Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. FAIDA MOHAMED BAKAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza, naomba kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutufikisha leo tukiwa katika hali ya afya njema. Pia napenda kutoa pole kwa wazazi wenzetu ambao wamepoteza watoto wao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naenda moja kwa moja kwenye makazi ya askari na vituo vya askari. Kama tunavyojua askari siyo vizuri kukaa uraiani kwa sababu askari hawa wana namna yao ya kuishi, wana siri zao na mambo yao ya kitaalam na ya kimaadili yao, siyo vizuri kuchanganyika yaani nyumba hiyo hiyo askari nyumba hiyo hiyo raia. Wao wanatakiwa watulinde sisi, wanatakiwa wawe na maeneo yao ya kuishi, lakini hawana nyumba. Kila nikisimama naongea kuhusu nyumba za askari hasa kule kwetu Pemba, hakuna nyumba za askari, wengi wanakaa uraiani na ni maili nyingi kutoka wanakokaa na kazini. Wanachelewa kufika kazini kutokana na usafiri, si vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri amekuja Pemba, Mheshimiwa Naibu Waziri amekuja Pemba, Pemba wanaijua, naomba nisiseme tena, naomba askari wajengewe nyumba na vituo vyao ni vibovu. Kituo cha Mkoani, Kengeja, Konde kote vituo ni vibovu vinavuja, mvua hizi zote zimo ndani kwenye vituo vile. Hivyo kweli jamani hatuwaonei huruma askari wetu, kwa nini tunawafanyia hivi askari? Naomba sana nisiseme tena kuhusu suala hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee hali ya amani na utulivu. Tunawashukuru sana wananchi wa Tanzania na Serikali yetu hasa kwetu Pemba kwa sababu zamani hatukuwa tunaishi vile, vyama vyote tulikuwa na matatizo kusema ule ukweli, huyu anampiga huyu, huyu anamuua huyu, huyu hamziki huyu, huyu haendi dukani kununua kwa huyu, lakini sasa hivi hali ya amani Pemba imetulia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunawashukuru sana wananchi wa Pemba na kwa kweli tujitahidi kuzidisha ushirikiano wetu ili tuweze kuishi kwa amani na utulivu katika Kisiwa chetu cha Pemba. Siasa tuiweke nyuma ili tuweze kuleta amani na utulivu na watoto wetu waishi vizuri katika Kisiwa chetu cha Pemba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee ajira za vijana katika Kisiwa changu cha Pemba. Kule Pemba kuna vijana wazuri tena wasomi, unajua wasomi wazuri wanatoka Pemba, nyie mnajua hilo? (Makofi)
Wasomo wazuri wanatoka Pemba, vijana ni wasomi, wana maadili na ni wachapa kazi, lakini wakati wa ajira vijana wa Pemba wanaachwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja.