Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CHADEMA
Constituent
Arusha Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. GODBLESS J. LEMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Naif Abazeed alikuwa ni kijana mdogo sana kipindi hicho wa miaka isiyozidi 16 na ndiye alisababisha machafuko yanayoendelea Syria sasa hivi. Pia Mohamed Bouazizi yeye ndiye aliyesababisha machafuko yaliyotokea kule Tunisia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mwanaharakati mmoja alisema maneno haya, naomba niyasome:-
“Kitu kimoja tu cha hakika ni kuwa, damu ikimwagika hasa damu ya kimapinduzi hutoa mvuke utakaonyesha na kutiririsha mafuriko katika mito na vijito vya haki. Kama itanyesha mvua ya radi basi itaambatana na mwanga na cheche zitakazowamulika walaghai, watesaji, wakandamizaji wa haki na watetezi wa haki watapata mwanga katikati ya giza totoro la unyanyasaji.” (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maneno haya ni message ya mwisho ya Ben Saanane ambaye hatujui kama ni marehemu ama ni hai, lakini hata kumjadili humu haturuhusiwi, nje mikutano ya hadhara hatufanyi. Kama kijana wa miaka 16 katika Taifa ambalo halina uhuru wa vyombo vya habari, halina chama cha siasa, aliandika maneno machache tu, “Assad must go, Assad will be next,” leo Syria haina amani. Kama kijana mmoja alijichoma moto Tunisia na Tunisia ikaingia kwenye machafuko, vyama vya siasa ni alternative ya amani, uhuru wa habari ni alternative ya amani siyo kikwazo cha amani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wanapoongea wanatema nyongo. Watu wanapoongea wana-release tension, leo tunapotaka kujadili mambo ya msingi mnatumia nguvu na uwezo mlionao, mtashinda. Kila jambo mnalotaka kulipitisha kwa wingi wenu mtashinda. Kila jambo mnalotaka kulifanya kwa wingi wenu mtatushinda. Kwenye mchango wangu uliopita nilisema Mungu hadhihakiwi, apandacho mtu ndicho avunacho. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nilikuwa magereza, vijana waliokamatwa kwa makosa ya cyber walioko magereza, makosa ambayo ni bailable offence ni wengi. Wanakamatwa kimya kimya wanapelekwa mahakamani, wanasomewa mashtaka bila ndugu zao kuwepo, wanapelekwa magereza. Vijana wamejaa magereza kwa sababu ya ukosoaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nimeona kwenye mitandao na mimi naomba nipaze sauti kabisa kwamba Kinana naye amefichwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naomba nimtetee Kinana kama Waziri Kivuli wa Mambo ya Ndani. Kama ni kweli Kinana amefichwa, kwa mujibu wa mitandao kwa sababu hata Ben Saanane kupotea tuliona kwenye mitandao, tukapuuza. Hii ya Kinana kama ninyi mtapuuza, mimi sitaki kupuuza, ni mpiga kura wangu Arusha, naomba nimtetee.
heshimiwa Mwenyekiti, kuna mtoto mmoja alipewa shilingi 200,000 na baba yake akaambiwa akalipe ada. Alipokuwa njiani akaenda aka-bet mchezo kwa shilingi 30,000. Alipo-bet akapata shilingi 3,000,000. Akamtumia baba yake message akamwambia, baba ile pesa uliyonipa ya ada nimetumia shilingi 30,000 nime-bet. Sasa baba kabla hajajua mtoto alipata faida ya shilingi 3,000,000 akaanza kumtukana mtoto, mjinga wewe, kwa nini umetumia fedha kufanya mambo yako ya kitoto? Mtoto akamwambia, baba hapana, nime-bet shilingi 30,000 nimepata shilingi 3,000,000. Baba akageuka akamwambia si unge-bet yote upate nyingi? (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, iko siku tutawabariki na mtakataa baraka. Yaani iko siku tutawatetea kabisa na mtakataa utetezi wetu kwa sababu kila mara tunapokuja na mambo ya msingi mnafikiri sisi ni maadui zenu. Ninyi sio maadui zetu, ninyi ni marafiki zetu, nyie ndiyo chama tawala. Leo tumeongea habari ya Ben Saanane mkakataa, nikaongea habari ya Katibu Mkuu wenu hata kama ni tetesi mlitakiwa mzichukulie maanani mseme huyu kijana ana roho nzuri, mmekataa, sasa nimeondoka huko. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, uhuru wa habari ni nini? Nimesema kwenye hoja zangu nilizojenga, hatuwezi kuwa na Taifa lenye amani bila kuwa na uhuru wa habari. Mheshimiwa Tundu Lissu amewaambia asubuhi hapa kwamba msifikiri mnatunga sheria ama msifikiri mnatumia wingi wenu kutukomoa sisi, mna watoto na wajukuu wanakua. Mheshimiwa Mkuchika hapa amesema yeye ana umri mkubwa, ni kweli ana umri mkubwa ndiyo maana kuna saa mambo mengine ya msingi yanaweza yakampita, lakini ninachosema ni kwamba Mheshimiwa Mkuchika ana watoto, ana wajukuu nawajua. Tunapopigania uhuru wa habari hatupiganii CHADEMA, tunapopigania uhuru wa habari hatupiganii CCM, tunapigania Taifa bora na Taifa huru. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ndiyo tukasema leo ndani ya Bunge hatusemi na kwenye mitandao hawaongei. Sasa kama kwenye mitandao hawataongea, vyombo vya habari havitasema, huko mitaani mikutano ya hadhara imezuiwa ndiyo maana nikaanza kujenga hoja kwa wale vijana wawili, yule wa Syria na yule wa Tunisia kwamba iko siku watu wataingia barabarani kutafuta uhuru mnaowanyima. Watu hawa hawatakuwa wametumwa na CHADEMA wala hawatakuwa wametumwa na CUF na siku hiyo kila mtu atatafuta nyumba ya kujificha, iko siku. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu unapozuia haki, unapozuia uhuru, unapozuia kweli, unatengeneza balaa katika Taifa hili. Tunalalamika kwa sababu familia zetu zinaishi hapa, tunalalamika kwa sababu sisi tunaishi hapa tumejenga Tanzania, tumeishi Tanzania, tumezaliwa Tanzania, tungekuwa na mpango wa kuondoka tungeenda kulalamikia Marekani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukisema miongozo ni mingi na sijui hata hotuba yangu itakuwaje sasa kama hotuba ya Waziri wa Michezo, Habari na Utamaduni mmeifanya hivi, hotuba ya Waziri wa Mambo ya Ndani na uzoefu wa Lijualikali alivyokuwa Magereza, uzoefu wangu nilipokuwa magereza mtaanza kuizuia kuanzia kwenye salamu. (Makofi)
Waheshimwa Wabunge mko wengi tusaidieni, Mawaziri tusaidieni huku kuna madaktari, kuna maprofesa tusaidieni, taifa hili tukishamalizwa sisi, narudia tena, tukishamalizwa sisi, msumeno utakaofuatwa utakuwa ni kwenu. Ni nini mnachokipigania Waheshimiwa Wabunge mnakipigania mnafanya kila kitu kinakuwa hovyo, ni fedha?
Mheshimiwa Mwenyekiti, utu wa mtu haupimwi kwa ghorofa, utu wa mtu haupimwi kwa cheo, utu wa mtu unapimwa kwa kazi na wajibu ulioufanya katika ulimwengu na wajibu huo ninyi kama Chama Tawala, mnaweza mkaufanya, sisi tutashindwa. Mimi nilikamatwa nje getini hapo, nikapelekwa Kondoa, nikawekwa lockup saa nne usiku mpaka saa nane usiku. Nikapelekwa Arusha nikatengwa chumba changu peke yangu, nikakaa jela nikatoka baada ya miezi minne. Mnaweza mkafanya hivyo leo, mimi mkitaka kuniua mnaniua leo, kesho ni mbali, mkitaka kumuua yeyote hapa mnamuua leo, kesho ni mbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunasema hivi haya mambo mnayotuzuia kuyasema mnafikiri tunayasema kwa sababu tunapenda uanaharakati, mimi na watoto na mtoto wangu wa kwanza ana miaka 11 na wa mwisho ana miaka minne, ningependa kuona watoto wangu, ndoa, harusi na elimu ya watoto wangu kwa macho yangu. Hata hivyo, ikibidi nisione hiyo harusi kwa sababu ya kupigania ninachokipigania watakumbuka kwamba maisha yetu Bungeni hayakupigania property yalipigania haki na msingi wa Taifa hili kazi hii ambayo mmeishinda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimwa Wabunge, Waheshimiwa Mawaziri, hapo alikaa Mzee Sitta leo ni marehemu, kila mtu atapita kwa wakati wake. Ni muhimu mkapita mkaacha faraja nyuma, ni muhimu mkapita mkaacha baraka nyuma, acheni kutumia wingi wenu vibaya.
Mheshimiwa Simbachawene wewe una historia, wewe ulikuwa kondakta, Mungu amekuweka hapo ulipo, tulitarajia tukuone wewe unapigania nchi hii, tulitarajia tukuone wewe unakumbukumbu ya haki na msingi, leo unaishi utafikiria umezaliwa kwenye familia Warren Buffet kila watu wakisimama kuongea ukweli …(Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)