Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizari ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Suzana Chogisasi Mgonukulima

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizari ya Maji na Umwagiliaji

MHE. SUZANA C. MGONOKULIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia jioni ya leo Wizara ya Maji. Maji ni uhai wa kila kitu, ikitokea jambo lolote hapa mtu mwingine ameanguka ghafla hapa Bungeni akifika pale hospitalini Madaktari wataanza kumwongeza drip la maji. Hivyo, tuone umuhimu wa maji unavyotakiwa katika maisha ya mwanadamu. Hata magari, meli, ndege vyote hivyo vinahitaji maji. Hata sasa hivi moto ukitokea jengo lolote utaona tunasema gari la zimamoto liko wapi, maji yaje ili waweze kuzima moto. Kama kweli maji ni uhai basi ifikie wakati muafaka wa kuona Serikali inaona jambo hili ni la umuhimu kitaifa na wazingatie kwamba kwa kukosa maji ni kukosa kuwa na maendeleo katika Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sera yetu inasema tunataka kumtua mwanamke ndoo ya maji kichwani. Imeonekana suala la maji siyo tatizo la kifamilia ila ni tatizo la mwanamke ambapo si kweli. Tatizo la maji ni tatizo la kitaifa na hivyo tulijue kama ni tatizo la kifamilia ni janga la kitaifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ningeomba kutokana na kuwa mwaka jana tulikuwa tumeweka ongezeko la bei ya mafuta ya dizeli na petroli kwa ajili ya kuhakikisha maji yanafika vijijini lakini imeonekana ongezeko ya bei ya mafuta haya limetatua changamoto ya maji kwenye miji yetu. Changamoto ya maji kwenye miji si kubwa kama ilivyo kwenye vijiji. Hivyo basi katika bajeti hii naomba Wabunge wote tuombe tuwe na ongezeko tena la tozo kwenye mafuta tufikie Sh.100, basi asilimia 70 iende vijijini na asilimia 30 iende mjini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ujumla suala la maji ameachiwa mwanamke utaona hata wakati wa uzinduzi, Waziri anakinga maji kwenye ndoo anamtwisha mwanamke kwa nini basi akikinga maji asimtwishe mwanaume wakati suala hili ni tatizo la kifamilia? Naomba tuelewe kwamba suala la maji siyo tatizo la mwanamke ni la kifamilia, hivyo basi, kama ni tatizo la kifamilia, isionekane ni kumtua ndoo mwanamke kichwani bali ni pamoja na waume zetu tuliokuwa nao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa niingie kuzungumzia Mkoa wangu wa Iringa, mkoa wenye neema na uliobarikiwa ambao una vyanzo vya maji, tuna Bwawa la Kihansi, Bwawa la Mtera, Mto Lukosi, Mto Mtitu na Mto mdogo Ruaha. Cha ajabu pamoja na kuwa tuna vyanzo vyote hivyo kuna vijiji vina shida ya kuliko mtu anavyoweza kufikiria. Vijiji hivyo ni Nyakavangalala, Lyamgungwe, Lupembelwasenga, Luhota, Mkalanga, Usolanga na vingine vingi katika mkoa huu pamoja na Mji Mdogo wetu wa Ilula ambapo chemchem ya Ibofye iko jirani sana na nafikiri ni kama mita za mraba zisizopungua arobani na tano. Tumeshindwa kuweka miundombinu ili watu wa Mji Mdogo Ilula waweze kupata maji? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi navyozungumza Mji Mdogo wa Ilula wanauziwa maji ndoo ya lita ishirini kwa Sh.500. Huo ni Mji Mdogo tena uko kwenye barabara kuu inayotoka Dar es Salaam kuelekea Zambia. Naomba Mawaziri wenye Wizara hii washughulikie tatizo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, chanzo hicho cha Ibofye kwanza kabisa kwenye bajeti ya mwaka 2000-2005, Bunge hili lilipitisha bajeti ili waende kufanya kazi ya miundombinu katika chanzo hicho, wakati huo akiwa Mheshimiwa Mbunge Mlawa. Hadi leo navyozungumza sielewi hata hizo fedha zilikoishia. Naomba Mawaziri wahusika walifuatilie suala hili iliwaelewe. Ndiyo maana tunasema tutakapoweka ongezeko kwenye bei ya mafuta kuwe na bodi maalum itakayofuatilia ongezeko la fedha hizi ili ziende kwenye miradi tuliokusudia wa kupunguza uhaba wa maji kwa wananchi katika taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Iringa ni kati ya mikoa ile minne inayozalisha sana chakula nchini Tanzania.

Nataka niseme njaa tunaitaka kwa makusudi kwa sababu ya kutokuwa na mbinu mbadala kwa wakati muafaka wakati nchi yetu ina wataalam waliosomea na kubobea. Tatizo letu ni kwamba wakati wa mvua hatuna mabwawa ya kutunza maji ya mvua ili wakati wote tuweze kuendelea na kilimo cha umwagiliaji. Kutokana na hilo, tuone ni wakati sasa wa kuhakikisha bajeti hii inayokuja kuombwa na Waziri mwenye dhamana imeongezeka ili tuweze kujenga mabwawa maeneo hayo ambayo nasema ni lazima tuwe na mabwawa yanayotunza maji ya mvua tuweze kuondokana na tatizo la maji. (Makofi)

Katika Mkoa wangu wa Iringa akinamama wengi wajasiriamali ni wakulima wa mazao ya mbogamboga. Hivyo kukosa mifereji ya umwagiliaji iliyo bora wanashindwa kumudu shughuli zao za kilimo na kuweza kujikwamua katika dimbwi la umasikini walilokuwa nalo ukizingatia kazi kubwa ya kulea familia ni ya mama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Waziri mwenye dhamana katika Mkoa wangu wa Iringa katika maeneo haya yote niliyoelekeza na vijiji ambavyo sikuorodhesha hapa kutokana na wanawake wale walivyo na juhudi kwenye kilimo ahakikishe amepeleka mradi wa maji ili waweze kuendelea na shughuli zao za kilimo cha mbogamboga.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna Kata yetu ya Mahengeā€¦

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. SUZANA C. MGONOKULIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, basi naunga mkono hoja ya Upinzani asilimia mia kwa mia.