Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MH. ZAYNABU M. VULU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehma aliyenijalia kusimama hapa na nichukue pia nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba yake nzuri aliyoitoa kwetu, pia wala sitaki kusema neno baya kwa upande wa pili niwapongeze kwa sababu wametupa nafasi na sisi tuweze kuongea, wananchi wajue Serikali yao chini ya Chama cha Mapinduzi imefanya nini na itaendelea kufanya nini. Niseme kwa niaba yenu, niwaambie wale ahsanteni sana, acheni tujimwage kwa raha zetu ndani ya Ukumbi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kuzungumzia suala la afya. Mheshimiwa Waziri Mkuu kwenye hotuba yake ameligusia vizuri sana suala la afya, ukiangalia bila afya bora hakuna ambaye anaweza akafanya kitu chochote, hata humu ndani kama afya zetu zisingekuwa bora tusingeweza kuja humu ndani, hivyo ninampongeza sana kwa kuliona hilo na kwa kulizungumzia lakini naiomba Serikali tusaidiane, tumeambiwa tuhamasishe suala la mfuko wa afya CHF wananchi wamepokea wito kwa nguvu zao zote, tatizo linakuja kwenye utoaji wa dawa. Wanafika kwenye dirisha hawapati dawa, sasa ni wakati muafaka, MSD (Medical Store Department) iwezeshwe vya kutosha, nimpongeze Waziri wa Afya na Naibu wake, kwa kazi nzuri wanayoifanya lakini MSD isimamie suala la upelekaji dawa ili watu wapate dawa afya zao ziweze kuimarika na waweze kufanya kazi vizuri. Mtu hawezi kwenda shambani kama afya yake siyo nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la kilimo. Kilimo ndiyo uti wa mgongo. Bila pembejeo, bila mbegu nzuri hakuna kilimo kitakachoweza kuwa kizuri. Ufunguaji wa milango ya biashara, ukimwezesha Mkulima kuna uhakika wa kutosha, akipata pembejeo, akipata mbegu bora, atalima yeye na atalima kwa ajili ya kuuza nje hata ndani ya nchi, hilo naomba tuliangalie na tulipe kipaumbele chake.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi natoka Mkoa wa Pwani. Mkoa wa Pwani tuna mabonde na mito mingi sana, tuna Mto Ruaha, tuna Mto Wami, tuna Mto Rufiji, tuna Mto Ruvu, tuna mambonde mengi sana, tunaomba kilimo cha umwagiliaji kiwekewe mkazo katika mabonde hayo ili wananchi waweze kunufaika.
Mheshimiwa Naibu Spika, vijana wakiwezeshwa, wakipewa teknolojia ya umwagiliaji hatutaweza kuwaona tena wanakwenda kucheza pool, tuwawezeshe vijana walime zao ambalo ni jepesi kulima kwenye mabonde, zao la mpunga, zao la nyanya, zao la vitunguu, zao la bamia, mbogamboga hata mahindi.
Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo, naiomba Serikali iweke utaratibu mzuri katika kilimo, pia kutumia maji katika mito yetu na kuweza kufanya zoezi la umwagiliaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, maji ya mito niliyoitaja mitatu, naiomba Serikali ifikie wakati sasa ule mradi wa Kisemvule uanze kazi mara moja. Mradi ule uko Wilaya ya Mkuranga lakini utakapowezeshwa utawanufaisha hata watu wa Dar es Salaam kama mradi wenyewe unavyosema. Lakini mpaka sasa hivi katika maeneo ya Wilaya ya Kisarawe, Wilaya ya Mkuranga, hata Wilaya ya Kibaha Vijijini na Mjini bado tuna matatizo ya maji, naomba sana Serikali ione umuhimu wa kuwezesha upatinaji wa maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiacha mradi huo wa Kisemvule tuone Serikali imechukua hatua zipi sasa za kuweza kuuwezesha mto Rufiji ufike kwenye maeneo jirani, ufike kwenye Wilaya Mkuranga, ufike Wilaya ya Kisarawe hata Dar es Salaam, maji ya Rufiji yanaweza yakasaidia badala ya kuyaacha maji yale yanakwenda yanaingia baharini hatuoni faida kwa watu wengine. Naiomba Serikali iangalie uwezekano wa kutusaidia katika upatikanaji wa maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue nafasi hii nimpongee Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kauli mbiu yake aliyoitoa ya kwamba Tanzania sasa iwe nchi ya uchumi na viwanda. Kweli huu ndiyo wakati muafaka umefika, Serikali ina wajibu wa kufanya hilo na sisi tunaunga mkono. Kwa kuanzia katika Mkoa wetu wa Pwani pamoja na maeneo mengine viwanda vipo lakini Wilaya ya Mkuranga tayari inaongoza kwa kuwa na viwanda vingi, ninaiomba Serikali iangalie umuhimu wa kuwasaidia Watanzania kwanza, tuweke mikataba ambayo itakuwa endelevu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali iwaangalie Watanzania wenye elimu ya kutosha, waweze kupata nafasi kusimamia shughuli za viwanda isiwe vijana wa ajira ndogo ndogo ndiyo waajiriwe katika viwanda vile. Kweli tunasema viwanda ni mkombozi, nimuombe kaka yangu na ndugu Mheshimiwa Mwijage ahakikishe kwamba wale Wawekezaji nazungumzia kwa upande wa Mkuranga sasa hivi ambapo ndiyo tunapokea malalamiko, wanalipwa shilingi 5000 kwa siku, anaingia saa mbili asubuhi, anatoka saa 2 usiku, shilingi 5,000 ukipiga hesabu elfu tano kwa mwezi ni shilingi 150,000, hapa tumemsaidia au tunatumia nguvu zake tu kuwasaidia wale wenye viwanda?
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaiomba sana Serikali iangalie hasa Wizara husika ya ajira ipite kwenye viwanda, ikibidi hata tufuatane naye Waziri husika akaangalie ili aweze kuona hata usalama wa wale wafanyakazi, tunachohitaji viwanda kwa ajili ya ajira, lakini pia vitakavyozalishwa vije kwa Watanzania waweze kununua na pato la nchi liongezeke, lakini tuangalie na maslahi ya Watanzania watakaouwa wameajiriwa pale.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la mikopo. Suala la mikopo kwa wakulima limeoneka vizuri, lakini naomba kujua je, wavuvi wao wamefikiriwaje? Watajiendelezaje katika uvuvi mdogo mdogo? Tunao wavuvi wa baharini, tuna wavuvi wa kwenye maziwa, pia kuna wavuvi wengine wapo kwenye mito yetu ambayo inatuzunguka katika nchi yetu ya Tanzania.
Ninaiomba Serikali iangalie uwezekano wa kuwawezesha wavuvi na kuangalia zile sheria, sheria zinamlindaje mvuvi mdogomdogo pamoja na hata yule mvuvi mkubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kwa kuipongeza Serikali yangu ya Awamu ya Tano kwa kuleta mkopo kuwawezesha wananchi milioni 50 kila kijiji, milioni 50 kila mtaa, ni wazo jema, tulipangie utaratibu mzuri, tuwawezeshe wanawake, tuwawezeshe vijana wetu bila kuwasahau wananume, wako ambao na wao wanahitaji kusaidiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo naomba nichukue nafsi hii kusema kwamba naunga mkono hoja ya Waziri Mkuu na tuko tayari Watanzania kufanya kazi kwa kuijenga nchi yetu na kukijenga Chama chetu ahsante sana.(