Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbulu Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Nami niungane na wenzangu wote ambao wametoa pole kwa wafiwa wote na kweli Mungu azilaze roho za Marehemu watoto wetu mahali pema peponi. Amina.
Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nitoe pongezi zangu kubwa sana kwa Mheshimiwa George Huruma Mkuchika ambaye alikuwa DC katika Wilaya yangu ambayo mimi nilikuwa mdogo sana kwa kujenga uwanja wa michezo, ambao umefanya mimi kama Flatei Massay kuwa mwanamichezo kutokana na viwanja ambavyo huyu mzee wetu ambaye ni Mbunge humu ndani ameifanya kazi hiyo vizuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa nini naamua kusema haya? Nasema haya kwa sababu kuna watu wanatakiwa kuenziwa katika Taifa letu. Kwanza, wamefanya kazi nzuri, uwanja wa Julius Nyerere ulioko Mbulu umejengwa kwa nguvu kazi ya kwake mwenyewe. Namkumbuka alikuja mimi nikiwa mtoto sana, nina miaka kama sikosei mitano. Nilikuwa naona jinsi akivaa magwanda yake ya kijeshi akiwa Captain na kuhamasisha wananchi wa Mbulu kujenga ule uwanja. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa uwanja umekuwa mzuri na naamini wachezaji wengi wametokea pale na wana riadha wengi wametoka pale. Sasa niiombe Wizara iangalie namna gani ya kuweza kusaidia viwanja hivi vya michezo? Kwa sababu wanariadha wengi ambao kimsingi wameonekana katika Taifa letu kuleta zawadi ya ushindi katika medali za Kimataifa wametokea pale, mfano, Filbert Bayi, John Stephen
Akhwari, John Bayo, hawa watu wote wamefanya kazi na kulitangaza Taifa hili katika ulimwengu huu wa Michezo na wameweka rekodi ambayo mpaka sasa naamini haijavunjwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naiomba Wizara iangalie sana uwanja ule, hata ikiwezekana basi waangalie namna ya kusaidia hata kwa kutumia maeneo ya ushauri tu nini kifanyike ili angalau michezo iweze kuendelea katika maeneo yale.
Mheshimiwa Spika, pia nataka kusemea hawa wazee wetu waliotusaidia sana kuitangaza Tanzania. John Stephen Akhwari, kwanza namshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Naibu Waziri, alifika akamtembelea mzee yule. Ana vikombe kama 15, Mheshimiwa Naibu Waziri aliona mwenyewe. Kwa sababu alifika, yule babu sasa anazeeka na hawezi kuishi miaka mingi kutokana na umri wake sasa. Naamini historia yake inaonekana na Mheshimiwa Waziri anayo. Hebu angalieni basi namna ya kuangalia malalamiko yake ambayo alimpa Mheshimiwa Waziri. Mimi ni Mbunge wake lazima nimwambie leo. Asingeweza kupata nafasi yoyote, nafasi ya kumsaidia ni wakati huu akiwa hai.
Mheshimiwa Spika, wakati ule walikuwa wanawasikiliza Taifa, ilikuwa ni ngumu sana kupata zile hela ambazo wanatunzwa wanaposhinda katika zile medali ambazo zimeisaidia nchi hii kusifika wakati huo. Kwa kweli walikuwa wanasaidia Tanzania na kuipatia heshima kama nchi. Hawakuwa wanapata jambo lolote.
Mheshimiwa Spika, sasa basi waje wasaidie kwa sababu wamekuja wale watu wa olympic kutoka nchi ya Australia ikitaka kumjengea huyu baba au babu uwanja wa michezo, lakini kwa sharti moja tu, ni kwa jina lake. Kwa bahati mbaya sana Serikali wakati uliopita haikukubali kabisa jina la uwanja huo kuitwa kwa jina lake. Wale wafadhili wamekuwa kila siku wakijaribu kutafuta namna rahisi ya kufanya muunganiko kati ya Serikali yao na sisi ili kumsaidia kumjengea mzee huyu ambaye ametangaza Tanzania katika ulimwengu huu wa michezo.
Mheshimiwa Spika, basi naomba Serikali ione namna gani ya kusaidia. Nafiri Mheshimiwa Naibu Waziri siku ile mzee yule alimwambia masikitiko yake makubwa. Sasa kabla hajafika mahali Mungu akamchukua kwa sababu ni mzee, waje basi wamsaidie haraka ili angalau jina lile lisifutike. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lingine ambalo nataka niliseme, Mbulu tumetoa wanamichezo wengi wa Kimataifa, siyo kwa sababu tu ni maarufu sana, hapana! Ni kwa sababu ya nature ya eneo lenyewe. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri, sasa hivi wanamichezo wengi hasa wanariadha kutoka Mbulu wanachukuliwa maeneo mengi mengi na watu hufadhili mmoja mmoja. Sasa naomba Wizara ijaribu kufanya jambo moja tu, isiondoe sasa eneo la michezo ya mazoezi kutoka Mbulu kuipeleka Dar es Salaam. Kwa sababu sasa mnavyofanya namna hiyo saa hizi, historia inaweza kufutika kwa sababu moja tu.
Mheshimiwa Spika, ukimtoa mtu Mbulu kwenye kitu kinachoitwa uwanda wa juu, sisi kule bahati nzuri hali ya hewa inatu-favour na milima inawasaidia wachezaji. Sasa ukimtoa mchezaji toka Mbulu ukamfanyia kambi Dar es Salaam ili aende kushinda, anashindwa kushinda kwa sababu ya mvuto anaotumia, upepo ule au hewa ya Dar es Salaam iko zero degree wakati huku Mbulu kuna 1,500. Sasa ukimtoa pale akafanye mazoezi Dar es Salaam akienda Ulaya, hawezi kushinda.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, sababu hizo nafikiri ni za kitaalam sana; mimi sio Daktari lakini naziona na ninazijua. Kwa hiyo, wasaidie basi kuliko Chama kile cha riadha kiamue moja kwa moja kwa sababu wao ndio viongozi waamue kambi kufanyika Dar es Salaam, wanaweza kufanya hivyo kwa sababu wao ni viogozi, lakini waone, Filbert Bayi wakati huo walikuwa wanafanya mazoezi na kufanyia pale Mbulu na wakashinda. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa sababu hii basi, walishinda kutoka na hali ya hewa iliyoko pale na nature ya mazingira ya kule ni milima na miinuko, ili akifika kule aweze kumaliza zile mbio akiwa na nguvu na kuisaidia nchi yetu tupate medali. Nimeona niseme hii moja kwa moja hapa kama mchango wangu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pili, nielezee sasa eneo la michezo. Michezo ni lazima uanzie ukiwa mdogo. Wenzetu ukiangalia historia ya michezo kwa sisi wanamichezo utaona watoto wetu wanafundishwa wakiwa watoto. Nami niungane na wenzangu kwa msingi huo ni vizuri kumfundisha mtoto akiwa mdogo akafahamu na kumjengea ile behavior akaweza akafanya michezo akiwa utotoni. Leo hii ukimfundisha punda mzee kulima, hawezi. Ni lazima basi hii michezo irudishwe shuleni. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, linguine, liko jambo ambalo nataka niseme kwenye sanaa na hasa Bodi ya Filamu. Bodi ya Filamu ina harufu ya rushwa. Naomba nirudie, ina harufu ya rushwa kwa sababu kwa sisi wasanii, nami nataka nikwambie, mimi ni msanii, lakini ukitaka kuomba chochote kwenye Bodi ya Filamu, wanaweka hali ambayo haimruhusu msanii kupata anachotaka. Kwa mfano, mpaka Bodi ikae unahitaji miezi mitatu.
Mheshimiwa Spika, ukitaka kufanya inter-connection wewe msanii wa Tanzania na Msanii aliyeko Ulaya, akija Tanzania inabidi aache kabisa kila kitu, anatakiwa asije na camera. Nashangaa sana, unamruhusu asije na camera wakati huo unamkubalia aingie na simu, sasa kama ni usalama wa nchi, sijui inawezekana. Simu nyingine zina capacity kubwa. Kama ukitaka asichukue hiyo picha, ataweza hata kutumia simu, si atachukua tu!
Mheshimiwa Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri, nimepeleka malalamiko katika Ofisi yake na nimeandika mwenyewe. Walikuja Wabunge kutoka nchini Norway, ni wafadhili wa miradi mingi nchini, lakini Bodi ya Filamu ikawazuia wale Wabunge wasiingie na camera jambo ambalo nililishangaa sana, likanifanya nipate mshtuko kwa sababu wale Wabunge walipoingia, walikuja wakiwa watupu wakisema, kwa nini hatukupewa?
Mheshimiwa Spika, bahati nzuri walifuata sheria za Tanzania, wamefuata sheria za mambo ya nchi za nje, wamefika Wizarani, wameandika, wametumia Ubalozi wa Norway, wametumia Ubalozi wetu ulioko Sweden, wameruhusiwa; wamekuja kwenye Wizara yako, wameomba kibali. Kilichowafanya wakatazwe wasipate kibali hicho ni Bodi ya Filamu. Wameomba, muda unatosha na bahati mbaya hawakupata majibu. Kwa nini hawakupata kibali cha kuingia na camera? Hiyo tu.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri, kwenye Bodi ya Filamu kuna shida pale; nami na-declare ninao ushahidi na nimempa kwa maandishi na nimesema kwa maandishi na Balozi pia amenipa barua yake kwa maandishi na nimempa copy yake. Naomba akachunguze Bodi ya Filamu, kuna shida pale. Bahati nzuri nimekwenda mwenyewe pale, ni mara tatu nimeshindwa kupata ninayotaka kuyafanya. Mara moja tu Mheshimiwa Nape alipokuwa Waziri alipiga simu ndiyo nikasaidiwa kwa sababu tu mimi ni Mbunge. Je, wasanii wangapi wana shida pale? Aangalie Bodi hii, kwa nini inatoa masharti magumu? Kama ni shida, tujue. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimeona nilisemee vizuri hili na nilisemee kwa uchungu mkubwa kwa sababu tunapoteza heshima. Anapokuja mtu anayefadhili nchi hii, lakini inafika mahali anakwamishwa kwa jambo dogo tu...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, nashukuru na naunga mkono hoja, lakini naomba kama hataleta majibu haya, nitashika shilingi.