Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nyang'hwale
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii na mimi niweze kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyenipa afya njema kwa siku ya leo na kuweza kusimama hapa. Pia nimshukuru Rais, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa na Baraza lote la Mawaziri kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya ya kutumbua majipu. Ni kazi nzuri sana inayofanyika pamoja na kwamba wengine wanakasirika lakini ndiyo ilikuwa kiu ya Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa napenda kuunga mkono hotuba hii nzuri ambayo imesheheni mambo mazuri. Napenda niwakumbushe wenzetu Kambi ya Upinzani, kuna mchangiaji mmoja alisema kipindi cha nyuma kwamba ninyi wana CCM mnapenda sana kupongeza, mimi sipongezi, wakati Mwenyezi Mungu anasema usiposhukuru kidogo hata kikubwa hauwezi ukashukuru. Hata kwenye maombi kwanza unamshukuru Mwenyezi Mungu kwa alichokupa na unachohitaji unaendelea kuomba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hivyo, napenda niikumbushe Serikali yangu Tukufu, tunaambiwa tunalalamika, hatulalamiki tunakumbushana. Mheshimiwa Rais wakati wa kampeni kwenye Jimbo langu la Nyang’hwale tulimweleza matatizo yetu na akaahidi. Tulikuwa na ahadi ambayo tuliahidiwa na Rais wa Awamu ya Nne kuhusu barabara ya kutoka Kahama – Nyang’hwale - Busolwa - Busisi kwamba itajengwa kwa kiwango cha lami. Pia alipokuja Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli wakati wa kampeni nilimkumbushia hilo na akaahidi kwamba barabara hiyo itajengwa. Kwa hiyo, naendelea kukumbusha barababa hiyo ijengwe angalau kwa kilometa chache kila mwaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda niishukuru Serikali yangu kwa ahadi yake ya kusambaza umeme vijijini. Jimbo la Nyang’hwale tayari tumeshapata umeme lakini ni kwa kiwango kidogo sana. Vijiji vingi havina umeme na Watanzania wengi waliopo Jimbo la Nyang’hwale wanasuburi kwa hamu umeme kwa ajili ya kufanya kazi zao mbalimbali ambazo zinahitaji umeme. Wanahitaji wafunge mashine ndogondogo kwa ajili ya kukamua alizeti, mpunga na mambo mengine.
Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri wa Nishati muda utapofika utukumbuke sana Jimbo la Nyang’hwale kutukamilishia ahadi ambazo ametuahidi mara nyingi kutupa umeme katka Jimbo la Nyang’hwale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia Jimbo langu la Nyang’hwale tuna tatizo kubwa la maji, nimeshaongea tangu nilivyoingia mwaka 2010. Nimezungumzia suala la maji kwa nguvu zote na Serikali ilisikia na ikaitikia wakatuahidi kutujengea mradi wa maji. Tuliahidiwa mradi mzuri na mkubwa wa kutoka Ziwa Victoria na kusambaza maji katika Jimbo la Nyang’hwale. Tumepangiwa shilingi milioni 15.7 ndani ya miaka mitano na huu wa sita tumeshapewa shilingi bilioni 1.9. Naomba sasa ili niweze kurudi tena Bungeni mwaka 2020 mradi huo wa maji ukamilike.
Mheshimiwa Waziri Mkuu kama utapenda tuwe pamoja tena mwaka 2020, naomba mradi huu ukamilike. Waziri wa Maji nipe hayo maji ili mama zangu na dada zangu waweze kunipa kura tena niwe na jambo la kusemea vinginevyo sirudi tena. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la afya. Kwenye Jimbo langu kuna hospitali ambayo imepandishwa hadhi na kuwa Hospitali ya Wilaya lakini kwa bahati mbaya hospitali ile ina majengo ya kizamani, haina wodi, haina x-ray na vifaa tiba hakuna. Kuna wodi mbili tu, wodi moja ya akina baba wanachanganywa wagonjwa wa maradhi yote mle ndani na wodi ile ina vitanda kama tisa tu. Kwa hiyo, naomba ili sasa iwe Hospitali ya Wilaya tuletewe vifaa mbalimbali ikiwa ni pamoja na vifaa tiba na kupanua majengo ikiwemo majengo ya wodi ya kulaza wagonjwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais alipokuja Jimboni kwangu aliwaahidi wachimbaji wa madini ya dhahabu kwamba watatengewa eneo, kuna eneo moja linaloitwa Mwasabuka huko Nyijundu, alisema watagawiwa wachimbaji wadogo wawe huru wapewe leseni ili waweze kuchimba na waweze kusaidiwa na Serikali ili waweze kunyanyua kipato chao na kipato cha Serikali.
Naomba kumkumbusha Waziri wa Nishati na Madini kwamba ahadi hiyo aifuatilie ili wananchi hawa, vijana hawa ambao wanapata kipato chao kutokana na uchimbaji wa madini basi wawafikirie na kuweza kuwatekelezea ambayo waliwaahidi wakati wa kampeni wasione kwamba tulikuwa tunawadanyanga kwa ajili ya kutupa kura, waone kabisa tulikuwa tukiwaahidi mambo yaliyo sahihi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la elimu, naishukuru Serikali imeanza kutekeleza mpango wa elimu bure. Kama walivyosema wachangiaji wengine, tuangalie stahiki za walimu wetu, wazipate kwa muda ili wawe na ari na kasi na nguvu mpya kabisa ya kuweza kusimamia suala la elimu. Kwa sababu stahiki zao zinachelewa, zikichelewa amani ama imani ya kazi inashuka. Kwa hiyo, naiomba Serikali ijaribu kuangalia sana stahiki zao ili waweze kuwa na moyo wa kufanya kazi hiyo bila kutetereka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa napenda kuongelea kuhusu wafugaji. Katika Jimbo la Nyang’hwale wafugaji wetu wamesahaulika. Nimeangalia katika mipango yote iliyopita sijaona wafugaji wa Jimbo la Nyang’hwale wamefikiriwa nini, hakuna soko, malambo wala majosho. Kwa hiyo, naomba wafugaji wa Jimbo la Nyang’hwale nao wafikiriwe kuboreshewa soko la mazao ya mifugo yao. Nimeangalia kwenye kitabu cha mpango, Mkoa wa Simiyu vinajengwa viwanda vitatu vya ngozi lakini Geita hakuna kiwanda hata kimoja cha ngozi, inakuwaje namna hii? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakulima wa Jimbo la Nyang’hwale na wakulima wote wa Tanzania kwa kweli wamekuwa wanakata tamaa kutegemea kilimo kwa sababu soko la mazao siyo la uhakika, pembejeo zinakuja mbovu, za gharama kubwa na zinachelewa kufika. Naiomba Serikali, kwa sababu wimbo mkubwa ni kwamba tuwasaidie wakulima, hebu tujaribu kweli kuwasaidia wakulima kwa kuwasaidia pembejeo na soko lao liwe la uhakika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bila kusahau napenda nimkumbushe Mheshimiwa Waziri Mkuu, kulikuwa na mchakato wa Makao Makuu ya Wilaya ya Nyang’hwale na bahati nzuri ulishaisha na Serikali ikatamka Makao Makuu ya Nyang’hwale yatakuwa Karumwa. Kwa bahati mbaya mpaka sasa hivi hati ya kujulisha kwamba Makao Makuu ya Nyang’hwale yako wapi haijatoka.
Mheshimiwa Waziri Mkuu utakaposimama hapa, waambie wananchi wa Jimbo la Nyang’hwale, hawa wapinzani hususan CHADEMA niliowashinda vibaya sana wanapiga kelele na kusema kwamba haya Makao Makuu hayapo mnadanganywa na Serikali ya Chama cha Mapinduzi. Naomba utakaposimama uwajibu hawa Watanzania wa Nyang’hwale pamoja na hao wapinzani, waelewe Makao Makuu ya Wilaya ya Nyang’hwale yako Karumwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuzungumzia kuhusu ardhi. Tuna ardhi nzuri, tunaomba ipimwe ili wananchi wetu waweze kunufaika na ardhi yao. Kwa bahati mbaya kuna zile hati za kimila, wananchi wetu wamepimiwa tangu mwaka 2011 mpaka leo hawajazipewa, ni zaidi ya hati 800 na kitu. Serikali ina mpango gani sasa kuwapa hizo hati za kimila ili ziweze kuwasaidia hawa wananchi kupata mikopo midogo midogo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala ambalo napenda kulizungumzia ni UKIMWI. Mimi ni Mjumbe wa Kamati ya UKIMWI na dawa za kulevya. Tunajaribu kuangalia matatizo makubwa ya UKIMWI yanaanzia wapi, tumejaribu kuzunguka na kuongea na wadau mbalimbali wakatushauri na kutuambia na sisi wenyewe kwa kuona kwa macho matatizo ya UKIMWI yanaanzia kwenye ulevi. Kuna ulevi wa aina nyingi, kwanza mirungi, viroba, bangi, watakapokunywa na kuvuta wanajisahau wanaingia kwenye ngono zembe. Kwa hiyo, angalieni sana UKIMWI unaanzia wapi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaiomba Serikali iweke utaratibu mzuri kutoa elimu ya UKIMWI kuanzia chekechea, shule za msingi, sekondari mpaka vyuo vikuu waelezwe UKIMWI unaanzia wapi na ni tatizo gani. Serikali ipange utaratibu wa kutoa elimu kwenye shule za msingi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali na hii bajeti ambayo imesomwa na Waziri Mkuu kuhusu shilingi milioni 50. Nategemea kwangu kupata shilingi bilioni 3.2, naamini kabisa ikitolewa elimu nzuri kwa hawa ambao wanalengwa, watanyanyua vipato vyao lakini kwanza wapewe elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ukusanyaji wa mapato katika Halmashauri. Halmashauri yangu ina vipato vingi lakini vidogovidogo lakini mapato yale hayakusanywi. Kwa nini hayakusanywi? Wanatumia stakabadhi za kuandika kwa mkono. Naomba zile mashine zisambazwe katika Halmashauri zote…
MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wako umemaliza, naomba ukae.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja asilimia mia moja kwa mia moja.