Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Capt. (Mst). George Huruma Mkuchika

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Newala Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE.KAPT.MST. GEORGE H. MKUCHIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwakunipa nafasi, nitangulie kusema kwamba, naunga mkono hoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kupongeza sana kazi nzuri inayofanywa na majeshi yetu. Kazi nzuri inayofanywa na askari waliopo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, bila wao hapa Tanzania pasingekalika, wanafanya kazi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe pole kwa ndugu zangu wa Rufiji, Kibiti, wajukuu zangu kwa mikasa wanayopata, wanauawa bila sababu, lakini kama mlivyosikia Jeshi la Polisi liko pamoja na ninyi jambo hili la muda litazimwa na majeshi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nitoe pole kwandugu wanaohusika na msiba wa jana kule Arusha, niseme jambo moja, mchangiaji mwenzetu mmoja hapa asubuhi alisema kwamba itakuwa vizuri kama kila Mbunge akaonja jela, ili kuweza kujua mambo ya kule ndani. Nataka nimjibu kwamba Wabunge wa Tanzania ni waadilifu sana, tunajitahidi kila tunavyoweza ili tusiende jela na kwa sababu tulimpata mtu kaenda jela katusimulia, imetosha. (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nijikite katika Jeshi la Zimamoto. Kwamba, Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Jeshi la Zimamoto kama Jeshi bado ni change, ilikuwa ni Idara chini ya Jeshi la Polisi lakini baada ya kufanywa kuwa Jeshi la Zimamoto na Ukoaji, Wizara mnatakiwa mlilee Jeshi la Zimamoto. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninasema hivi kwa sababu gani mimi ni Mjumbe ya Kamati ya Ulinzi na Usalama. Nilipotembea Majeshi ya Zimamoto tumegundua matatizo mengi. Kwa mfano, iko Tume ya Majeshi inayopandisha vyeo, kuajiri ni Tume ya Majeshi, Magereza wamo, Polisi wamo, bado hamjawaweka Zimamoto. Sasa kama hawamo kwenye Tume watapandaje vyeo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, kule Zimamoto ukimwondoa Thobias Andengenya ambaye ni Kamishna Jenerali wanaomsaidia wote acting,hizo bado tangu lilipoanza Jeshi pale mpaka leo wana act? Hii inawezekana kwa sababu Tume ya kuwapandisha haipo. Natoa kutoa rai watu wale hatua ichukuliwe haraka, tuwe na Makamishna siyo acting. (Makofi)

Suala lingine kuonesha kwamba sisi Wajumbe tuna mashaka kwamba pengine Waziri jicho haliangalii sana Jeshi hilo, asubuhi umetueleza hapa majengo mapya ya Polisi, Uhamiaji, Magereza, tukawa tunasubiri Zimamoto kimya, hata hela kumalizia Zimamoto ambayo tayari wameanza kujenga kule Dar es Salaam, kimya! Niishie hapo.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili nizungumzie juu ya magereza. Leo bajeti ya magereza ni kubwa kwa sababu Magereza hawajitoshelezi kwa chakula. Tumetembelea kambi za magereza nyingi tu. Tumekwenda Songwe tumeona ardhi nzuri, eneo nzuri la kulima, walituambia tunaomba Waheshimiwa Wabunge iambieni Serikali itupe matrekta, itupe vifaa vya kilimo, tuna uwezo wa kulima na kugawa chakula kwa magereza mengine, badala ya kuomba hapa Mheshimiwa Waziri hela ya magereza ya chakula omba matrekta wale watu wako tayari kujilisha wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu ni maeneo ya utawala. Leo Wilaya mpya zote zina matatizo ya kiutawala, kwa sababu hawana magereza hawana vituo vya polisi, hawana mahakama. Kwa hiyo, kuna kazi kubwa sana inafanywa na magereza kubeba askari kutoka Wilaya mpya kuwapeleka Wilaya mama watuhumiwa kwenda kusikiliza kesi, gharama ile ya mafuta ni kubwa. Ushauri wangu ni kwamba maeneo mapya ya utawala yanapoanza izingatiwe kwanza magereza, kituo cha polisi, mahakama ni sehemu ya utawala. Mkuu wa Wilaya hawezi kukamilika kama hana kituo cha polisi, kama hana magereza, kama hana mahakama…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE.KAPT. MST. GEORGE H. MKUCHIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nilidhani dakika zangu ni kumi kumbe tano. Naunga mkono hoja kwa kuombatu kwamba Uhamiaji wajenge kituo cha uhamiaji kule Newala na mmalizie kituo cha polisi ambacho mnasema kimefika asilimia 85.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.