Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

Hon. Hamidu Hassan Bobali

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Mchinga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

MHE. HAMIDU H. BOBALI: Mheshimiwa Spika, nianze kuchangia Wizara hii kwa kumpongeza kwa kuteuliwa kushika wadhifa wa Uwaziri katika Wizara hii. Pamoja na pongezi hizo, natambua kuwa majukumu yaliyopo katika Wizara hii ni makubwa mno kutokana na ukweli kwamba Wizara hii inagusa furaha za Watanzania wengi kupitia michezo.

Mheshimiwa Spika, kwanza nishauri kufanya marekebisho katika kanuni za ligi kuu ya Vodacom kwa kuondosha kanuni inayoipa timu iliyoshindwa uwanjani ushindi eti kwa kigezo cha timu shindani kumchezesha mchezaji mwenye kadi za njano tatu. Kanuni hii imepitwa
na wakati na nchi nyingi duniani wameiboresha kwa kubakisha point kwa timu iliyoshinda na ile timu ilivyotumia mchezaji mwenye kadi tatu za njano huadhibiwa kwa kutozwa faini na mchezaji husika kupigwa faini pia.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri jambo lingine ni lugha ya Kiswahili; lugha hii ni miongoni mwa urithi ambao tuliopo leo tumerithi na hatuna budi na sisi kurithisha kizazi kijacho. Lugha ya Kiswahili ni alama muhimu isiyo na shaka kabisa kuwa inalitangaza Taifa letu. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri kuandaa mipango madhubuti ya kukilinda na kukienzi Kiswahili kwani Serikali haijengi chuo maalum cha kufundisha Kiswahili pekee. Chuo hiki kitafanya kazi kubwa ya kukienzi Kiswahili kwa kufundisha masomo mahususi yanayohusu Kiswahili tu.

Mheshimiwa Spika, kwa nini Kiswahili kisitumike kama lugha ya kufundishia na kujifunzia kwa elimu ya sekondari na vyuo hapa nchini. Kitendo cha kuendelea kukitumia Kiingereza kama lugha ya kufundishia katika masomo ya elimu ya juu ni kuendelea kuwa watumwa wa kikoloni. Nashauri lugha ya Kiswahili iwe ndio lugha rasmi ya kufundishia na kujifunzia katika masomo ya elimu ya juu.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni kuhusu uozo uliopo TFF na Vyama vya Mpira vya Mikoa na Wilaya. TFF imetawaliwa na watu wanaosimamia maslahi yao binafsi badala ya mpira wa miguu. Kwa nini kila kukicha utasikia stori za magari ya Timu ya Taifa kuzuiwa hotelini au TRA. Hizi habari za TFF kudaiwa na TRA pamoja na hoteli ambazo timu zetu zinaweka kambi ni dalili za wazi kuwa TFF wana upungufu katika utendaji kazi wao. Mfumo wa usimba na uyanga uliokithiri pale TFF ni adui kwa maendeleo ya soka nchini.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni kutorushwa mubashara kwa matangazo ya Bunge. Jambo hili ni kinyume kabisa na katiba ya nchi yetu inayotoa haki ya Watanzania kupata taarifa na habari hususan za Bunge ambapo wawakilishi wao wanawasemea wao lakini kwa bahati
mbaya wananchi hawaoni jinsi wawakilishi wao wanavyofanya kazi walizowatuma.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri jambo lingine ni kuhusu Ciber Crime Act. Sheria hii imekuwa ikitekelezwa kwa wananchi ambao wana mlengo mmoja tu wa kisiasa (Wapinzani). Katika wingi wa vijana waliowahi kushtakiwa na kuhukumiwa wote ni aidha CHADEMA au CUF, kwa nini vijana wa CCM ambao kila kukicha wanaendelea kutoa maneno ya kejeli na matusi kwa viongozi wa upinzani lakini hakuna hata mtu mmoja aliyewahi kukamatwa na kufikishwa mahakamani. Tunaomba Serikali iache kutekeleza usimamizi wa sheria ya mtandao kwa ubaguzi wa itikadi za kisiasa.