Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Hassanali Mohamedali Ibrahim

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kiembesamaki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. IBRAHIM HASSANALI RAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi. Kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunifikisha hapa leo Bungeni nikiwa mzima wa afya. Vilevile nichukue nafasi hii kutoa mkono wangu wa pole wa rambirambi kwa wazee ambao walifiwa na watoto wao juzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya kuelezea changamoto yangu katika Wizara hii Mambo ya Ndani ya Nchi, kwanza nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri anayofanya kuweka nchi hii katika hali ya utulivu na amani. Tukienda kwenye changamoto katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi nitazungumzia upande wa Zanzibar. Kwa kweli Vituo vingi vya Polisi Zanzibar vipo katika hali mbaya sana vimekuwa kama magofu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unaweza kwenda Kituo cha Polisi ukastaajabu kwa sababu vitendea kazi kwanza hamna, Polisi wanafanya kazi katika mazingira magumu sana, jengo limechaa, mapolisi wengi Zanzibar hawana radio call za kuwasiliana na viongozi wao na hawana magari. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri aiangalie Zanzibar kwa jicho la huruma kwa sababu mapolisi wanafanya kazi katika mazingira magumu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija kwa upande wa trafiki, kwanza nichukue fursa hii nimpongeze kaka yangu Kamanda Mohamed Mpinga na timu yake nzuri kwa kazi wanayofanya kwa kweli wametusaidia sana katika Jiji letu la Dar es Salaam, sasa hivi madereva wanafuata sheria na nidhamu imekuwepo lakini bado kuna matatizo mengi sana hasa katika suala la kupaki magari sehemu ambapo hairuhusiwi. Kwa hiyo, namwomba kaka yangu Mohamed Mpinga suala hili alitilie mkazo zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuna suala hili la mapolisi wanapotaka kwenda likizo wanaambiwa waende halafu wakirudi ndiyo watapewa haki zao kwa maana ya posho zao. Mimi namuuliza Mheshimiwa Waziri wakati polisi anapokwenda likizo unamwambiaje aende likizo halafu akirudi ndiyo apewe marupurupu yake, inakuwa si haki. Polisi anapopangiwa kwenda nyumbani basi apewe haki zake zote aende akastarehe na mama watoto na watoto wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili kwa kweli linawavunja nguvu Jeshi la Polisi kwa sababu wanafanya kazi katika mazingira magumu sana. Naomba Wizara hii walitupie macho Jeshi la Polisi kwa sababu wanafanya kazi katika mazingira magumu sana na wanastahiki posho muda ukifika na kama kuna uwezekano posho zao ziongezwe kwa sababu wao ndio wanatulinda sisi na mali zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti,tukiwavunja nguvu Jeshi la Polisi hakuna litakaloendelea katika nchi yetu hii. Kwa hiyo, namwomba sana Mheshimiwa Waziri aliangalie Jeshi la Polisi kwa macho ya huruma kwa sababu wanafanya kazi ngumu na ya hatari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia hawa maafande wetu wanapokwenda kwenye kazi maalum (task force) nashauri wapewe vifaa ambavyo vitawasaidia hususan mapolisi. Dar es Salaam kuna mapolisi ambao tunawaita Polisi Tigo kwa kweli zile uniform wanazovaa akitokea mtu yeyote mwenye nia mbaya na kuwapiga risasi basi inapenya tu kwa sababu hazistahili kutokana na kazi yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda katika upande wa Uhamiaji, niwapongeze kwa kazi nzuri wanayofanya, lakini naomba wazingatie suala la wakimbizi. Kuna hawa wakimbizi wanaotoka nchi jirani wanakuja nchini kwetu na kutuharibia amani yetu, kwa sababu wakija nchini kwetu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. IBRAHIM HASSANALI RAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naunga mkono hoja ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.