Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

Hon. Cosato David Chumi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafinga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi na laiti ningejua Mheshimiwa Mapunda angekuwa na maneno mazito hivi, ningeridhia kumpa muda wangu, lakini kwa sababu ameshamaliza ngoja niendelee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, napenda kuunga mkono hoja na kwa sababu muda unaweza ukaniwia mchache, nina mambo machache ya kuzungumza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kuzungumza kuhusu mchezo wa mpira ambao ndiyo unapendwa kuliko mchezo wowote. Katika kuzungumzia suala la mchezo wa mpira, napenda kuzungumzia umuhimu wa timu yetu ya Taifa kujiweka katika mazingira ambayo inaweza ikawa inapata nafasi za kushiriki katika mashindano ya Kombe la Dunia na mashindano ya AFCON.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa nina takwimu, katika takwimu za viwango vya FIFA mpaka mwezi Machi sisi Tanzania tulikuwa wa 157 wakati Afghanistan walikuwa wa 156, unaweza kupata picha ina maana hata Afghanistan wametuzidi sisi. Kwa nini inatokea hivi? Viwango vya FIFA vinapangwa kulingana na idadi ya mechi unazocheza zilizopo kwenye kalenda ya FIFA.



Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo letu sisi, wasimamizi wa mpira ambao ni TFF hawalizingatii hilo na matokeo yake tunacheza mechi chache sana kufuatana na kalenda ya FIFA kitu ambacho kingeweza kutupa sisi points za kupanda kwenye viwango vya FIFA. Sasa unapokuwa chini ya viwango vya FIFA maana yake ni nini? Hata unapopangiwa kwenye mashindano ya ku-qualify kwenda AFCON au kwenda World Cup unajikuta kwamba uko kwenye pot four, maana yake ni kwamba pot one wanaingia wale ambao ni vigogo kadhalika pot two na pot three. Sasa kila mara utakuta wewe unapangiwa na timu ambazo ni vigogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye mashindano ya ku- qualify kwenda Kombe la Dunia, sisi mechi ya kwanza tulipangiwa na Malawi tukashinda, lakini mechi ya pili tukajikuta tunaangukia kwa Algeria. Kilichotupata wote mnajua, goli saba kwa mbili. Kwa sababu gani? Kwa sababu sisi hatushiriki ipasavyo mechi za Kimataifa kulingana na kalenda ya FIFA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatoa mfano, katika mwaka 2016 Tanzania imeshiriki mechi tatu tu ambazo ziko kwenye kalenda ya FIFA ukilinganisha na wenzetu, kwa mfano Rwanda wamecheza mechi 11, Uganda mechi 13, Kenya mechi 10, hata hao Afghanistan wenye matatizo, walicheza mechi sita; sisi tumecheza mechi tatu tu, utawezaje kupanda kwenye viwango vya FIFA?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama vile haitoshi, nimechukua takwimu za miaka mitatu iliyopita na miaka mitatu tuliyomo; katika kipindi cha miaka mitatu kutoka mwaka 2014 mpaka 2016 sisi tumecheza mechi za FIFA 24 tu ukilinganisha na Rwanda mechi 26, Uganda mechi 43, Kenya mechi 27, hata Afghanistan mechi 29. Sasa kuna watu hapa wanamkumbuka Leodgar Tenga, ni kwa sababu ya mambo kama haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha uongozi wa TFF ya sasa hivi tumecheza takribani mechi 24 tu; kwa kipindi kama hicho, wakati wa Tenga tumecheza mechi 47.

Sasa takwimu hizi ndiyo zitakupeleka kwenye viwango bora vya FIFA na ili ujihakikishie kuwa kwenye ushindani unaoweza kukupeleka kushiriki Kombe la Dunia au AFCON, lazima uwe kwenye viwango bora vya FIFA angalau namba moja mpaka 100. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kutoshiriki mechi hizi athari yake ni nini? Athari yake kama nilivyosema, unajikuta unapangiwa na vigogo kama Algeria. Kuonesha kwamba ushiriki wa mechi za FIFA ni muhimu, baada ya kucheza mechi zilizopo kwenye kalenda ya FIFA na Burundi na Botswana, ukienda kwenye takwimu za FIFA World Rankings zilizotoka jana, tarehe 4 Mei, sasa hivi kutoka 157 tumefika 135. Kwa hiyo, kuna umuhimu sana wa TFF kujikita katika kuhakikisha kwamba inahakikisha kuwa Timu ya Taifa inacheza mechi nyingi kulingana na kalenda ya FIFA. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu mmoja tunataniana hapa, tulikuwa tunaangalia kirefu cha TFF - Tanzania Football Federation, lakini inaanza kugeuka sasa inakuwa Tanzania Football Fungiafungia. Maana yake sasa tazama watu wanafungiwa, hata hapa Bungeni mtu akikosea anaitwa anapata haki ya kusikilizwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2016 kutokana na ile waliyosema kupanga matokeo, kuna wachezaji wamefungiwa miaka kumi katika soka. Hata dunia ya akina Messi na akina Ronaldo, huwezi ukacheza maximum of more than ten years. Unapomfungia mtu miaka kumi, si umeua kipaji chake. Maana yake ni nini? Lazima tuwe considerately. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa TFF isijikite tu kwenye mambo haya ya usimamizi wa nidhamu ikajikuta inaacha kusimamia mambo ambayo yangetufanya sisi tupande katika viwango vya FIFA. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba pia nizungumzie soka letu. Nilisema hata mwaka 2016, kwa nini tusi- commercialize mpira wetu? Uingereza timu yao ya Taifa inasuasua, lakini hakuna mahali ambapo kuna biashara kama katika soka ya EPL. Je, Serikali, Mheshimiwa Dkt. Mwakyembe, wewe ni mwanasheria, naamini unaweza ukatusaidia, kwa nini tusi-commercialize mpira wetu na sisi ikawa ni chanzo kikubwa cha kutupa mapato?

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika dunia ya sasa hivi, soka ni uchumi ndugu zangu. Usione watu wanamnunua Ronaldo au Messi kwa mamilioni ya pesa, yanarudi kwa namna nyingi tofauti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaishauri Serikali, hebu tufikirie, kama sisi sasa hivi tuna soko huria, kwa nini pia katika soka tusi-commercialize hii ikawa professional football? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, narudi pia katika vilabu; siwezi kuisema tu TFF peke yake, hata vilabu vyetu vikubwa Simba na Yanga; hivi wewe unajiita Rais wa Klabu, majengo toka walivyojenga akina Marehemu Tabu Mangala, mnashindwa hata kujenga viwanja vya michezo vya mazoezi? Unaenda kila siku kuazima uwanja Boko Veteran! Wewe Rais wa Simba au Rais wa Yanga, unaacha legacy gani katika klabu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nyakati hizi kuna fursa nyingi sana za kuweza kupata wadhamini, watu wa kuwekeza; Azam wamekuja juzi tu tumeona. Sasa lazima tujisifu kwamba ni viongozi wa vilabu ambao kweli tunaacha legacy katika vilabu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Nkamia amesema lazima soka ianzie kwenye timu za vijana, lakini mimi nataka niende mbele zaidi, hata Serikali Mheshimiwa Dkt. Mwakyembe peke yako huwezi, lazima ushirikiane na Wizara ya Elimu, lazima ushirikiane na TAMISEMI na Wizara ya Ardhi kutenga maeneo na kuyapima kwa ajili ya michezo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimesoma Malangali sekondari, ilikuwa ni shule yenye mchepuo wa kilimo. Tulikuwa tuna shule kama Shycom cha mchepuo wa biashara, lazima kama tuko serious tunataka tuvune kutoka michezo tuanzishe shule ambazo zitakuwa na michepuo ya michezo, tutaziwekea miundombinu ya kimichezo, lakini lazima pia ziwe na walimu kutoka Chuo cha Walimu wa Michezo kule Malya, otherwise Mheshimiwa Dkt. Mwakyembe tutakuja tuta- table hapa bajeti tutachangia, tutaondoka 2020 itafika, World Cup tutaishia kuiona kwenye tv, AFCON tutaishia kuiona kwenye tv. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Dkt. Mwakyembe, kama seriously tunataka kuwekeza kwenye michezo, ni lazima tufanye mambo hayo. Kwa sababu gani? In connection na michezo, moja, kwanza unatangaza Taifa. Tumeona Alphonce Simbu amekwenda kule London Marathon. Kitendo cha kuwa mtu wa tano tu, tayari sisi umeshavutia idadi kadhaa ya watalii, umeongeza mapato katika Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunapopiga kelele kuhusu michezo, siyo kwa ajili ya kuburudika, hapana, ni kwa sababu michezo ni chanzo kikubwa sana cha mapato na hivyo itakuwa na mchango mkubwa katika uchumi wa Taifa letu. Marekani leo hii, entertainment and sports industry mchango wake katika Pato la Taifa la uchumi wa Marekani siyo chini ya asilimia saba. Kwa hiyo, hatuzungumzii kuhusu tu kuji-entertain. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, lazima nizungumzie pia wasanii. Juzi hapa kumetokea mvutano kwamba Serikali izuie picha kutoka nje, hapana. Ninachosema Mheshimiwa Dkt. Mwakyembe, filamu zinazotoka nje ikiwa msanii wa ndani lazima alipie COSOTA, lazima alipie BASATA, lazima alipie Bodi ya Filamu kukaguliwa picha zake; ni lazima pia na hizi filamu zinazotoka nje tuweke utaratibu ziweze kulipia mapato katika Taifa hili. Sasa filamu kutoka nje inanunuliwa shilingi 1,000, filamu ya ndani inanunuliwa shilingi 2,500 lakini hii ya nje haijapitia mfumo wowote ambao utahakikisha kwamba inalipia kodi. Kwa hiyo, tunaposema haya tunazungumzia mapato katika Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, nizungumze pia kuhusu wasanii na wenyewe wafanye kazi ambazo zina mvuto, isiwe kama tunavyoona kwenye mitandao ya kijamii, dhihaka imejaa sana. Kwa hiyo, nao wafanye kazi kadri inavyotakiwa. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema pale mwanzo, naunga mkono hoja lakini lazima tuoneshe seriousness kwa vitendo katika suala zima la michezo kwa sababu za kiuchumi na kimapato. Ahsante sana.