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake, hivyo basi Wizara itoe taarifa kwa Wakurugenzi ili fedha zitoke na wanawake watumie fursa ya kujikwamua kiuchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu na huduma za lishe ni muhimu sana ili kuondoa udumavu kwa watoto. Hivyo Wizara isimamie Halmashauri zote kuhakikisha zinatoa elimu na kusimamia lishe kwa watoto kwa kuhakikisha wazazi wanachangia gharama za lishe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri alitoa taarifa nyakati tofauti kuwa mikoa tisa itapata Madaktari bingwa na Mkoa wa Katavi ukiwemo. Sasa zoezi hili limefikia wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.