Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kiteto
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. EMMANUEL P. JOHN: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwanza nianze kwa kushukuru na kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba nzuri ambayo imejaa mambo mengi ambapo yote yanakidhi matarajio ya Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na suala la kilimo. Wizara ya Kilimo nilidhani ingeweza kutusaidia kwa maana kwamba Benki ya Kilimo ingeweza kubeba zile pesa ambazo ziko TIB ili kuongezea mtaji ambao ni ile shilingi bilioni 60 inayotajwa kwenye hotuba ya Waziri Mkuu. Fedha nyingine nilizotaka ziweze kuhama ni zile za Mfuko wa Pembejeo wa Kilimo ambazo ziko Exim Bank. Zile pesa kama zingehama zingeweza kuongezea capital kwenye ile bilioni 60 ili wananchi waweze kukopa kwa urahisi kwa sababu itakapokuwa fedha zote ziko mahali pamoja itatusaidia kuweza kukopa na wananchi wetu wengi ambao ni asilimia 80 wako vijijini wangeweza kukopa pesa hizo, hilo ni jambo la kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili NFRA wamesema watanunua tani laki moja. Tani laki moja ni kiasi kidogo cha chakula, naomba Serikali iweze kununua chakula karibu tani laki mbili ili itakapotokea shortage tuweze kukabiliana na uhaba wa chakula. Hata hivyo, tutakapokuwa na excess wana uwezo wa kuuza nje kwa maana kwamba kurudisha pesa ili waweze kwenda kwenye season nyingine ya ununuzi wa chakula.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pembejeo za kilimo. Hebu tuangalie ni njia ipi ambayo inaweza kutusaidia. Kwenye kilimo ningeshauri tuangalie ni namna gani ya kuweza kuzalisha mbegu zetu wenyewe kuliko importation ya mbegu ambapo tunatumia foreign currency kuziingiza hapa nchini, ni gharama kubwa. Pia Serikali iangalie ni namna gani ya ku-invest kwenye kilimo cha mbegu ili tuweze kuzalisha mbegu wenyewe nchini na kupunguza hali ya kutegemea mbegu za nje ambazo mara nyingine ni hatarishi kwa maana ya kilimo chetu hapa nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni dawa za ruzuku za mifugo. Ukiangalia dawa za ruzuku za kuogesha mifugo hapa nchini zinasumbua, haziui isipokuwa kwenye ile zero grazing (ng’ombe wale wa majumbani) lakini ukienda kwenye wale ambao wanafuga nje mifugo mingi kupe hawafi. Nashauri na kuiomba Serikali iangalie importation ya dawa hizi au wale watengenezaji basi waangalie mara mbili kwa sababu kupe hawafi, ng’ombe wanazidi kuumwa na hii inachangia sana kusababisha mifugo yetu kutokuwa na afya na mwisho wa siku tunakuwa na mifugo ambayo haiko kwenye kiwango kwa sababu ya dawa ambazo hazikidhi kiwango cha kuweza kutibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuomba ujenzi wa Kiwanda cha Nyama pale Ruvu. Naomba Serikali ijikite kuangalia namna gani ya kujenga Kiwanda cha Nyama ili mifugo yote inayoweza kuingia Pugu iishie pale Ruvu ikachakatwa, nyama zikaingia kwenye supermarkets na masoko yetu tukawa na nyama bora. Hii itasaidia kuwa na nyama ambazo zimepimwa na ziko kwenye viwango. Pia tutaweza kujua ni mifugo kiasi gani tumechinja lakini hata ili revenue yetu haiwezi kupotea kuliko kwenda kushindana pale Pugu. Hilo ni jambo ambalo ningeomba Serikali ijikite kulishughulikia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine naomba soko la mazao Kiteto, sisi tunazalisha mazao mengi sana. Ukiangalia central zone nzima inategemea mazao ya Kiteto, Dar es Salaam inategemea Kiteto, Tandale nzima inategemea Kiteto kwa asilimia karibu 50 lakini hatuna soko.
Naomba Serikali ilione hili itujengee soko ndani ya Wilaya yetu hata kama kuna soko la Kibaigwa lakini tuwe na soko letu la ndani. Mheshimiwa Waziri wa Viwanda alione hili, tuwe na soko letu la ndani tuweze kuwa na internal collection yetu, tuweze kuona ni namna gani na sisi tunaweza kuvuka huko mbele tunakokwenda ili tuweze kupata namna gani ya kuweza kuingiza mapato lakini na watu wetu waweze kufaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiachana na hilo, lile soko pamoja na NFRA kwa mfano inanunua mazao Kiteto zaidi ya tani labda 10,000 au 15,000 ile transportation cost ya kuja NFRA tungependa wapewe wananchi wetu wenye magari wasafirishe kile chakula kuliko kumpa zabuni mtu akasafirisha kile chakula na wananchi wakabaki pale. Ni mojawapo ya creation employment kwa vijana wetu. Watu wetu waweze kufaidi hata hii asilimia ndogo ya kusafirisha hicho chakula kwa sababu na wao magari wanayo. Hii inaweza kusaidia kwa sababu tenderer anaweza kusafirisha kwa gharama kubwa wakati wale wananchi wanaweza kusafirisha kwa gharama ndogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu shilingi milioni 50 kila kijiji, plan yake vyovyote vile itakavyokuwa kwa Kiteto tumejitahidi kufungua VICOBA, SACCOS na vikundi mbalimbali lakini ningeomba nitengeneze commitment. Hebu twende tuangalie kwenye maeneo hizi pesa zikienda, je, kwa mfano Kiteto tunaweza kutengeneza commitment yetu ya kutumia pesa hizi, tukazalisha, zikazunguka kwa wananchi, tukazisimamia wenyewe, kukaja returns kwa kufikiria muundo wetu wa namna gani ziweze kuzunguka zikafikia watu. Maana tukienda kwa maana kwamba kuna watu wale ambao watakuwa ni wajasiriamali ndiyo wapate hizo pesa then wale ambao siyo wajasiriamali katika ile routine ya mzunguko wa zile pesa wao watakuwa wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri sisi Wilaya ya Kiteto tulete plan yetu mkiona inafaa basi tu-guarantee, tu-sign contract, mtupe hizo pesa tuzizungushe kwa maana ya wananchi wetu katika zile SACCOS and then tuzalishe ile riba na bado tuoneshe ile flow ya matumizi ya zile pesa na jinsi ambavyo zinavyoweza kurudi Serikalini ili ziwasaidie wengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hiyo trend ni kwamba tutakapokuwa tumeweza kuwapa watu wengine wale wazee ambao hawawezi kupata hizo pesa basi watakwenda kwenye ile role ya TASAF. Ile asilimia 10 ya vijana na wanawake ambayo itakusanywa kutokana na ile collection ya Halmashauri basi itasaidia vijana. Lengo letu ni ku-make sure kwamba tunaweza ku-monitor wenyewe, tukajua ni watu gani wanaweza kupata pesa hizo na nani hana, nani anastahili na nini kifanyike ili mradi ile community nzima iweze ku-benefit kutokana na hiyo collection na zile generation ya income ambazo tutakuwa tumezipata.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba nizungumzie kuhusu mapato. Tumekubaliana ndani ya Serikali zile electronic machines zitatumika kukusanya mapato. Kuliko sasa hivi kwenda kwenye ku-tender, sijui tenderer amepata pesa, nashauri kwamba Watendaji wa Vijiji, Watendaji wa Halmashauri wasimamie kwa kutumia electronic machines tukusanye mapato wenyewe. Hii ni creation of employment, tujue tumepata nini, Halmashauri zetu zinaweza kukusanya zaidi kuliko tenderer ambaye anaweza ku-benefit zaidi kuliko Halmashauri zetu ambazo zingeweza kusimamia zenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kuna barabara ambayo inatoka NARCO hapa njiapanda kwenda Kiteto. Hii barabara wakulima wengi wanaitumia, tunaomba Serikali ituone. Ni ahadi ya Serikali tangu mwaka juzi, Mheshimiwa Jakaya Kikwete alituahidi kwamba angeweza kuitengeneza barabara hii. Tunaomba Serikali ya awamu hii kupitia mpango wake wa fedha hebu tuoneeni huruma, hii barabara haina shida kabisa, ina madaraja mawili tu au matatu. Mheshimiwa Waziri Mkuu uko hapa, tuokoe kidogo angalau na sisi tupitishe mazao yakafikie walaji kwa gharama nafuu lakini na mkulima aweze ku-benefit kale ka-profit kwa sababu transportation cost zitashuka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna barabara ya Handeni – Kilindi – Kiteto – Chemba – Singida. Barabara hii inafungua mikoa mitano, inafungua Tanga, Manyara, Dodoma na Singida. Ile pipeline ya mafuta wanayosema ya kutoka Uganda itapita pale. Hebu Serikali tuoneni huruma, tunaomba hii barabara muiweke kwenye mpango. Barabara hii itakapofungua mikoa hii itapunguza hata msongamano wa hii barabara ya Dar es Salaam ili watu wengine wapitie kule lakini tutakuwa tumefungua mikoa kwa maana ya programu ya kufungua mikoa yote kwa barabara za lami na watu wote waweze kupita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu CDA naomba Serikali ijaribu kuona ni namna gani inaweza kutengeneza plan ya EPZ zone kubwa hapa Dodoma ili vitu vingi na investors wengi waje Dodoma wakuze mji wetu na ivutie watu ili tupunguze msongamano Dar es Salaam. Hilo la msongamano linaweza kuhamia Dodoma, tukaweka kijiji kingine ambacho ni business city center ndani ya mji wetu wa Dodoma na ikapanua mji na kuongeza ajira na watu wakaongezeka Dodoma na sisi tukaendelea ku-benefit. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, muda wangu ni mchache naona umekwisha, naomba kuishukuru Serikali. Nimpongeze Rais Magufuli kwa kazi anayoichapa, wote tumuunge mkono. Tulimuomba Mungu atupe Rais ambaye anatufaa Watanzania kwa sasa. Hebu tumuunge mkono, tukubaliane naye, maamuzi anayoyafanya tumuunge mkono, tusibaguane kwa itikadi za vyama, tuhakikishe kwamba tunamuunga mkono, tumpe full support ili aweze kulisukuma gurudumu la maendeleo ya Watanzania kule tunakotakiwa kwenda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tumuunge mkono Mheshimiwa Waziri Mkuu, anachapa kazi, yuko makini, hana mjadala, kazi lazima iende, tusiwakatishe tamaa viongozi wetu. Tunawaunga mkono Mawaziri wetu, chapa kazi tuko nyuma yenu, fungulieni speed zote, fanana kama gari linaloshuka mlima halina break tusonge mbele, huko tutakakoishia Watanzania wote tutakuwa tumekubaliana kwamba lazima maendeleo yapatikane. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba kuwasilisha na naunga mkono hoja, ahsante sana.