Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

Hon. Maulid Said Abdallah Mtulia

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kinondoni

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

MHE. MAULID S. MTULIA: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia uzima. Pili, nakushukuru nawe Spika wangu kwa kunipa fursa ya kuzungumza katika Wizara yetu hii muhimu sana kwangu nikiwa kama Mbunge wa Jimbo la Kinondoni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi ni mwanachama wa Simba Sport Club na kadi yangu ni hai. Kuna maneno yamesemwa hapa lazima yawekwe sawa. Nashukuru uligundua kwamba yanayosemwa hayako sawasawa, ukaamua kusimamisha sasa mimi kwa sababu nakuja kusema sawa sasa, record tuna-balance story. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwanza timu ya Simba ndiyo timu bora kabisa Tanzania. Vile vile ndiyo timu ambayo imecheza vizuri na imeshinda mechi zake na hasa mechi zote ngumu. Wanaodai kwamba tunapendelewa, record zinaonesha tumewafunga Zanzibar, tumewafunga juzi pale na wanamkumbuka sana Kichuya na kona zake. Kwa hiyo, suala la upendeleo kwa Simba halipo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hata hiyo mbao iliyowatoa machozi, ikawafanya wasicheze fainali, sisi tuliwafunga Mwanza na wao wakafungwa Mwanza. Kwa hiyo, ukitafuta timu ambayo ina kiwango kidogo na ambayo siku ukienda kwenye mechi za Kimataifa wanatutia aibu sana hawa wanaobebwa halafu… (Makofi)

TAARIFA...

MHE. MAULID S. MTULIA: Mheshimiwa Spika, taarifa hii siipokei, kwa sababu record zinaeleweka kwamba Simba siyo muda mrefu tu ilikuwa inashiriki na imeshiriki kwa ufanisi na ukizungumza timu ambayo inatambulika nchi hii, hakuna kama Simba. Tunawashinda kwa kuanza hata kuvaa viatu, sikwambii kuvaa jezi. Kwa hiyo, Simba ni timu ambayo haiwezi kusahaulika na timu ambayo watu hawawezi kuisahau. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, cha msingi hapa ambacho nataka tukieleze ni kwamba mpira wa miguu una sheria na taratibu. Bahati nzuri msemaji kasema kabisa anataka Wizara iachane na soka, ifuate michezo mingine. Bila shaka yeye ana mchezo mwingine zaidi ya soka, japokuwa hajausema, naamini utakuwa labda kuogolea au kuvuta kamba. Kwa hiyo, hafahamu vizuri Sheria za Soka.

Mheshimiwa Spika, Sheria ya Soka imewekwa kabisa kwamba mchezaji akipata kadi tatu, haikupaswa hata Simba kukata rufaa, ni automatic kwamba mtu amevunja sheria, wasimamizi wa sheria wanatakiwa Simba wawape points zao. Kama hili halitoshi, sisi leo tunakwenda Gabon kule, kwa sababu wale ambao walipata ushindi kinyume na utaratibu walinyang’anywa zile points. Sasa nashangaa leo hao hao wanashangilia Gabon lakini utaratibu huo huo ukiwa kwa Simba inakuwa nongwa.

Mheshimiwa Spika, nilikuwa nataka niweke hayo mambo sawa, Simba ni timu makini, itachukua ubingwa, makombe yote mawili, bila kubebwa na huyo Yanga tunamsubiri tutaonana naye. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sambamba na hili, naiomba Wizara isaidie sana timu zetu hizi kubwa Simba na Yanga. Nikiri kwamba Wizara hasa Mheshimiwa Waziri, tumekubaliana tupate muda tukae tujadiliane kuhusu michezo na mambo ya sanaa katika Jimbo langu la Kinondoni, lakini timu zetu hizi za Simba na Yanga ni timu ambazo zinaunganisha umoja wetu. Leo mimi na ndugu yangu Mheshimiwa Mtolea nahitilafiana naye, lakini naungana na Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa wengine wa CCM. Leo usishangae Mheshimiwa Mwigulu Nchemba akakaa pamoja na kiongozi wangu Mheshimiwa Mbowe katika soka. Sasa hizi timu zina umuhimu mkubwa sana, kwa sasa hizi timu zinalinda mpaka utaifa wetu, tunaweza tukahitilafiana kwenye vyama, lakini tukakutana kwenye mpira.

Mheshimiwa Spika, kwa taarifa yako hatuhami timu hizi. Unaweza kuhama vitu vingine vyote, lakini ni ngumu sana kuhama timu. Sasa kama timu hizi zimefika mahali zinalinda utaifa wetu, Wizara sasa izisaidie hizi timu. Msaada ambao nautaka kwa Wizara; hizi timu zimeanza miaka ya 1930, 1936 ni timu ambazo zimeanza siku nyingi, lakini inaonekana huko nyuma viongozi walifanya kazi kubwa. Wamejenga majengo. Clubs zote zina majengo makubwa. Wamejenga imani ya watu, Clubs zote zina wapenzi wengi, lakini inaonekana sasa hivi viongozi wetu wameshindwa kututoa pale walipotufikisha wazee kutupeleka kule tunakotamani. Nahisi kuna tatizo la menejimenti, kuna tatizo la ufahamu wa uendeshaji hizi clubs zetu kama wanavyoendesha wengine.

Mheshimiwa Spika, timu ambazo zina wapenzi wa kutosha, lakini ndiyo timu ambazo zinaongoza kwa kuombaomba, ni timu ambazo zinaishi kwa kutegemea wafadhili. Wakati mwingine inashindwa hata kututumia sisi wanachama wake na wapenzi wake. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri atafute namna ya kukaa nao na atumie wataalam wake wa Wizara kuzisaidia hizi timu ili ziweze kutumia rasilimali zake ilizokuwa nazo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nirudi kwenye muziki. Mimi natoka Jimbo la Kinondoni, Jimbo la Ma-star, nina Wasanii wa kutosha kabisa. Kama nilivyosema, Mheshimiwa Waziri ameniambia tutafanya vikao vyetu na vijana hawa. Naomba jambo la kwanza ni-declare interest kwamba mimi ni mpenzi mkubwa wa wanamuziki wangu wa Kinondoni, nikianza na mtu mzima Diamond; na kwa sababu Diamond na Ali Kiba wanakuza muziki huu wa kizazi kipya, naye namtambua na nampenda sana.

Mheshimiwa Spika, pia mimi ni mpenzi wa muziki mpya unaitwa singeli. Huu huwezi kumsahau Msaga Sumu, kijana Manifongo, hata Profesa J, ametoa muziki wake mmoja anasema Kazi, Kazi. Anasema watu wafanye kazi.

Mheshimiwa Spika, hawa vijana wakati wanafanya hizi kazi zao, Wizara yetu inatakiwa iwalinde. Niliwahi kuzungumza na Diamond, yeye kama yeye muziki wake unatumika kwenye Makampuni ya Simu kama milio ya simu, lakini malipo anayoyapata hayaendani kabisa na thamani ya muziki wake. Wizara sasa iingilie, iwahoji, wanatumia vigezo gani kuwalipa hawa vijana wetu?

Mheshimiwa Spika, la pili amelisema Profesa J, nimeongea na Diamond TRA wanampelekea anadaiwa milioni 400, hivi ukidaiwa milioni 400 maana yake yeye mwenyewe mapato yake basi ni karibu shilingi bilioni 1.2. Sasa haya mapato kama ndio hivyo TRA wanasema yeye alipe kodi shilingi milioni 400, mapato yake ni mabilioni hayo, yamekwenda wapi?

Mheshimiwa Spika, vile vile vijana hawa wanahitaji kusaidiwa kwenye menejimenti. Leo Diamond katoka alikotoka, kafika pale. Hivi tunamwacha pale pale adumae au tunamwendelezaje? Yeye ameshakua sasa hivi ni kama model kwa wasanii wa Tanzania, East Africa na hata Afrika kwa ujumla. Wizara lazima iangalie namna gani inaweza kumtoa pale; na wakati mwingine siyo kwa kutoa pesa, ni kukaa nao hawa vijana na kuwasaidia katika mambo ya utawala. Kwa sababu tuna viongozi wetu wa mambo haya ya sanaa, washiriki katika kuwasaidia wasanii wetu kwa mambo ya utawala.

Mheshimiwa Spika, pia niseme, pamoja na mapenzi yangu makubwa kabisa na wanamuziki hawa na wasanii wa maigizo, bado nahimiza wasanii wetu lazima wajikite kwenye nidhamu. Nidhamu ndiyo mafanikio ya kila jambo. Haina maana ukiwa msanii ukose nidhamu. Leo wasanii wamekuwa ndio katika watu wanaoandikwa andikwa kwenye magazeti na wengine wanaamini wakifanya utovu wa nidhamu ndio majina yao yatatajwa. Mimi Mbunge wao siamini katika hilo. Naamini kwamba wafanye kazi kwa juhudi, walinde vipaji vyao, wafanye kazi kwa umakini.

Mheshimiwa Spika, kuna tatizo kwamba malipo wanayoyapata hayaendani na kazi wanayoifanya. Leo wasanii wa maigizo, wanatengeneza filamu wakati mwingine kwa shilingi milioni 15, shilingi milioni 12; anakwenda kuingia mkataba shilingi milioni 20, kazi ndio imeuzwa kabisa! Maana yake hawezi hata ku-print tena ile kazi. Kazi ndiyo imeuzwa, imeenda kwa Step Entertainment au nani au nani na huyo mtu anayenunua kazi ni kikampuni kimoja tu. Kwa hiyo, naiomba sana Wizara, iangalie hawa watu wanaonunua kazi za wasanii na kupora kabisa kazi na kuchukua hati miliki ya kazi, lazima waangaliwe.

Mheshimiwa Spika, kubwa nawaunga mkono vijana wangu, nawaandaa, tutafanya kikao na Wizara, lakini kubwa waangalie nidhamu na maadili ya Kitanzania.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. MAULID S. MTULIA: Nakushukuru sana.