Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

Hon. Aida Joseph Khenani

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Nkasi Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwanza napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kuweza kunijaalia uzima, kuweza kusimama tena ndani ya Bunge hili Tukufu. Pia napenda kupongeza na kushukuru kwa dhati Ofisi yako kwa kuweza kuokoa maisha yangu.

Mheshimiwa Spika, namshukuru pia Naibu Spika na Waheshimiwa Wabunge wote kwa ushirikiano waliouonyesha na nitakuwa sio mtu mwema sana nisipowashukuru Wabunge wa Mkoa wa Rukwa na Katavi kwa upendo waliouonyesha bila kujali itikadi za vyama vyao.

Mheshimiwa Spika, pia naungana na wazazi, Walimu, ndugu na jamaa katika kuomboleza msiba uliotukuta juu ya wanafunzi ambao walituacha. Tunasema kazi ya Mungu hatuwezi kuhoji, lakini tumepokea, ingawa mambo haya hayazoeleki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitakwenda kuchangia mambo machache nikianza na upande wa habari. TBC ni Television ya Taifa wote tunajua, lakini inachangiwa na walipa kodi wa nchi hii wakiwepo wa Mkoa wangu wa Rukwa, leo tunapokuwa tunajadili bajeti, wanashindwa kujua wawakilishi wao wamezungumza nini? Je, wamezungumza yale waliyowaambia? Kwa sababu hawawezi kuona tena Bunge live.

Mheshimiwa Spika, yawezekana hata nia njema ya Serikali hasa anapokuwa anazungumza Mheshimiwa Rais kwamba watu wafanye kazi, lakini tunafahamu fika kwamba Rais anapokuwa anafanya jambo lolote anaonekana live. Rais huyu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alichaguliwa kwa kura za Watanzania, Wabunge wamechaguliwa kwa kura za Watanzania. Sijajua utofauti mkubwa uliojitokeza hapo katikati.

Mheshimiwa Spika, nawaomba Waheshimiwa Mawaziri pamoja na sisi Wabunge, mimi bado linanichanganya kwenye kichwa changu. Tofauti ni nini? Ni nafasi au ni kazi kama alivyozungumza? Kwa sababu ule muda anapoonekana yeye, wananchi wanaacha kazi wanamsikiliza, basi angalau hata kipindi hiki cha bajeti sasa ili wananchi waweze kuwaona Wawakilishi wao wanafanya nini? Je, wanazungumza yale waliyowaambia wazungumze au inakuwaje? Sidhani kama itakuwa busara au uzalendo anaousema yeye aonekane, Waheshimiwa Wabunge wasionekane, wakati wote walikwenda kuomba kura na wananchi ni wale wale ambao wanatakiwa waone nini kinazungumzwa na nini kinatendeka. Sidhani kama uzalendo uko mahali hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri labda aje atuambie kwamba pesa zinakuwa nyingi sana kuonyesha Bunge, lakini upande wa Rais na vitu vingine pesa zinakuwa siyo nyingi. Wakati huo huo TBC inaweza kuonyesha mambo mengine. Napenda tupate taarifa Mheshimiwa Waziri atakapokuja ku-wind-up kwamba kwa mara ya mwisho ni lini taarifa za Upinzani zilionyeshwa TBC? Nimekuwa mfuatiliaji sana wa TBC. Sasa kama TBC imekuwa na ubaguzi, ni vyema Mheshimiwa Waziri aje kutuambia tujue. Ni lini kwa mara ya mwisho TBC ilionyesha habari za Upinzani, wakati wote ni Wabunge na wote ni Wawakilishi wa wananchi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la pili kwa upande wa habari, ni juu ya Waandishi wa habari. Pamoja na Bunge kutoonyeshwa live, Watanzania hawa wanategemea kupata habari kwenye vyombo mbalimbali. Leo waandishi wa habari wanakuwa na hofu ya kutoa habari. Hatujasikia tamko kutoka kwa Mheshimiwa Waziri linaloonesha moja kwa moja uzito juu ya ulinzi wa Waandishi wa Habari. Tumeangalia matukio kadhaa, achana na hayo ya huko nyuma ya akina Mwangosi na watu gani, lakini bado hatujaona jitihada za Serikali juu ya ulinzi wa Waandishi wa Habari.

Mheshimiwa Spika, naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja atuambie mikakati yake aliyoipanga juu ya Waandishi wa Habari. Wananchi hawawezi kujua chochote bila kuwaona au kuwasikiliza Waandishi wa Habari.

Mheshimiwa Spika, Mkoa wangu wa Rukwa kuna maeneo hakuna TV, wanategemea kusikiliza redio. Hizo redio zenyewe sasa hivi habari haziendi kama zilivyo; sijui mpaka zichujwe wapi, zifanywejwe! Sasa haya mambo inafikia mahali yanakuwa na ukakasi. Tunaomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja atuambie ni mikakati gani ameiweka juu ya ulinzi wa Waandishi wa Habari pamoja na wamiliki wa vyombo vya habari? Sambamba na hilo, ile ripoti ya Mheshimiwa Nape tunataka tuisikie, kwa sababu hapa ndiyo mahali pake, aje atuambie nini kinaendelea juu ya kile kitu? Kama kuna kiini macho tujue kwamba imeshindikana, lakini imeshindikana kwa nini?

Mheshimiwa Spika, upande wa michezo, hatuwezi kuboresha michezo tukiwa hatujaboresha viwanja vya michezo. Hapa tutapiga story siku zote na kutafuta mchawi. Kwa sababu huwezi kusema watu waje wacheze, unategemea kwamba waje wacheze Dodoma tu; kwa sababu hawa watu wanatoka kwenye Wilaya na Mikoa. Huko kwenye Wilaya na Mikoa hali za viwanja ni mbaya.

Mheshimiwa Spika, katika viwanja hivyo kuna viwanja vinamilikiwa na Chama Tawala; siyo dhambi, basi viendelezeni. Viko kwenye hali mbaya! Shida ni nini? Yawezekana bado hakujawa na mikakati thabiti kwa sababu hatutegemei kuangalia Serengeti boys wale wale wakae miaka 20, tunataka mikakati ya wale ambao wanaandaliwa sasa kuja kuwa Serengeti Boys wa mwaka 2020. Hawa watu wanapatikana wapi? Wanapatikana kwenye Wilaya na Mikoa. Ni utaratibu gani umewekwa ambao utakuwa rafiki kwa hawa vijana wanaotoka kwenye mikoa na wilaya?

Mheshimiwa Spika, siamini kwamba Mkoa wangu hakuna wachezaji wazuri. Mkoa wa Rukwa wanakula samaki, kuna watu wanacheza vizuri sana. Ni lini utawajua? Utawajua kwa kufuata ule utaratibu uliokuwepo zamani. Kulikuwa na michujo inafanyika shule za msingi na sekondari. Nakumbuka kwa mara mwisho UMITASHUMTA pamoja na UMISETA wakiwa wanakwenda Geita nafikiri, ilitokea tamko hawarudi wale watoto. Tunaomba mtuambie sasa, hiki kitu ndiyo kimefutwa moja kwa moja au kuna mikakati gani inaandaliwa juu ya suala hili? Maana imeshakuwa sasa hatuelewi, tupo tu.

Mheshimiwa Spika, siamini kama wachezaji wengi wanatoka Dar es Salaam na Mwanza tu; na Mikoa mingine wachezaji wapo. Wekeni mikakati, wekeni mazingira rafiki ya kuwapata wachezaji wazuri na wapo, wanapatikana maeneo yote.

Mheshimiwa Spika, vile vile tusiwekeze kwenye mpira peke yake. Kama tumeshindwa kwenye mpira, lazima tuwe na plan B. Tutafute mchezo mwingine ambao hatutaitwa shamba la bibi Tanzania, haiwezekani! Naamini vipaji vipo vingi tu, lakini ni namna ya kupata hivyo vipaji na kuvifuata kule viliko. Kwa hiyo, kumekuwa na shida kidogo.

Mheshimiwa Spika, vazi la Taifa limekuwa likizungumzwa sana. Siamini kwamba mpaka leo tumeshindwa kupata vazi la Taifa. Mheshimiwa Waziri, atakapokuja kufanya majumuisho atuambie, maana nimeona huku pembeni nyuma ya hiki kitabu, lakini haijaonesha kwamba ndiyo hili, sijui! Nafikiri ndiyo utaratibu unaandaliwa. Muda umekuwa mrefu, mpaka lini kwa mwendo huu unaokwenda? Kama ndiyo hili limepitishwa, basi mtuambie lilivyopitishwa.

Mheshimiwa Spika, hiki kitu inatokea, hata ukiangalia kwenye muziki, watu wengi hasa wanawake unakuta mavazi wanayovaa pale ni tofauti na wanaume, wao watavaa suti nzuri na tai safi kabisa, lakini wanawake wanavaa vibaya! Leo mtawaambia nini wakati hakuna vazi lililoteuliwa? Tunaomba mtakapokuja, tena Mheshimiwa Naibu Waziri,yeye ni mwanamke, kwa sababu inapotokea kudhalilishwa, hawadhalilishwi wale walioko pale na wanawake wengine wote wanaozunguka kwenye jamii hizi tunapata aibu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na hilo, lilizungumzwa sana siku ya Ijumaa suala la Mwenge. Naomba Mheshimiwa Waziri aje anipe ufafanuzi kidogo. Kwenye Mkoa wangu wa Rukwa Wenyeviti wamekamatwa kwa kutochangisha pesa za Mwenge. Naomba kujua, ni sheria ipi ilitumika kuwakamata Wenyeviti hawa kwa kutochangisha pesa za Mwenge? Kwa sababu kitu kinachoitwa mchango kwa mimi ninavyoelewa, ni hiari siyo lazima. Sasa ni sheria ipi ilitumika kuwakamata Wenyeviti hao wa Serikali ambao hata mshahara hawalipwi; na kila siku tunajadili hapa, hakuna siku imepitishwa Wenyeviti wataanza kulipwa mshahara au posho. Sasa ni sheria gani ilitumika kuwakamata Wenyeviti hawa? Naomba kauli ya Serikali Mheshimiwa Waziri atakapokuja ku-wind up.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, kichwa changu bado hakijakaa vizuri. Ahsante kwa nafasi uliyonipa kutoa mchango huo.