Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Fatma Hassan Toufiq

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Na mimi naomba nichukue nafasi hii kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema na kuweza kusimama katika hili Bunge Tukufu kuzungumzia kuhusu hotuba ya Waziri Mkuu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kuzungumza ndani ya Bunge hili, naomba nichukue fursa hii kuwashukuru sana wanawake wa Mkoa wa Dodoma kwa kunichagua na kunifanya niwe Mbunge wao. Sambamba na hilo niwashukuru pia wanaume wa Mkoa wa Dodoma kwa kuwaruhusu wake zao na watoto wao kuweza kuja kunichagua kwa hiyo, nawashukuru sana wote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue fursa hii kwa unyenyekevu mkubwa kumpongeza sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi nzuri anayoifanya lakini pia nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba nzuri aliyoitoa. Nalipongeza pia Baraza la Mawaziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda sana kuzungumzia kuhusu hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, ukurasa wa 73 ambao ulikuwa unazungumzia suala la Ustawishaji Makao Makuu. Naamini sote tunafahamu kwamba suala la Ustawishaji wa Makao Makuu lilianzishwa mwaka 1973 lakini kwa masikitiko makubwa sana mpaka leo hii hakuna sheria ambayo inazungumzia uwepo wa Makao Makuu Dodoma. Kukosekana kwa sheria hiyo imechelewesha sana kuhamia Makao Makuu Dodoma. Pamoja na taarifa nzuri ambayo imetolewa kwamba kuna baadhi ya mambo yamepangwa katika Ustawishaji Makao Makuu, lakini kumbe ipo sababu ya msingi kabisa ya kutungwa sheria ambayo itaharakisha Makao Makuu yawe Dodoma na Ofisi ziweze kuhamia Dodoma, hatimaye Mji Mkuu wa Tanzania yetu uwe Dodoma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, labda niwakumbushe tu kwamba wenzetu Nigeria walibaini kwamba wanatamani wapate Mji Mkuu mpya mwaka 1976, wakajitahidi by mwaka 1991 wakaweza kufanikiwa kuhama kutoka Lagos kwenda Abuja. Sisi tangu mwaka 1973 mpaka leo mwaka 2016 bado hatujaweza kuhamia Dodoma. Kwa kweli hili jambo inabidi zichukuliwe hatua za uhakika kuhakikisha kwamba sheria hii inatugwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, uwepo wa sheria ya kutambua kwamba Dodoma ni Makao Makuu utasaidia sana kwa sababu kuna muingiliano mkubwa sana wa utendaji kati ya Manispaa pamoja na hii Mamlaka ya Makao Makuu. Kwa hiyo, naamini kwamba ukiwekwa mkazo wa uhakika kutungwa kwa hii sheria utasaidia kabisa kutofautisha kazi kati ya Manispaa pamoja na hii Mamlaka ya Ustawishaji wa Makao Makuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo ni kwamba uwepo wa sheria ile utasaidia kuharakisha kuwa na uwekezaji katika Mkoa wetu wa Dodoma. Kwa kweli katika Mkoa wa Dodoma, miaka ya nyuma kulikuwa na baadhi ya viwanda kwa mfano, Kiwanda cha Coca-cola lakini tunashangaa kiliondoka vipi, kulikuwa kuna Kiwanda cha Mvinyo bahati mbaya kikafa, kulikuwa kuna Kiwanda cha Magodoro, tunaona tu Magorodo Dodoma lakini magodoro yale hayatengenezwi hapa Dodoma.
Kwa hiyo, naamini kabisa kama ukiwekwa mkazo na naamini katika Bunge hili tutahakikisha sheria hii inatungwa basi uwekezaji utaweza kupata tija.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ili kupunguza mwingiliano wa kazi kati ya Manispaa pamoja na CDA, ikiwezekana kiundwe chombo kimoja tu ambacho kitasimamia ustawi na upimaji wa mipango miji katika Mkoa wa Dodoma kwa sababu Manispaa wanafanya shughuli hizohizo ambazo zinafanywa na CDA. Kama sheria itaweka chombo kimoja ambacho kitasaidia sasa kufanya mambo yote ya mipango miji, naamini kabisa itasaidia ustawishaji na hatimaye Makao Makuu yanaweza yakaja Dodoma lakini kubwa zaidi ni suala la sheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie pia suala la miundombinu. Katika Mkoa wetu wa Dodoma pamoja na kwamba mji umepangwa vizuri lakini kuna maeneo tofauti tofauti kwa mfano maeneo ya Area C, Nkuhungu, Medeli na maeneo mengine mapya ambayo yameanza kujengwa, zile barabara za ndani za mitaa hazipo, mvua zikinyesha kwa kweli kunakuwa na adha kubwa sana kwa wananchi. Kuna maeneo ambapo mashimo ni makubwa sana, kuna maeneo mifereji iliyopo sio mifereji ambayo inaweza ikasaidia kupitisha maji, kwa hiyo inaleta madhara makubwa sana. Kwa kuwa Waziri Mkuu yupo hapa na analisikia sheria hii ikitiliwa mkazo naamini kabisa mambo mengi yanaweza yakafanyika.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nataka kulisisitiza ni kuhusu sewage system katika huu Mkoa wa Dodoma. Kuna maeneo ni kweli imejengwa sewage system, lakini maeneo mapya ambayo Ustawishaji Makao Makuu wameyaweka sewage system bado sio nzuri. Kwa hiyo, tunaomba na jambo hilo lifikiriwe kwa ajili ya afya ya wananchi wa Mkoa wa Dodoma.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine nililokuwa nataka nilizungumzie ni kuhusu uwanja wetu wa ndege katika eneo la Msalato. Ninaamini kabisa kwamba uwanja huu uko katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi, lakini bado sijaona hatua za haraka au zinazoenyesha kwamba uwanja huu unaweza kujengwa haraka. Kwa sababu uwanja huu kwa kweli utakuwa una tija sana kwa wananchi wa Mkoa wa Dodoma lakini pia na wananchi wengine wote wa Tanzania kwa ujumla. Kwa hiyo, nimeona na hilo nalo nilizungumzie ili uwanja huo nao uweze kuangaliwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nataka kulizungumzia ni kwamba katika Mkoa wa Dodoma kuna eneo karibu kama kilometa nane kutoka pale Chuo cha Mipango bado halijawekwa lami. Kwa kweli imekuwa ni kero sana kwa wananchi na wamekuwa wakiilalamikia sana Serikali kwa kuona ukimya uliopo kwa sababu limekuwa la muda mrefu sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naamini kabisa katika bajeti hii nalo litatiliwa mkazo ili kusudi eneo lile liweze kuwekewa lami.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nataka kuzungumzia ni kuhusu suala la maafa na majanga na hasa kwenye janga la moto. Tumekuwa tukisikia matukio mbalimbali kuhusu janga la moto lakini bado nchi yetu haina vifaa vya kutosha kwa ajili ya kukabiliana na janga hili. Kwa hiyo, niombe Serikali waone ni utaratibu gani tunaoweza kuufanya walau wa kuweza kupata magari na vifaa vya uokozi wa moto katika kila Wilaya ili kusudi inapotokea dharura yoyote ya moto waweze kupata fursa ya kuweza kuzima huo moto kwa sababu wananchi wengi sana wamekuwa wakipata hasara.
Mheshimiwa Naibu Spika, mengi wameyazungumza wenzangu kuhusu masuala ya afya, maliasili na kadhalika lakini naomba tu nizungumzie kidogo kuhusu suala la Bima ya Afya au CHF. Wenzangu wamelizungumza na mimi naomba nitoe msisitizo, hebu Serikali ione kwa sababu hii asilimia 27 ya wachangiaji ni asilimia ndogo sana, bado tuna sababu ya msingi sana ya kuhamasisha wananchi ili kusudi waweze kujiunga na huu Mfuko wa CHF kwa sababu una tija sana kwao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni jambo la kushangaza sana Watanzania wenzangu hatuko makini sana kuchangia masuala mbalimbali ya kimaendeleo. Watu wako makini sana kuchangia harusi na sherehe mbalimbali, lakini kwenye suala afya inaonekana watu hawana mwamko. Nitoe shime kwamba na sisi viongozi tulifanyie kazi suala hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, ahsante sana.