Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ZAYNABU M. VULU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii nami jioni hii ya leo niweze kutoa mchango wangu katika hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, Waswahili wana msemo wao, wanasema hivi, “ng’ombe hashindwi na nunduye.” Nina hakika pamoja na uchache wa pesa ambazo zimetolewa, Serikali ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli haitashindwa kutekeleza miradi ya maji ambayo tunaitarajia katika maeneo yetu. Nawatoa hofu wenzangu, hilo walijue kwamba hakuna nundu yoyote ambayo ng’ombe imemshinda akasema mimi leo, siwezi kutembea, nundu hii imezidi ukubwa, nakaa chini. Hata siku moja! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninapozungumzia suala la maji, lazima tutazungumzia suala la fedha; na tunapozungumzia suala la fedha, maana yake tunataka miradi hii ifike kwa walengwa na kwa wakati. Tumeona baadhi ya maeneo yamepata maji.
Mhshimiwa Naibu Spika, nimesoma kitabu cha hotuba, mimi natoka Mkoa wa Pwani; Mwenyezi Mungu ametupa neema, tuna Mto Rufiji, tuna Mto Ruvu, tuna Mto Wami, lakini pamoja na uzuri wa wananchi wale kulinda vyanzo vya maji katika mito ile, kwenye kitabu hiki yametajwa mabomba yaliyowekwa kutoka Ruvu, mitambo ya Ruvu Juu na Ruvu chini kwenda Dar es Salaam na baadhi ya maeneo kwa Wilaya ya Kibaha, Bagamoyo na Dar es Salaam. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunataka kumtua ndoo mwanamke kichwani. Wanawake wa Pwani ndoo wao kwao siyo shida, maji siyo shida, lakini wao wanachotaka miundombinu ya maji kutoka kwenye mito iweze kufika kwenye maeneo yao. Unakuwa na mti wa matunda unatarajia mti ule ukupe kivuli na ule yale matunda, lakini kule baadhi ya maeneo wanatunza maji, wanajitahidi, lakini maji yale yakiwekwa mabomba moja kwa moja yanakwenda Dar es Salaam. Siwaonei wivu ila nasi tunahitaji hayo maji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali, imetenga fedha, lakini bado fedha zile hazitoshelezi. Kwa mfano, Shule za Sekondari za Rufiji, wako karibu na Mto Rufiji, lakini shule zile kama Utete, Ngorongo, Kibiti na maeneo mengine hawana maji. Kuna visima vimechimbwa lakini tunaomba yawekwe mabomba ambayo yatafika kwenye shule.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama imeshindikana, kuna DAWASA na DAWASCO waweke miundombinu ya kuvuna maji ya mvua ya kuweka matenki. Maji yale siyo kwa watoto wa kike tu na akinamama wanaoyahitaji, hata watoto wa kiume wanahitaji maji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, bado katika vyanzo hivyo hivyo vya maji, kuna wakulima wadogo na wakubwa. Naomba Wizara husika na Taasisi husika ziangalie utaratibu gani utatumika kuzuia zile dawa ambazo zinatumika kwenye kilimo zisiende zikaharibu afya katika yale maji, kwa sababu baadhi ya watu hawana mabomba, wanakunywa maji yale yale ambayo kwa sasa hivi kwa mfano mvua zimekuwa nyingi, yametiririka maeneo mengi, dawa nyingine ni sumu. Matokeo yake watu wanakunywa maji, maradhi ya aina mbalimbali yanapatikana. Mwishowe tunajiuliza, kunani? Mbona magonjwa yamekuwa mengi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba uwekwe utaratibu, wakulima wadogo wadogo wapate elimu, wapewe namna ya kuweza kuhifadhi vyanzo vyao vya maji ili zile dawa wanazomwagilia kwenye mazao zisiweze kuharibu yale maji wanayoyatumia.
Mheshimiwa Naibu Spika, hali kadhalika, katika huo Mradi wa Ruvu Juu ambao umeanzia Mlandizi; mto umeanzia Morogoro umekwenda Dar es Salaam; watu wanaokaa maeneo ya Kisarawe, kuna eneo la Kimaramisale, Kigogo, Mzenga na Kurui. Hao wote hawana maji safi na salama yanayotoka kwenye mabomba ambapo wao ndiyo wanatunza vile vyanzo vya maji vya Mto Ruvu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali, pamoja na kutenga hizo fedha, lakini bado kuna utaratibu wa kufuatwa, tunaomba tusaidiane, tushirikiane nao, inapobidi hata kutoa elimu wananchi wa Kisarawe tutakuwa tayari hata kujitolea katika uchimbaji wa mitaro, watuletee mabomba tu. Sisi shida yetu ni mabomba na dawa za kuhakikisha maji yale hayataharibu afya za watu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona mvua hizi jinsi gani maji mengi yamepotea yamekwenda baharini na jinsi gani maji yameharibu kilimo chetu, lakini bado kungeweza kukafanywa utaratibu wa kuvuna maji ya mvua, elimu ikatolewa majumbani. Siyo mara ya kwanza nasema neno hili. Elimu ikatolewa mashuleni, pesa zikatengwa na Halmashauri zetu na Serikali Kuu ili kuhakikisha maji ya mvua yanavunwa, wananchi wanatumia maji ya mvua kwa wakati fulani, yakiisha wanajua sasa maji yamekwisha. Tunaachia maji yanakwenda bila kuwa na utaratibu wa kuyavuna. Kwa kweli hilo ni tatizo kubwa sana! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kilimo cha umwagiliaji, tuongeze scheme za umwagiliaji katika maeneo yetu. Nchi yetu haiwezi kuwa na shida ya njaa; iwe mchele au sukari lakini scheme za umwagiliaji zikiongezwa tutakuwa tumevuka hatua kubwa sana especially akinamama wanaolima mpunga. Wale akinamama wakiwezeshwa, wakajengewa scheme nzuri za umwagiliaji, watalima mpunga wa kutosha, watalima miwa ya kutosha, tutaondokana na njaa, watu watajiwezesha, wataendeleza maendeleo katika nchi yetu. Naomba sana, hilo pia liangaliwe na Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo la adha ya mfumo wa majitaka. Mji wa Dar es Salaam umekua vibaya sana, kwa maana ya kwamba kwanza ongezeko la watu limekuwa kubwa, miundombinu ya nyumba zile za kwetu tulizozaliwa nazo za vyumba sita banda la uani, hazipo! Kumejengwa nyumba za ghorofa, lakini miundombinu ya kuchukulia maji machafu bado haijakaa sawa. Naomba sana hilo nalo liangaliwe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naelekea Kisiwa cha Mafia. Sote tunaifahamu Mafia. Mafia ni kisiwa ambacho kina visiwa vingine zaidi ya vitatu, lakini kuna kisiwa kimoja kinaitwa Jibondo. Kisiwa hicho kina watu zaidi ya 3,000, lakini watu wale hawayajui maji matamu mpaka wavune maji ya mvua kwa sababu wako juu ya jabali. Juhudi zimeanza kuoneshwa za kutaka kupelekewa maji; ni kilometa tisa tu kutoka kisiwa kikuu kwenda kwenye Kisiwa cha Jibondo na usafiri wake ni boti. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaiomba Serikali iangalie utaratibu wa kuwajengea miundombinu ya kuvuna maji ya mvua au kuweka utaratibu wa mabomba kutoka kisiwa kikuu cha Mafia kupita chini ya bahari ili waweze kupatiwa maji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru na naunga mkono hoja.