Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

Hon. Richard Phillip Mbogo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nsimbo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata nafasi hii. Kwanza nimshukuru Mungu na pia nimpongeze Waziri kwa uwasilishaji mzuri pamoja na Kamati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kuchangia suala la shule za msingi na sekondari kwa ujumla wake upande wa sanaa, michezo na utamaduni. Sijui kama ni sera imebadilika au ni kipi kilichotokea tofauti na miaka ya nyuma, shule zetu za msingi tulikuwa tunafundishwa michezo, sanaa, utamaduni na muziki. Hii ilikuwa inatujenga mpaka hata leo hii wengine tunaweza kuimba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ilikuwa inasaidia kwa mtu ambaye anaendelea kusoma mpaka chuo kikuu anaenda kusomea muziki na kuna kozi zingine kwa mfano kama physical education, mtu anasomea muziki somo lingine la kufundishia. Kwa hiyo, atatoka ni mwanamuziki lakini pia anakuwa na somo la kufundishia. Msingi unakuwa umejengwa kuanzia shule ya msingi na tuna vyuo vingine ambavyo vilikuwa vinatoa diploma kwa mfano kule Mwanza (Butimba) watu wamesoma sanaa.

Kwa hiyo, tuombe Waziri atakavyokuja ajaribu kutuelekeza kwamba ni jinsi gani ataweza kurudisha kwenye shule zetu za msingi na sekondari jambo hili ambalo lilikuwa linatusaidia katika kukuza hivi vipaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, Wizara hii tunaoanisha na utalii, kwa misingi ipi? Tunavyowakuza watu waka-perfom nje ya nchi, kama walivyokuwa akina Filbert Bayi na wengine, tukiangalia nchi za Kenya, Ethiopia watu ambao wanaweza kufanya hizi mbio za marathon kama akina Haile Gebrselassie wameingia mpaka kwenye matangazo, wanatangaza nchi yao, wameingiza mapato ya ndani katika nchi yao kwa kuleta fedha za kigeni. Sasa na sisi Wizara hii itakuwa ni moja ya Wizara ambazo zitaweza kuukuza utalii katika nchi yetu kwa watu kufanya kazi nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyikiti, kwa upande wa sanaa kwa mfano tulikuwa na Marehemu Kanumba aliweza kufanya collaboration na Wanaigeria, imeenda, sasa hizi tuna mwanamuziki Diamond anafanya collaboration na wanamuziki mbalimbali mpaka Marekani na huko kwingine. Kwa hiyo, Wizara hii inakuza utalii ni muhimu sana kwenye pato letu la nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine dunia sasa hivi imekuwa kwenye kiganja, teknolojia imekua. Ni jinsi gani Wizara inachukua ukuaji wa teknolojia katika kudhibiti mambo mbalimbali pamoja na kuongeza mapato. Kwa mfano, sasa kupitia simu zetu (smart phone), ukiingia youtube utaangalia wimbo umekuwa viewed labda mara milioni 900. Kwa mfano wimbo wa Diamond Mdogo mdogo ukiingia youtube sasa hivi viewers wame-view kwa milioni 900 karibuni na laki tatu. Je, kama Serikali kwa kupitia hii mitandao, tuna njia gani ya kuongeza mapato katika maeneo hayo? Sasa hivi watu wana-create application mbalimbali ambapo unaweza ukaingia uka-download na ukapata miziki mbalimbali, je, Serikali kupitia hizi applications tunaweza kufanyaje ili tuweze kuongeza mapato? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusu ukuzaji wa mapato. Tukiangalia mchanganuo wa makusanyo ya maduhui, Baraza la Michezo la Taifa (BMT) ndio limeingiza shilingi 70,560,000 katika mapato ya kiujumla haya ya shilingi bilioni 36, kwa hiyo ni asilimia ndogo mno. Je, hawa viongozi wa Baraza la Michezo wana mkakati gani kuhakikisha kwamba wanapandisha mapato? Mapato haya ni madogo tatizo ni nini? Tuna poor internal control au vyanzo vingi vya mapato havifuatiliwi? Kwa hiyo, tutaomba Mheshimiwa Waziri wakati anahitimisha angalau awe na majibu ya jinsi gani BMT waweze kukuza mapato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni ukuzaji wa vipaji, hizi academy. Tunamshukuru Mheshimiwa Jakaya Kikwete pale Kidongo Chekundu Dar es Salaam aliweza kuweka ile academy. Je, kwa ujumla wake tukienda kikanda, tuna mkakati gani angalau kikanda tukawa na ukuzaji wa
vipaji ili vijana wetu katika michezo ya aina mbalimbali mfano riadha, tufe, mikuki, netball, basketball yote ili tuweze kwenda kimataifa. Leo hii mimi ukanipeleka nikawe mwanamchezo mzuri wa football siwezi kuwa lakini mtoto mdogo kuanzia miaka mitano diyo wanatakiwa wajifunze. Sasa hivi ukiangalia mtoto wa Ronaldo anacheza mpira mzuri, yuko kwenye shule na ni academy, mzazi wake anamlipia na atakuwa mchezaji mzuri, ataingiza pato lake binafsi na la nchi. Sasa hizi academy kama Wizara kwa kushirikiana na vyama mbalimbali vya michezo mje mtuambie mkakati gani ambao mnaolenga kuweza kukuza michezo nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala la sheria mbalimbali zilizoko katika Wizara. Mara ya mwisho ziliboreshwa lini ili kuendana na uhalisia wa hali halisi ya dunia ilivyo sasa hivi? Kwa hiyo, tutaomba Mheshimiwa Waziri upungufu wowote ulioko kwenye sheria mbalimbali hata hizi za haki miliki ambazo wasanii wengi wanalalamikia zije kwa ajili ya maboresho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sikufuatilia kwa ukaribu, tutaomba kujua ile mikakati ya vazi la Taifa na tamaduni mbalimbali lilifikia wapi? Nakumbuka mwaka jana ilizungumziwa lakini imefikia wapi kwamba hili ndilo vazi la Mtanzania ambaye akivaa hivi unajua ametoka Tanzania. Wenzetu Wahindi ukiona tu lile vazi unajua hili la Kihindi, ukimwona Mnaigeria unajua vazi la Kinaigeria na nchi zingine sasa na sisi Tanzania identity yetu katika utamaduni ni ipi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho lakini siyo dogo, ni jinsi gani tunavyo-link Wizara na Halmashauri zetu za Wilaya, Manispaa na Majiji kupitia Idara za Utamaduni. Nashauri wapewe vifaa angalau pikipiki kwa ajili ya kuzunguka katika maeneo mbalimbali ili wafanye kazi zao kiufanisi. Ukiangalia Maafisa Utamaduni ni moja ya idara ambazo katika Halmashauri hazina vifaa kabisa, Wabunge tukienda tunataka kuendesha ligi inabidi umtafutie usafiri ili ndio akazunguke huko vijijini na vijijini tuna vijana wanamichezo wengi kweli kweli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hukitimisha tu naomba sana michezo upande wa shule za msingi na sekondari tuirudishe ili vijana wetu waweze kukuza vipaji na ni njia ya afya mojawapo, ukiangalia sasa hivi Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu ametoa wito kwa watumishi kufanya mazoezi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, ahsante sana.