Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

Hon. Ali Hassan Omar King

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Jang'ombe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii. Awali nitangulize shukrani zangu kwa Mwenyezi Mungu ambaye ametupa uhai na aliyetufanya tukaja leo hapa katika mazingira ambayo tuko salama.

Mheshimiwa Spika, pili, tutoe pole kwa familia ambazo zimepata msiba kutokana na tukio ambalo limetokea ingawa inajirejea, lakini kipekee nahisi sitaitendea haki nchi yangu bila kutoa pole kwa janga ambalo limetokea.

Mheshimiwa Spika, katika kuchangia suala hili, kwanza nianze na chombo muhimu sana ambacho ni TBC. TBC ukiangalia katika dira yake, kwa mujibu wa kitabu ambacho kimetolewa na Mheshimiwa Waziri hapa, ni kwamba kuwa na Taifa linalohabarishwa vizuri na katika dhima wakaandika kwamba upatikanaji stahiki wa habari; halafu tukija katika slogan yao wanasema, “Ukweli na Uhakika.”

Mheshimiwa Spika, sasa kutokana na dhima hii na dira ambayo imeelezwa ya TBC, moja kwa moja ni kwamba TBC inataka kutuhabarisha Watanzania habari za ukweli na uhakika na ndivyo walivyoji-position. Hapo hapo, habari hizo za ukweli na uhakika bila ya kuwa na miundombinu mizuri, bila hawa TBC kuwezeshwa hatutaweza kupata habari za ukweli na uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tukisema habari za ukweli na uhakika, wakati mwingine inawezekana kikatangulia chombo kikatoa habari ambazo siyo za ukweli na siyo za uhakika. Sasa TBC baadaye ndiyo ije ikanushe. Sasa inaweza ikachelewa kutoa habari kutokana na miundombinu ambayo wanayo au mazingira ya kazi ambayo yapo. Sasa ili tuihabarishe vyema jamii yetu, basi hapa tunahitaji tuwekeze katika TBC. Tutakapowekeza katika TBC ina maana tunawekeza katika Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hata Serikali inafanya mambo mengi sana ambayo chombo cha kitaifa kipo cha TBC, kwa hiyo, kinao uwezo wa kuitangaza Serikali kupitia mambo yote ambayo wanayafanya. Kwa hiyo, tunaomba kwa Mheshimiwa Waziri kwamba tuangalie zaidi katika hii televison yetu au chombo hiki ili tuwekeze mtaji wa kutosha ambao naamini utatulipa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo ni muhimu sana, kwanza namshukuru sana Mheshimiwa Waziri na Wizara hii ya Habari kwa kuifanya Zanzibar sasa ni mwanachama katika Shirikisho la Soka Afrika. Najua hizi jitihada zilifanywa na TFF. Kwa hiyo, napongeza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nina pongezi nyingine lakini pamoja na ombi, tunajua kuna mchakato pengine kwamba Zanzibar pia iweze kutambuliwa na FIFA. Kwa hiyo, nalo hilo pia tunapongeza kama mchakato huo utakuwa unaendelea, utakuwa unakwenda kwa haraka zaidi. Kwa hiyo, hapo nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa kufanya kazi hiyo nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine nakumbuka hapa tumepisha sheria ambayo inahusiana na vyombo vya habari na wanahabari, ukatengwa mfuko wa taaluma kwa ajili ya waandishi wa habari. Kwa hiyo hili Mheshimiwa Waziri lisimamiwe vizuri, kwa sababu lengo la sheria ile moja ni kuwawezesha wanahabari. Kwa hiyo, tutenge fedha za kutosha na tulisimamie ili tuweze kuwa na wanahabari wazuri na waweze kutoa habari zao kwa uhakika.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine nije katika soka ambalo linazungumzwa; nazungumzia kuhusiana na habari za academy. Tunajua Wizara ndiyo mlezi wa michezo. Basi Wizara iweke sheria, utaratibu na vivutio ambavyo vitawawesha watu kuweka hizi academy, kwa sababu siyo rahisi academy zote zikawekwa na Serikali.

Mheshimiwa Spika, yakiwekwa mazingira na vivutio, inaweza ikachangia kabisa kuwa na wanamichezo wazuri, siyo kwa soka peke yake katika academy, tunaweza tukawa na academy za mambo mengi kama kuogelea na mambo mengine kadha wa kadha.

Mheshimiwa Spika, lingine ambalo ni muhimu, nilisikitika sana hapa kumsikia mtu mmoja anauliza katika kuchangia hotuba hii kwamba Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi yuko wapi, labda anaweza akawa ametekwa. Kwa taarifa tu, kwenda kwa Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi hakuingizi kwenye chama. Katibu Mkuu siyo kazi yake kumwingiza au kupokea mwanachama. Katibu Mkuu kazi yake ni kuongoza chama. Kwa hiyo, nami namshauri Mheshimiwa Lema, kama anataka kuja CCM, apite katika shina lake kule Arusha, apite katika ngazi ya Tawi, atapatiwa kadi na atajiunga na chama chetu. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, tunajua kwenda kumtembelea Katibu Mkuu siyo kuingia katika chama. Kwa hiyo, uje ufauate taratibu hizi za chama na miongozo ambayo ipo. Kwa nini umshike Katibu Mkuu wetu? Ninyi mmechagua Katibu Mkuu siyo zamani sana, lakini hajulikani. Hilo ndiyo tatizo, kwamba hatambuliwi. Sasa unaanza kuingia kwa Katibu Wakuu wa wenzako. Pilipili iko shamba, inakuwashia nini? Eeh, pilipili iko shamba inakuwashia nini au ndiyo kiherehere? (Kicheko/ Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hili walifahamu vizuri kwamba siyo jambo la kusema unazungumza hivyo.

Mheshimiwa Spika, lingine, nizungumze jambo ambalo limewahi kuzungumzwa na watu wengine katika sanaa. Tumeweka sanaa katika mazingira ambayo wasanii wanaweza wakajiajiri na wasanii wanaweza wakajiajiri kupitia njia mbili; wanapoweza kufanya sanaa zao wakazi- record, lakini pia huwa wanafanya maonesho ya live; tuchukulie mfano kama michezo hii ya kuigiza au muziki. Sasa kumetokea sintofahamu, kitu ambacho hakijulikani kimetokea vipi?

Mheshimiwa Spika, wasanii wameshajiandaa kufanya show, tayari wanavamiwa. Sasa ile ajira ambayo tunasema kwamba itatokana na sanaa, au itapatikana kutokana na sanaa, inakufa. Unapokwenda katika kumbi zile katika michezo hii au katika kumbi za sanaa unaweza ukakuta askari wanavamia. Sasa hili siyo jambo zuri, kwa sababu tunawavunja moyo, kwa sababu wao wanapata mapato yao kwa mujibu wa kuuza kazi zao na kufanya maonesho ya live ambayo watu wanaingia kwa vingiilio. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, namuomba Mheshimiwa Waziri kwa ushirikiano, kwa sababu inawezakana ikawa Wizara yake imeruhusu, lakini pengine inawezekana kuna muingiliano. Kuna baadhi ya Mikoa mingine wasanii hawana raha; wanaingia kwenye show wanabebwa pamoja na watazamaji. Kwa hiyo, hili naomba lingeangaliwa likafanyiwa utaratibu mzuri ili waweze kufanya kazi.

Mheshimiwa Spika, lingine katika timu yetu hii ya Serengeti Boys, ni kweli timu yetu inafika mbali, lakini tunahitaji kuwekeza katika soka. Tusiwe na Serengeti Boys hii ambayo kwa mwaka huu imeonesha mfano; na tuliwahi kuwa na timu kama hiyo miaka ya nyuma ya akina Ngasa na wenzake waliokuwa katika timu ile ya Serengeti Boys iliyopita. Inapita miaka mitano halafu ndiyo inakuja kuibuka Serengeti Boys nyingine ambayo inaweza ikatupa matumaini Watanzania. Hili jambo tunaomba liwe endelevu.

Mheshimiwa Spika, kama tunakumbuka katika soka, wachezaji wengi sasa hivi ambao wanamalizia umri wao kucheza, walitoka kwenye Serengeti Boys, lakini toka timu ile ilipokuwa ikifanya vizuri, basi mpaka leo imekuja hii nyingine ndiyo inatufuta machozi.Kwa hiyo, tunakaa sana, miaka 10, 15, ndiyo inatokezea timu nyingine ya vijana, inaundwa inakuwa inafanya vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ombi langu kwa Mheshimiwa Waziri, tuliangalie hili, timu zetu hizi ziwe endelevu. Tulishashika usukani katika kuingia mashindano ya Afrika, basi tuwe tunaonekana pale mara kwa mara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia tujaribu kufanya kitu kama hicho kingine katika riadha, isiwe mwaka huu, tumeshinda kwenye riadha au tumepata nafasi ya tano kwenye riadha katika mwaka huu, wengine wameshinda China kule, wengine wameshinda India. Sasa isije ikaja ikapotea hii, hizi nguvu ambazo tumezitoa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naunga mkono hoja.