Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Sikudhani Yasini Chikambo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, kwanza napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu aliyenijalia kuwepo katika Bunge hili. Haikuwa rahisi lakini kwa uwezo wake leo niko hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa dhati ya moyo wangu napenda sana niwashukuru wananchi wa Mkoa wa Ruvuma kwa kuendelea kukiamini Chama cha Mapinduzi, kwa kuchagua kwa kura nyingi viongozi wanaotokana na CCM. Wamempa kura nyingi Mheshimiwa Rais, lakini wamechagua Wabunge wote wanaotokana na CCM, nawashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niahidi mbele yako kwamba nitashirikiana na Wabunge wa Mkoa wa Ruvuma wanaotokana na CCM nikiamini kwamba wao wamechangia uwepo wangu katika Bunge hili. Ninaahidi kufanya nao kazi hasa zinazohusu akina mama usiku na mchana. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kabla sijaendelea kusema niunge mkono hoja, lakini nianze kuchangia hotuba ya Waziri Mkuu. Naomba nipongeze sana hotuba hii imekaa vizuri lakini kwa kuwa ni wajibu wetu kusema neno na mimi naomba niseme neno.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie suala la shilingi milioni 50 za kila kijiji. Sote tunafahamu kwamba Mheshimiwa Rais wetu alitoa ahadi kwa wananchi wetu kwamba Mwenyenzi Mungu akimjalia kushinda katika nafasi hiiā€¦
MHE. ZUBEDA H. SAKURU: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu utaratibu.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Sikudhani, naomba ukae.
KUHUSU UTARATIBU......
MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimwambie kwamba miongoni mwa mabingwa wasemaji bila kusoma ni pamoja na mimi. Naomba nimhakikishie hilo na ili kuthibitisha naomba niendelee. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze kwa kuzungumzia shilingi milioni 50 ambazo Mheshimiwa Rais alitoa ahadi kwa wananchi wetu. Namuomba awe anaangalia ahakiki kama hapa nilipo sisomi ili kumthibitishia kwamba niko vizuri na sina shaka, nimepikwa nikapikika. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais wetu wakati anaomba kura alitoa ahadi ya kutoa shilingi milioni 50 kila kijiji na mimi napongeza ahadi hii na sina shaka ahadi itatekelezwa na kwa bahati nzuri kwenye hotuba ya Waziri Mkuu imeelezwa. Kwa kuwa zoezi hili la ugawaji wa hizi pesa wamesema watahakikisha zinatolewa kupitia SACCOS na baada ya utaratibu huu kukamilika kinachofuata sasa ni utekelezaji. Nashauri kabla hatujafika kwenye hatua ya utekelezaji maelekezo yatolewe kwa wananchi wetu ya namna njema ya upatikanaji wa pesa hizi ili kusitokee mkanganyiko. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivyo mbele ya Bunge lako kwa sababu hivi tulivyo hapa kule vijijini tayari akina mama wanaendelea kuchangishana pesa na kufungua akaunti. Inawezekana kabisa wakafungua akaunti lakini mwishoni mtu akajikuta hapati kile alichokusudia. Kwa hiyo, naomba yatolewe maelekezo wakati tunaingia kwenye utaratibu huo kila mmoja anajua vigezo gani vitatumika vya kutoa hizi pesa. Sina shaka na Serikali yangu, naamini watatekeleza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu amezungumzia pia masuala ya Mfuko ule wa TASAF. Mheshimiwa Waziri Mkuu atakubaliana na mimi kwamba jambo hili ni jema na kwa kweli linasaidia kaya maskini na kwa bahati nzuri wameelezea kaya ambazo zimenufaika na kiasi ambacho kimetolewa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama vile ambavyo tunahakiki watumishi hewa, naomba na katika eneo hili turudi tuhakiki wanufaika. Kwenye eneo hili kuna watu ambao wananufaika lakini siyo maskini kama vile ambavyo tumekusudia. Kwa hiyo, inawezekana kabisa jambo likawa jema lakini lisilete manufaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe Ofisi ya Waziri Mkuu kama vile ambavyo tunahakiki watumishi hewa basi na kwa upande wa TASAF kwa kuwa tumekusudia kusaidia kaya maskini, twende tusaidie kaya maskini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie suala la ugawaji wa maeneo ya utawala. Kama nilivyosema kwamba mimi natokea Mkoa wa Ruvuma lakini naomba niizungumzie Wilaya ya Tunduru. Wilaya ya Tunduru ni miongoni mwa Wilaya kongwe katika nchi hii, ina Kata 39 na Majimbo mawili. Tumezungumza kwenye vikao vyetu na tumeomba kupata Wilaya nyingine. Niombe kupitia ofisi yake wakati utakapofika basi waiangalie na Wilaya ya Tunduru kwa kuiweka katika mgawanyo ule wa kuongeza Wilaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nafikiri huwa tunaongeza maeneo ya utawala kwa ajili ya kurahisisha kutoa huduma kwa wananchi wetu. Kwa dhati ya moyo wangu na kwa bahati nzuri Waziri Mkuu ni msikivu na naamini pale alipo Waziri Mkuu ananisikia, wakati utakapofika wataangalia na kuipa umuhimu Wilaya ya Tunduru. Wala hapigi story Mheshimiwa Waziri Mkuu pale ananisikiliza. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie suala la asilimia 10 ya mikopo ya wanawake na vijana. Kwenye eneo hili wachangiaji wamesema kwamba utaratibu wa siku za nyuma tulikuwa tunaziagiza Halmashauri zetu zitenge asilimia 10 kwa ajili ya kusaidia mikopo ya wanawake na vijana. Mimi naomba ukubaliane na mimi kwamba yako maeneo hayafanyi vizuri. Naomba sana sana tusisitize Halmashauri zetu zitenge hizi pesa kwa ajili ya kusaidia wanawake na vijana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, yako mengi ya kusema lakini naomba niseme mimi ni mmoja wa Wajumbe wa Kamati ya Masuala ya UKIMWI. Wewe utakuwa shahidi, Kamati ya UKIMWI imewasilisha taarifa yake hapa, miongoni mwa mambo ambayo tumekuwa tukiyajadili kwenye vikao vyetu ni kwamba utaratibu wa uendeshaji wa Bunge hauna tofauti sana na utaratibu wa uendeshaji wa Halmashauri. Utakubaliana na mimi kwenye Halmashauri zetu Kamati hizi haziko kama zilivyo kwenye Bunge. Tulileta maombi kwako, tulikaa na wewe, nikubali inawezekana kabisa kabla sijawa Mjumbe wa Kamati pengine nilikuwa sijajua ugumu na tatizo kubwa lililopo la dawa za kulevya na UKIMWI lakini nilipokuja kwenye Kamati hii nimeona kwamba hili tatizo ni kubwa na Wajumbe wenzangu watakubaliana na mimi kwamba ni tatizo kubwa. Tumewasilisha hapa bajeti yetu, tutaomba Bunge liridhie kwa kile ambacho tumeomba na wakati utakapofika basi kitolewe kwa wakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, tulikuwa tunaomba kwa heshima na unyenyekevu na tunaamini nyie viongozi mlioko mbele ni sisi ndiyo ambao tumewaweka na kiongozi msikivu ni yule anayesikia kilio cha watu anaowaongoza, tunaomba sana Kamati hii irudi kwenye mfumo uliokuwepo huko nyuma ambapo Wajumbe wa Kamati hii walikuwa wanapata nafasi ya kushiriki kwenye Kamati nyingine. Wanakuwa na nafasi ya kwenda kuzungumzia masuala ya barabara, maji, zahanati lakini leo sehemu kubwa sisi ni ku-deal na masuala ya maboksi ya condom, masuala ya dawa za kulevya na uingizaji wa vidonge hivi vinavyowasaidia wenye UKIMWI. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nikuombe kwamba katika eneo hili, naamini wewe ni msikivu na Spika ni msikivu na wote nyie ni wasikivu na mmekaa hapo kwa ajili ya kusikiliza kilio cha watu mnaowaongoza na sio wengine ni pamoja na sisi Wajumbe wa Kamati hii, tuko tayari kufanya kazi. Kwa nafasi hii naomba sana nimpongeze Mheshimiwa Jenista Mhagama lakini nimpongeze na Naibu wake wametupa ushirikiano sana, pale tulipowataka kwenye Kamati yetu wamekuja wametupa maelezo, niombe sana mliangalie hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini liko tatizo lingine la MSD. Tumefika sisi mpaka MSD wanadai pesa na inawezekana kabisa itafika wakati watashindwa kabisa hata kupakua mizigo bandaraini. Kuna pesa ambayo wanaidai Serikalini na kwa bahati nzuri Naibu Waziri wa Afya tulikuwa naye wakati tumeenda MSD na yeye aliahidi kwamba kile kiasi cha pesa kitatolewa. Niombe watekeleze ahadi yao ya kuwalipa MSD.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii, naunga mkono hoja. Nawatakia kila la kheri na kazi njema, ahsante sana.