Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Maswa Mashariki
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Kwanza kabisa, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya njema. Nianze kwanza na ushauri kabla sijaongea mambo mengine. Ushauri wangu kuhusu Mwenge, leo ni mjadala ulikuwa umeendelea kuhusu Mwenge, watu wameongea sana na wanaongea hasa kuhusu gharama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nami naomba niungane na wenzangu kutetea umuhimu wa Mwenge. Tuendelee kukimbiza Mwenge, uendelee kuangaza hadi nje ya mipaka ulete upendo na amani katika nchi yetu. Ushauri wangu ni kwamba, kama tunaona kuna gharama kubwa, tusiwe na haja ya kuukimbiza Mwenge kila siku nchi nzima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuchague siku moja kama ni siku ya Uhuru tarehe 9 mwezi wa 12, tarehe 8 unawashwa katika Mkoa ambao wanaazimisha siku hiyo ya Kitaifa kama ni Mkoa wa Kilimanjaro mfano, unawashwa, tarehe 9 unazimwa na unafanya kazi zile zote ambazo Mwenge unafanya katika Mkoa husika. Mwaka unaofuata tunakwenda kwenye Mkoa mwingine tunafanya vile. Hayo ni mawazo yangu, lakini tunaweza tuka-discuss zaidi katika modarity ya kuukimbiza Mwenge kama tunaona gharama ni kubwa. Huo ni ushauri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili kuhusu TBC. TBC inavyoonekana kwa kweli, imewekwa pembeni. Tuangalie namna ya kuwasaidia TBC. Matangazo ya TBC yanakatika, quality ya picha ni mbovu, wakati mwingine unatazama sauti inakata na wakati mwingine unaona kabisa kwamba hapa kuna upungufu, teknolojia imeshawapita, wako nyuma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri iangaliwe namna ya kuwasaidia hawa kupitia vile wanaita ving’amuzi. Wale wateja wa ving’amuzi waweze kulipa pesa na pesa zile zikilipwa TBC wapewe hela yao moja kwa moja kuliko kuanza kupeleka pesa Hazina, mara process zinafanyika za hapa na pale na matokeo yake wanachelewa kupata pesa. Wanahitaji mitambo mipya, wanahitaji teknolojia mpya. Wako nyuma, hawako kibiashara kabisa! Tunaomba muwaangalie kwa jicho la namna ya pekee ili kusudi muweze kuwasaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine natoa pongezi kwa Serengeti Boys; kazi wanayofanya ni nzuri kabisa, wametuletea heshima katika nchi hii. Tunaomba hiyo timu muilee vizuri, hiyo timu itatufikisha mbali. Nakumbuka kuna timu ya vijana ilienda hadi ikachukua ubingwa wa dunia, lakini baada ya pale kuja kurudi ile timu sijui imepotelea wapi. Tunaomba muiangalie hii Serengeti Boys, itatupeleka mbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumze kwa kina kidogo, naomba ku-declare mimi ni Mwenyekiti wa Chama cha Mpira katika Mkoa wa Simiyu. Kwa hiyo, mimi ni mdau mkubwa wa mpira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme kwamba katika timu ya Taifa ni lazima tuwe na utaratibu wa kutengeneza timu yetu ya Taifa. Watu tunadhani kwamba premier league ndiyo inayotengeneza timu ya Taifa. Hivi vilabu, huwezi kutengeneza timu ya Taifa kutoka kwenye hivi vilabu. Timu ya Taifa ya Mpira wa Miguu inatengenezwa kutokana na Football Academy.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiwa na Football Academy nzuri za kutosha tutakuwa na vijana wengi ambao tutaweza kutengeneza kutengeneza timu ya Taifa. Premier league ni typical commercial league. Hiyo ni commercial football, pale ni biashara, siyo timu ya Taifa. Mshindi wa Premier League anapokwenda kwenye Champions League anakwenda kucheza kibiashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo sisi tunadhani kwamba kutengeneza Timu ya Taifa ni lazima wachezaji watoke kwenye Premier League, ni makosa. Premier League ni biashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, unapotegemea Premier League kutengeneza Timu ya Taifa, utajikuta huyu mwenye timu, kwa mfano Azam tumchukulie, Azam ana uwezo wa kununua wachezaji kutoka nje hata 20; leo bingwa wa Tanzania akipatikana, anapokwenda kwenye Champions League ya Afrika anaenda kukutana na TP Mazembe, ambapo TP Mazembe yeye amenunua wachezaji karibu ya 20 kutoka nje, kwa sababu anafanya biashara. Sisi leo Azam unamzuia kwa mfano asinunue wachezaji zaidi ya watano kutoka nje, hii sheria haina maana yoyote. Hii muiondoe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wachezaji wapatikane first division kushuka chini kutokana na zile Football Academy zetu. Nawapeni mfano, Zambia walipoteza wachezaji walikuwa wanaenda Gabon, walianguka na ndege.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Zambia wamepoteza wachezaji, makocha wakajiunga wakarudi kwenye Football Academy zao wakaangalia wachezaji wakatengeneza timu nyingine mpya ya watoto wadogo, wakaunda Timu ya Taifa ikaenda Gabon na ikacheza ikafika finali ikatolewa na Nigeria. Kila mtu anakumbuka hapa! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda Brazil, kuna wachezaji kama Romario alikataliwa asiingie Timu ya Taifa, kocha akasema tuna mchezaji anaitwa Gaucho kutoka kwenye Football Academy. Alivyoingia Gaucho wakachukua kombe la dunia. Sisi leo tunang’ang’ania wachezaji wa Premier League ndio wacheze Timu ya Taifa. Hatuwezi kufika popote! Undeni Football Academies za kutosha, fufueni vile Vyuo vya Michezo vya kutosha ili kusudi mpate watoto wa kutosha kwenda kucheza Timu ya Taifa. Kwa mtindo huu hatutafika. Kwanza league zenyewe hazina quality, you cannot predict. Ukienda kuangalia mpira, mara refa amekula mlungula, anaamua penati, anaamua kitu cha ajabu ajabu. Leo kuna points zinanyang’anywa mezani, hakuna! Tunafanya nini?
Mheshiiwa Mwenyekiti, nawashukuru TFF, wanafanya kazi nzuri. Hata ukitazama kalenda ya Kimataifa TFF wamefanya kazi nzuri. Ukitizama zile kalenda za michezo ya Kimataifa katika nchi 12 za CECAFA, TFF wamejitahidi badala ya mechi moja wanacheza mechi mbili, hilo nawapa pongezi, lakini waunde miundombinu ya kutafuta wachezaji wa Timu ya Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, twende kwenye Bongo Movies; hii ku-burn sinema za kutoka nje sijui imetoka wapi? Hivi una-burn sinema za kutoka nje mnatuuzia zile sinema zenu za jambazi ameingia na soksi! Eti jambazi ameingia na soksi kuvamia mtu, ulishawahi kuona wapi? Tuleteeni sinema; sisi tunamjua Rambo. Mimi nikiwa mdogo namjua James Bond. Kwenye miziki ya zamani tulikuwa tunamjua Bob Marley. Mbona wenye muziki wamejitahidi!
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilienda Kenya, kwenye club za Kenya unakuta watu wanapiga miziki ya Kenya. Sasa hivi ukienda unakuta wanapiga Bongo Flava, ina maana Bongo Flava wamejitahidi. Nyie Bongo Movie, mna-burn kuingiza sinema kutoka nje. Hii imetoka wapi? Naomba tusitafute kiki kwa shortcut …
MHE. STANSLAUS H. NYONGO: …warudi nyuma, wajitahidi kutengeneza sinema vizuri, wataingia kwenye soko ndani na nje ya nchi. Sasa una-burn ku-import sinema kutoka nje: Je hao wa Kenya, Wanaigeria; sisi tunataka leo tuuze sinema Kenya na Uganda. Sasa tutaziuzaje kule? Tutaziuza iwapo tume-improve quality ya sinema zetu za Bongo. Warudi nyuma wajipange. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la Kiswahili. Ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge, nilikwenda South Africa nikakuta kuna Wakalimani kwenye Mkutano. Mkalimani anaongea ki-Portugal na Kiingereza. Nikauliza, Mkalimani wa Kiswahili yuko wapi, kwa sababu nataka niongee Kiswahili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mnapokwenda kwenye mikutano, mwombe Wakalimani wa Kishwahili kule mnakokwenda. Kwa sababu mkiweka wakalimani wa Kiswahili, mtawapa soko wakalimani na watu watajifunza Kiswahili, wataona kwamba kina soko. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kiswahili ni lugha kubwa, imekuwa ya pili kwa Afrika ikiongozwa na lugha ya Kiarabu. Lugha ya pili ni Kiswahili, ina maana lugha yetu ni kubwa, tusiibeze lugha yetu. Tuitukuze lugha yetu. Naomba tumjali, tumtetee na tumlinde na tumheshimu Mheshimiwa Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere kwa kukitukuza Kiswahili. Turudi tuendelee kuongea Kiswahili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampa hongera Mheshimiwa Magufuli kwa kwenda kuongea Kiswahili nje ya nchi. Ombeni siku zote mnapokwenda kwenye Mikutano mwombe Mkalimani wa Kiswahili. Semeni, hatujui Kiingereza. Tatizo la Sisi Wabongo, tunajifanya tunajua Kiingereza, hatujui. Unafika kule hata ukipewa muda wa kuongea, unaongea point mbili, tatu, baada ya hapo umetoka nje ya line. Tuongee Kiswahili. Tuweke Wakalimani wa Kiswahili, Kiswahili ziwe na soko. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hongera Mheshimiwa Magufuli kwa kwenda kuongea kiswahili nje ya nchi. Siku zote mnapokwenda kwenye mikutano ombeni mkalimani wa kiswahili, semeni hatujui kiingereza. Tatizo la sisi wabongo (watanzania) tunajifanya tunajua kiingereza, hatujui. Unafika kule hata ukipewa muda kuongea unaongea point mbili, tatu baada ya hapo umetoka nje ya line. Tuongee kiswahili, tuweke wakalimani wa kiswahili, ili kiswahili kiwe na soko. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ngoma za kienyeji, tv zetu, hawa TCRA mtu anayeomba leseni ya tv katika vipindi anavyoomba kwamba mimi nitaonyesha vipindi moja, mbili, tatu, kiwepo na kipindi cha ngoma za kienyeji kwenye tv. Iwe ni utaratibu kwa sababu sisi kwa mfano kule Usukumani tuna ngoma nyingi na nadhani hakuna kabila lenye ngoma nyingi kama Wasukuma. Tuna ngoma za gugobogobo, wigashe, bugoyangi na kadhalika kuna ngoma nyingi zionekane, mbona makirikiri tunaiona kutoka Zimbwabwe?