Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu lakini pia kukushukuru wewe kwa kunipa nafasi hii. Nikupongeze sana kwa namna unavyofanya kazi ya kuliongoza Bunge hili, kwa umahiri mkubwa ikiwa ni pamoja na timu yako. Hongereni sana, chombo kinakwenda barabara, tumeridhika na utendaji wako wa kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba kuchangia hotuba ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na nitakwenda moja kwa moja kwenye haki za wasanii. Naomba niongelee tu kwenye eneo hili la wasanii. Wasanii wetu wa Tanzania wanafanya kazi nzuri. Moja kati ya kazi kubwa ambayo wanaifanya ni pamoja na kuitangaza nchi yetu. Wako wasanii wazuri ambao wanafanya vizuri kwenye michezo kwa maana ya mpira wa miguu lakini pia kwenye kuimba na mambo kadha wa kadha.
Mheshimiwa Spika, napenda niwatambue baadhi ya wasanii hapa ambao wanafanya vizuri kwa mfano, Mzee Jongo, Ray, Diamond, Khadija Kopa, Ali Kiba, Profesa Jay na kijana mmoja machachari sana ambaye anawakilisha Mkoa wa Ruvuma yuko katika Bendi ya TOT anaitwa Neka, kijana huyo anatoka katika Wilaya ya Namtumbo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hawa wasanii wetu ni vizuri kabisa tukahakikisha kwamba wanapata haki zao za msingi ili kuweza kufanya usanii wenye tija. Inaonesha kwamba hawa wasanii kumekuwa na sheria ambayo inawabana. Wakati mwingine wanapenda kurekodi video zao ili watengeneze kanda lakini wanakuwa wanabanwabanwa, kwa mfano, labda anahitaji kwenda kurekodi kwenye eneo la daraja lile la Kigamboni, visheria vinawabanabana wanashindwa kufanya hivyo. Wakati mwingine wanatamani hata watumie labda gari la polisi kwa ajili ya kurekodi lakini wanashindwa kufanya hivyo, lakini wakitoka hapa wakaenda nchi za wenzetu wanapewa ushirikiano wa kutosha.
Mheshimiwa Spika, naomba kama kuna sheria inawabana kutumia vitu hivyo basi tuweze kuileta hapa tuirekebishe ili wapate haki za msingi za kuweza kufanya recording ambayo itawasaidia na watakuwa wanafanya uwekezaji wenye tija kwenye usanii huo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niende pia kwenye suala la usikivu wa TBC. Kule kwetu Nyasa bado TBC haisikiki vizuri. Namwomba Mheshimiwa Waziri afanye kazi ya ziada, kwa sababu mpaka sasa hivi tunasikiliza habari za Malawi. Kuna ka-station fulani ya ka-Malawi kanachezacheza pale, sisi hatutaki, sisi sio wa Malawi, sisi ni Watanzania, weka TBC, acha maneno, weka muziki. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, juzi alisimama Mbunge mmoja hapa, nadhani matatizo ya kwenye jimbo lake yamekwisha kabisa hata wananchi wake wamekuwa wana hali nzuri kiasi ambacho hawana changamoto yoyote amejikuta anaacha kushughulikia mambo ya jimbo lake anaenda kushughulikia mambo kama ya shilawadu. Amesimama hapa akiongelea suala la Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi kufichwa, mimi nashangaa sana Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi amefichwa wapi au kutekwa kwa namna moja au nyingine wakati huyu Katibu Mkuu yuko Arusha. Naomba niseme haya hayamhusu, ashughulike na ya kwake yanayomhusu. Pia huyu Kinana ni Katibu sio wa lelemama huwezi kumlinganisha Katibu huyu wa Chama kikubwa Chama cha Mapinduzi ukamlinganisha na Makatibu wa vyama ambavyo vinafanana na SACCOS fulani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Kanali Mstaafu Kinana ni kiongozi mzuri, ni mwamba wa vita, ni mpiganaji hasa hasa kwenye Chama chetu cha Mapinduzi. Pia ni mkweli, ni mchapakazi na hana uwoga kwenye kusemea Chama chake cha Mapinduzi. Sasa nashangaa ukamchukua Kinana unamlinganisha na chama chake na wala nisimfiche ni Mheshimiwa Lema, anamlinganisha Kinana gwiji la siasa, mwanaume kabambe ambaye anaweza kusimamia Chama cha Mapinduzi ipasavyo na Katibu wake ambaye haeleweki kama yuko duniani au yuko akhera mpaka sasa hivi, hii inasikitisha sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimshauri tu kaka yangu Lema na mimi niseme toka nimefika hapa nimeanza Bunge hili la Kumi na Moja sijawahi hata siku moja kusikia akiongelea masuala yanayohusu jimbo lake amejikita kwenye mambo ya diplomasia ya kitaifa na kama nasema uongo rejeeni Hansard zake zote mtaona. Niseme hivi kwamba kama anahitaji aje tu CCM wala hatuna hiyana tutampokea lakini hii kutafuta chokochoko sio njema.
Mheshimiwa Spika, niende kwenye Jimbo hilo la Arusha, naomba nimshauri kaka yangu Lema ajikite huko, watu wa Arusha bado wana changamoto kubwa sana wanahitaji wasemewe na Mbunge wao, badala yake yeye amejikita kwenye mambo ya ushilawadu na kwenye mambo ya unabii…
Mimi niseme kazi ya unabii siyo yake kwa sababu ni nabii wa uongo.
Mheshimiwa Spika, alitabiri hapa Dkt. John Pombe Magufuli atakufa na hajafa, ndio kwanza anaendelea kutekeleza majukumu yake, kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi ipasavyo na maendeleo yanaonekana. Kazi anazozifanya Dkt. John Pombe Magufuli…
Ni kazi nzuri na wanachi wote wanazikubali.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, unabii wake ni wa uwongo na mimi leo nataka nimbatize jinaJina ninalombatiza leo hii ni nabii Israel mtoa roho za watu.
TAARIFA...
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana na ndiyo maana nimesema uko vizuri na unachapa kazi ipasavyo na tunakubaliana na utendaji wako wa kazi. Kwa sababu wako watu sasa wanashindwa kujitambua nini aseme hata ulivyokuwa unajaribu
kumfundisha, tunakushukuru umekuwa mwalimu kwetu, umemfundisha hapa msemaji mmoja alikuwa anaongelea vyeti, mara ooh siyo lazima uwe na vyeti, mara nini, haeleweki, Mbunge wa Ubungo umemfundisha hapa vizuri lakini unaendelea kutoa hiyo elimu hata Mwalimu na yeye umemfundisha vizuri. Tunakushukuru sana na tunakuombea kwa Mwenyezi Mungu endelea kuchapa kazi tuko nyuma yako tunakuunga mkono. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hiyo taarifa siipokei kimsingi amenipotezea muda na naomba unilindie dakika zangu, nina mambo ya msingi sana ya kuchangia hapa. (Makofi/ Kicheko)
Mheshimiwa Spika, naomba nichukue nafasi hii kwa utulivu sana kumpongeza sana Waziri mwenye dhamana ya habari. Sina mashaka na utendaji wake wa habari, sina mashaka na utendaji wake wa kazi, ni Waziri mahiri, ni Waziri ambaye ameshafanya kazi Wizara mbalimbali na kila eneo alilopewa kufanya kazi amefanya vizuri. Kwa hiyo, ni matumaini yangu atawatendea haki wasanii wa nchi hii na ataitendea haki Wizara hii.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba niwatie moyo Mheshimiwa Waziri, Naibu pamoja na timu yako yote fanyeni kazi. Hizi kelele za chura hazimzuii mwenye nyumba kulala, wala kelele za chura hazimzuii chura kunywa maji, kwa hiyo endeleeni kuchapa kazi, tuko nyuma yenu tunawaunga mkono. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya maneno haya, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.