Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Kavuu
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi ili na mimi niweze kuchangia hoja ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Kwanza, napenda niwashukuru wananchi wangu wa Jimbo la Kavuu, kwa kuniamini na mimi nawaambia sitawaangusha tuko pamoja.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze na hotuba ya Waziri Mkuu ukurasa wa 15, uwezeshaji wananchi kiuchumi. Katika hili, napenda kwanza niishukuru Serikali yangu kwa kuweza kuanzisha VICOBA na SACCOS ambazo zimekuwa na mchango mkubwa katika kuinua pato la wananchi. Pia napenda nishukuru Chama changu cha Mapinduzi katika Ilani yake ilipokuwa inajinadi kuanzisha mfuko wa shilingi milioni 50 katika kila kijiji. Katika hela hizi kutokana na namna tulivyokuwa tunajinadi, basi ziende zikatumike hivyo, kwa makundi mbalimbali ndani ya kila kijiji ambavyo vitakuwa vimesajiliwa na Halmashauri na kutambuliwa kisheria. Kwa sababu tunaelewa katika makundi ya vijana na akina mama tuna asilimia 10 ya kila mapato ya Halmashauri. Kwa Halmashauri ambazo hazifanyi hivyo basi Serikali isimamie.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende ukurasa wa 25 kuhusu Hifadhi ya Mifuko ya Jamii. Mifuko hii imekuwa na michango mikubwa katika shughuli za maendeleo katika kuendeleza Taifa letu kiuchumi. Niwaombe na niiombe Serikali, kwa sababu tumekuwa tunawahimiza wananchi wajiunge na Mifuko ya Bima ya Afya na kwa sababu hii Mifuko ya Bima ya Afya inachangia katika maendeleo ikajenge zahanati kwenye vijiji, ikatusaidie hata kupata vifaa tiba katika zahanati zetu na vituo vya afya. Kwa nini natamka hivyo? Hii itatusaidia kujenga imani kati ya wananchi na hii mifuko na hivyo itakuwa rahisi kwa wananchi kujiunga na mifuko hii kwa sababu wataona wananufaika, wataona faida yake na watajiunga kwa urahisi. Kwa hiyo, niwaombe NHIF watusaidie kuwekeza katika zahanati zetu na vituo vya afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niongelee suala la mifugo hususani suala la migogoro, nafikiri Serikali imepokea malalamiko mbalimbali kutoka katika kila Jimbo kuhusiana na migogoro ya ardhi. Naongelea katika Jimbo langu kuhusiana na migogoro inayojitokeza kati ya wafugaji na mipaka ya Hifadhi ya Taifa hususani Hifadhi ya Katavi. Migogoro imekuwa ikiwasilishwa mara kwa mara. Serikali hii nafahamu ni makini kweli kweli na inafanya kazi kweli kweli na Mbunge mwenyewe Kikwembe anafanya kazi kweli kweli, kutokana na namna tulivyojipangia kutatua hii migogoro, niombe sasa baada ya Bunge hili, baada ya Bajeti, Serikali ikaanze kutatua migogoro kati ya wakulima na wafugaji, kati ya wananchi wanaoishi mipakani na Hifadhi za Taifa, tuondokane na kero hii ili tuweze kufanya shughuli za maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini naomba niongelee suala la uwekezaji kwa wananchi. Tunakuwa na uwekezaji mzuri ambao unalenga kukuza pato la mwananchi. Napenda niongelee uwekezaji katika masuala la mawasiliano. Mawasiliano ni kitu cha msingi sana, napenda niishukuru Serikali yangu kutoka awamu iliyopita mpaka hii tuliyonayo kwa kuwezesha mawasiliano vijijini kupitia mtandao wa Halotel, Mkoa wa Katavi sasa hivi tuna 100% ya mawasiliano. Ninachopenda kusema tumekuwa na migogoro kati ya wawekezaji hasa wanapokwenda kuweka minara. Nafahamu Halotel imekuja kutatua tatizo ambalo makampuni mengine yalishindwa kwa sababu yanajiendesha kibiashara zaidi lakini Halotel wamefanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe Serikali kupunguza matatizo ambayo yanajitokeza hivi sasa kati ya wawekezaji hawa wa Halotel na wananchi katika maeneo husika, waweze kuangalia namna watakavyoweza kutoa zile tozo. Siamini kabisa kwamba hawa Halotel wanatoa huduma bure na sisi tunalipia hizo huduma.
Kwa hiyo, huu mpango wa kusema shilingi 30,000 kwa mwezi katika eneo husika, kwa kweli bado si sahihi, naomba Serikali waliangalie hilo. Pamoja na kwamba wametusaidia kiasi cha kutosha na nawapongeza sana Serikali kwa kuwaleta hawa Wavietnam ambao wamekuwa mkombozi katika mawasiliano vijijini lakini naomba tuangalie upya hizo tozo kuondoa migongano kati yao na wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niongelee upande wa barabara. Naishukuru Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi, Bunge lililopita Mheshimiwa Rais alikuwa Waziri wa Ujenzi. Amejitahidi kwa kadiri ya uwezo wake, tumepata pesa ya kutengeneza barabara kwa kiwango cha lami kutoka Mpanda – Tabora. Wananchi wa Katavi, Tabora na Kigoma kwa ujumla tunasema ahsante.
Kama ilivyokuwa kwenye mipango ya Serikali iliyopita ya kutengeneza barabara ya lami kutoka Majimoto - Inyonga naomba iwemo ndani ya bajeti kwani sijaiona na Daraja la Kavuu sijaliona na liko kwenye mpango. Kwa hiyo, niombe sana wazingatie kuweka kwenye bajeti hii mipango iliyokuwepo kipindi kilichopita. Si kwa Jimbo la Kavuu tu ambalo ni jipya, niombe katika Majimbo yote mapya, tuwekeeni hata barabara za vumbi ambazo zinapitika kwa kuanzia si haba tofauti na ambavyo hatuna barabara kabisa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie suala la reli. Lengo la Serikali ni kutandika reli mpya na nzito zaidi kwa kiwango cha standard gauge. Huu wimbo umekuwa ni wa muda mrefu si chini ya miaka saba iliyopita. Kwa sababu Serikali yetu ni ya hapa kazi tu tunachohitaji ni vitendo. Let us put our ideas into action. Tumechoka na huu wimbo kwenye reli ya kati, tunataka tuone reli ya kati inatengenezwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niongelee suala la maji. Tarehe 20 Aprili nilipata majibu mazuri kutoka Serikalini kwamba kuna pesa imetengwa kwenye kata zangu kwa ajili ya suala hili. Hizo pesa ni za bajeti iliyopita, bajeti itaisha tarehe 30 Juni, niombe pesa hizo zitoke kabla ya bajeti mpya ili tuanze shughuli za kujipatia maji safi na salama.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende ukurasa wa 47, aya ya mwisho inaongelea umeme Gridi ya Taifa. Mkoa wa Katavi ulikuwa kwenye mpango wa kupita Gridi ya Taifa kutoka Biharamulo sijaona kwenye mpango huu. Kwa vile kwenye bajeti iliyopita tulitenga naomba iendelee kuwepo na itekelezwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwenye bajeti iliyopita kulikuwa na suala la generator mbili zilizokuwa zinatoka Belgium kwenye bajeti iliyopita hazijafika Katavi mpaka leo na hivyo kuifanya Mpanda na Katavi kwa ujumla kutokuwa na umeme wa uhakika, na kushusha mapato ya Mkoa. Kwa hiyo, tunaomba kabisa hilo suala la generator hizo mbili nalo lipatiwe majibu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naishukuru Serikali yangu katika sekta ya elimu kwa kubana matumizi katika shughuli za Bunge lakini isibane tu katika shughuli za Bunge ibane hata kwenye baadhi ya vifungu ambavyo vinasemekana viko kisheria kwenye mafungu ya bajeti mtayaona, kwenye masuala ya simu, magazeti, nyumba, umeme, haitavumilika, haiwezekani milioni nane, milioni 10, milioni 20 zinakwenda kule zirudishwe. Wote tunafunga mikanda, hakuna atakayesema nalipiwa simu kisheria, tunafunga mikanda. Kwa hiyo, wote tufunge mikanda tuiweke pesa kwenye maendeleo ya maji, tupeleke elimu, tupeleke kwenye barabara na tupeleke afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niongelee suala la Ustawishwaji Makao Makuu Dodoma. Hili suala limekuwa ni tatizo kwa wananchi wote wanaokaa Dodoma, ni shida, ni taabu, ni kero isiyokuwa na majibu.
Mheshimiwa Naibu Spika, CDA wana mambo yao, Manispaa wana mambo yao, mwananchi unalipa kodi zaidi ya mara mbili, kunakuwa na mgongano wa kazi kati ya Manispaa na CDA. CDA wanapandisha kodi, una kiwanja ulikuwa unalipa shilingi 97,000 leo unalipia ile kodi mara nne yake, si sahihi. Lazima iletwe sheria kwa niaba ya wananchi wa Tanzania tuweze kujadili hili suala. (Makofi)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa muda wako umekwisha.
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru na naunga mkono hoja.