Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizari ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Joseph Kasheku Musukuma

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizari ya Maji na Umwagiliaji

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia kwa mara ya kwanza. Niungane na Waheshimiwa Wabunge wenzangu katika kutoa pole kwa wananchi wa Arusha.

Mheshimiwa Naibu Spika, namwaangalia rafiki yangu Mheshimiwa Kangi Lugola, ameondoka; naanza kwa kuunga mkono hoja, nami ndiye nitakayeongoza ile sauti ya ndiyo ambayo atazunguka nayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Rais, pia nampongeza sana Mheshimiwa Waziri na Naibu wake kwa kazi nzuri wanayoifanya kwenye Idara ya Maji. Sisi wengine ni waathirika wa miaka mingi na tunaona mabadiliko yanavyokwenda kwa speed. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi niko tofauti kidogo na Waheshimiwa Wabunge wenzangu wanaosema tusipitishe, hela ni ndogo. Binafsi yangu naona hii hela ni nyingi sana, tatizo itoke yote. Kwenye bajeti ya mwaka 2016 ukisoma ukurasa wa 13 utaona tulipitisha shilingi bilioni 915 lakini mpaka leo ni shilingi bilioni 181 tu. Kwa hiyo, Wizara ya Fedha wakitoa pesa yote, hii pesa ni nyingi wala hata hizi kelele hatutazisikia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kitu cha pili, kwenye Ilani ya CCM tumeahidi kumaliza matatizo ya maji, lakini hatukuahidi kumaliza mwaka huu peke yake, bado tuna miaka mitano. Kwa hiyo, kazi zilizoahidiwa kwenye Ilani ni nyingi, wala siyo moja na kila mahali tunataka pesa. Sisi tunataka barabara, tumepiga kelele tunataka afya, tunataka watoto wasome bure; kwa hiyo, hizi hela ni nyingi, tuziunge mkono, wala tusiwasumbue, tuwape nafasi waende wakafanye kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine, mimi nashangaa wana-CCM wenzangu, jana nimesikiliza mchango wa Mheshimiwa Kitwanga analalamika anasema yeye ataenda ku-mobilize wananchi 10,000 wakazime mashine. Nilisikitika sana! Nataka niwaulize ninyi Mawaziri wa Mheshimiwa Dkt. Magufuli, hivi vile viapo mnavyovila mnavifahamu maana yake? Kama hamvijui sina hakika kama mko sawasawa na kama hamko sawasawa Mheshimiwa Ndalichako hebu apitishe operation ya vyeti, pengine na kwenyewe kuna feki za kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, inawezekana vipi mtu aliyekuwa Waziri anasimama anasema kwa kuwa nilikuwa Waziri, nilikuwa nimebanwa kuzungumza. Kwa hiyo, sisi ambao hatuzungumzi kwa kuwasaidia ninyi, tumebanwa na nani? Anasimama anasema nilikuwa nimebanwa, sasa nazungumza, naenda kuunganisha wananchi 10,000 wakazime mashine ya Ihelele. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niwakumbushe kidogo, mwaka 2014 Mheshimiwa Kitwanga nilitegemea atakuwa pale. Akiwa Waziri wa Nishati na Madini, aliyekuwa anashughulika na mambo ya madini, alikuja Geita, mimi kama Mwenyekiti wa Mkoa niliwalazimisha wananchi wasitoke mpaka walipwe na Mzungu. Yeye akaja, akamwambia Mkuu wa Mkoa, hata kama kuna Mwenyekiti wa Mkoa, piga mabomu. Kweli kesho yake tulipigwa mabomu!

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimwambie Waziri wa Mambo ya Ndani, siku anaenda kuunganisha wale wananchi, apeleke mabomu Misungwi pale, aonje joto la jiwe. Haiwezekani Waziri aliyeapa kiapo, akitimuliwa anakuja humu anatuchanganya sisi wengine ambao hatujui mambo mnayoongea kwenye Cabinet.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ndugu yangu Mheshimiwa Nape yuko hapa, jana alichangia…

Hakuna kuogopana humu, anayeguna nani? Mimi ndio nachangia. Ndugu yangu Mheshimiwa Nape aliyekuwa Mwenezi wangu wa Taifa, jana alizungumza mambo mazuri, lakini kuna moja alisema tusipowatekelezea suala la maji wananchi, hawataturudisha, haiwezekani! Wananchi wa Tanzania wanatutegemea kwa mambo mengi wala siyo maji peke yake na tumewafanyia vizuri. Hata hizi Ilani hazijaanza kuzaliwa kwenye Awamu ya Tano, tumepitisha awamu nne, zote zilikuwa zinaandaa hayakamiliki. Kwa hiyo, suala hapa siyo kulazimisha Ilani yote ikamilike. Rais gani aliyewahi kutekeleza asilimia mia moja ya Ilani? Tusibebeshane mzigo! Wewe ulikuwa unaongea nilisikiliza, sikiliza! Kwa hiyo, tupeane nafasi, Rais wetu anafanya kazi nzuri, tusianze kumchambachamba humu ndani. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri aliyoifanya pale Geita. Tulikuwa na malalamiko ya awamu mbili. Leo ukifika Geita, hatujawa na asilimia mia moja lakini tuna nafuu. Tuna mradi wa shilingi bilioni sita; uko asilimia karibia 85, halafu tusimame hapa kuiponda Serikali ya Awamu ya Tano, kwa miaka miwili! Haiwezekani! (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna Wabunge wamo humu akina Mheshimiwa Mnyika, unataka tumalize tatizo la maji leo, kwa nini haisemi population ya Dar es Salaam? Wakati anaomba maji Awamu ya Kwanza alivyokuwa Bungeni, Jimbo lake lilikuwa na watu wangapi? Kila siku binadamu wanaongezeka, hatuwezi kumaliza tatizo hili kwa awamu moja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tuipitishe bajeti hii kwa speed, tushauri tu kwamba Wizara ya Fedha iachie fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niongee kidogo kwamba tumeona mfano kwa CEO wa DAWASCO; hivi Mheshimiwa Waziri watu kama hawa, wamesifiwa mpaka na Kamati, tunawezaje kutafuta watu kama akina Ruhemeja kwenye Tanzania hii? Mtu amekuta kuna deni la shilingi bilioni 40 na kitu, leo hakuna deni! Kwa nini watu kama hao msiwachukue na kuwapa vyeo vingine vikubwa ili wakawafundishe na Wakurugenzi wa kwenye Halmashauri nyingine na Majiji mengine? Tusikae hapa kuponda bajeti, issue kubwa hapa hela zitoke. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nawaomba Waheshimiwa Wabunge wenzengu wa CCM, Kanuni ya 105 imeelekeza jinsi ya kufanya, hatuhitaji kuponda bajeti hapa, tunahitaji kuwapa zile siku sita wakajadili, waje watuambie, lakini bajeti ipite tena kwa ndiyo. Kama Mheshimiwa Kangi Lugola anataka kuzunguka na ndiyo za Waheshimiwa Wabunge, term hii sasa aandae record, ataenda na za bass ambayo hajawahi kuiona.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.