Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

Hon. Mary Pius Chatanda

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Korogwe Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza kazi nzuri inayofanywa na Waziri, Naibu Waziri na Watendaji wote wa Wizara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii ya Afya ndiyo Wizara Mama kwa maisha ya Watanzania. Hivyo, ipo haja bajeti inayotengwa kutolewa yote ili kuiwezesha na kuipa wepesi Wizara hii kutekeleza majukumu yake. Bila afya nzuri hakuna viwanda wala shughuli zingine zinazoweza kuinua uchumi wa nchi yetu. Hivyo basi, nashauri bajeti inayotengwa itolewe yote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Mji wa Korogwe haina hospitali. Asilimia 60 ya wananchi wanapata matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Korogwe Vijijini lakini jitihada za makusudi zinafanyika kujenga kituo cha afya chenye majengo ya ghorofa matatu. Nimshukuru kwa ziara aliyoifanya Korogwe, alishiriki shughuli za maendeleo (Msalagambo) na kuahidi kuchangia shilingi milioni 300 katika ujenzi unaoendelea. Aidha, nimshukuru ametuahidi kutupatia ambulance. Mwenyezi Mungu ampe wepesi kukamilisha ahadi ambazo wananchi wa Korogwe wamejenga matumaini makubwa kwake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jengo la Chuo cha Wauguzi Magunga lililopo Korogwe Mjini la ghorofa ambalo lilianza 2010 kwa ajili ya madarasa na Ofisi za utawala limetelekezwa kwa kutotengewa fedha kwa ajili ya ukamilishaji. Mwaka wa fedha 2016/2017 lilitengewa shilingi milioni 400 lakini hazikupelekwa hadi sasa. Niiombe Serikali kulitengea fedha jengo hili kwani linachakaa na litasababisha hasara kwa Serikali kutenga fedha zingine kwa ajili ya ukarabati, huko kutakuwa ni kufuja fedha za wananchi walipa kodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, naomba Serikali iangalie upya kutenga bajeti ya kutosha kwa ajili ya kuwanusuru akinamama wajawazito. Kutofanya hivyo kutaendelea kusababisha vifo vya wanawake hawa na kupunguza nguvu kazi ya Taifa ambayo kwa namna moja au nyingine wanawake ndiyo watenda kazi wazuri katika Taifa hili.