Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Mary Pius Chatanda

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Korogwe Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nianze kwa kuunga mkono jitihada za Mheshimiwa Rais wa Jahmuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Waziri Mkuu na Mawaziri kwa kazi nzuri ambayo wamekuwa wakiifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wameshuhudia juhudi zao katika kutekeleza dhamira ya uwajibikaji na maadili kwa viongozi, watendaji na watumishi wasiyo waadilifu kwa kuwatumbua majipu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ikishafika sasa hivi saa moja kwenye taarifa ya habari, ikifika saa mbili kwenye taarifa ya habari wananchi wanakimbia kwenda kusikiliza leo kunatokea kitu gani. Wananchi walikuwa wameshachoka na tabia ya baadhi ya watendaji wa Serikali ambayo walikuwa wakiifanya, kwa hiyo, sasa wanafurahia juhudi ya Serikali ambayo inafanya ya kuhakikisha kwamba hakuna matabaka kati ya walio nacho na wasiyo nacho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nianze kwa kunukuu maneno aliyosema Kitilya Mkumbo kwenye mtandao wa twitter amesema; “Tunahitaji upinzani utakaojikita katika sera mbadala. Upinzani unaotegemea makosa ya Serikali ya CCM pekee unaweza kupwaya sana katika kipindi hiki.” Mwisho wa kunukuu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona ninukuu hili la Mkumbo kutokana na kitendo cha Kiongozi wa Kambi ya Upinzani kutowasilisha hotuba ya bajeti ya Kambi ya Upinzani na hasa ukiangalia bajeti yetu sisi ya Waziri Mkuu ina karatasi kama 100 kitu hivi lakini ya mwenzetu huyu amekuja na karatasi tatu. Matokeo yake kwa sababu kashindwa kuiandika bajeti anashawishi wenzake watoke nje. Hoja ya Kitilya Mkumbo iko sahihi kabisa hawa watu wamefilisika na wamepwaya kisiasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nichukue nafasi hii kuishukuru Serikali ya Tanzania kwa kupata mradi mkubwa wa bomba la mafuta kutoka Uganda kuja Tanzania hususani Mkoa wa Tanga. Ni matarajio yangu kwamba fursa hii ambayo tumeipata tutaisimamia vizuri na kuweza kuanza kufanya maandalizi ya maeneo ambayo mradi huu utapita kwa kutoa elimu kwa wananchi wa maeneo yale na hatimaye kuanza kufanya maandalizi ya fidia kwa maeneo yale yatakayokuwa yamepitiwa na mradi kama kwenye mashamba na nyumba ili kuondoa usumbufu katika utekelezaji wa mradi huu. Ni matarajio yangu kwamba watatoa elimu kwa wananchi ili waweze kutambua faida ya mradi huu ambao umepatikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikubaliane kabisa na kaulimbiu kwamba Tanzania kuwa ya viwanda inawezekana. Ili kufanikisha jambo hili ni vizuri tukaimarisha suala la kilimo. Tukiimarisha kilimo vizuri tukakipa kipaumbele kitaweza kuzalisha malighafi ambazo ndizo zitakazoweza kulisha hivyo viwanda.
Tusiposimamia vizuri kuhakikisha kwamba kilimo tunakipa kipaumbele tunaweza tukajenga viwanda na hatimaye tukakosa malighafi, viwanda vikawa vipo na havifanyi kazi na ile kauli mbiu ya kwamba Tanzania iwe ya viwanda ikawa ni kazi bure. Hivyo, naishauri Serikali tusimamie na tuhakikishe kwamba kilimo kinapewa kipaumbele, kiende sambamba na upatikanaji wa maji. Kama maji hayapo kiwanda hakiwezi kufanya kazi, kama hakuna umeme wa uhakika kiwanda hakiwezi kufanya kazi, kama miundombinu hakuna, kiwanda kinaweza kikafanya kazi lakini usafirishaji wa hayo mazao itakuwa ni shida. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, miundombinu ni pamoja na reli. Tunapozungumzia reli kama ambavyo wezangu wengine wametangulia kuzungumza reli ni kitu muhimu sana. Reli inapunguza uharibifu wa barabara, magari makubwa yanapita yanaharibu barabara kila siku inafanyiwa matengenezo. Reli ikitengenezwa nadhani mizigo yote itapita kwenye reli na viwanda vyetu vitakapokuwa vimezalisha mazao yatapitishwa kwenye reli, hivyo angalau shughuli za uzalishaji na mali kupeleka kwenye mikoa kupitia reli. Napozungumzia reli basi naomba ifahamike kwamba ni pamoja na reli ile ya kutoka Tanga - Kilimanjaro - Arusha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nizungumzie suala zima la Mfuko wa PSPF. Huu Mfuko wa PSPF unachelewesha mno mafao ya watumishi waliostaafu. Niiombe Serikali, watumishi hawa ambao wanakuwa wamestaafu hizi fedha zao ndizo zinazowasaidia kuweka maisha yao vizuri. Inapokuwa wanacheleweshewa kupata mafao yao inakuwa ni shida. Kwanza, inawapa ugumu wa maisha kwa sababu ameshajipanga kwamba amestaafu kuna hizo fedha anategemea kufanya shughuli ambazo zitamwezesha kupata kipato, lakini anacheleweshewa kupata fedha hizi. Niombe Serikali, hawa wastaafu wanapostaafu basi iwe ni muhimu sana kuwaandalia mafao yao mapema ili waweze kutoka wakiwa na fedha zao na hatimaye waweze kuishi muda mrefu kuliko ilivyo hivi sasa. (Makofi)
Mheshimwa Mwenyekiti, suala la walimu. Lipo tatizo kwa walimu kuhusiana na upandishwaji wa madaraja. Walimu wamekuwa wanachukua muda mrefu kwenye kupandishwa madaraja na hata wakipandishwa mishahara yao kwa maana ya stahiki zao zile zinachelewa sana kufanyiwa marekebisho, inachukua hata miezi sita mtu hajarekebishiwa. Niombe wanapopandishwa madaraja basi na zile stahiki zao ziwe zimeandaliwa. Kule Korogwe wapo baadhi ya walimu wanadai malimbikizo toka 2010 hadi hivi sasa hawajalipwa na wamepandishwa madaraja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali iangalie upya suala la posho ya kufundishia (teaching allowance) kwa walimu. Tuseme tusemavyo walimu wana jukumu kubwa sana, wanafanya kazi kuliko mfanyakazi mwingine yeyote.
Tukirudisha teaching allowance kwa walimu haki ya Mungu hii elimu itakwenda vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe Serikali hebu tulitazame jambo hili. Walimu hawa wamekuwa wakitoka shuleni wakifika nyumbani ni kazi ya kuanza kufanya maandalizi, kusahihisha mitihani, kusahihisha madaftari na kuandaa maandalio ya kesho. Kwa bahati mbaya sasa itokee mama ndiyo mwalimu, baba labda ni mhasibu, yule mama anakaa kufanya kazi ya ualimu pale nyumbani mpaka saa nane ya usiku hebu niambie, baba amelala yupo kitandani. Unatarajia hiyo nyumba ya mwalimu na huyo mumewe inakuwaje? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe Serikali hata kama atafanya kazi kwa o kwa muda huo…
MWENYEKITI: Mheshimiwa umemaliza muda wako naomba ukae!
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana, naunga mkono hoja.