Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Muleba kusini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. PROF. ANNA K. TIBAIJUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Na mimi naomba niungane na waliotangulia kwanza kabisa kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyetuwezesha kuwa hapa leo katika Jumba hili Tukufu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sina budi kuanza kwa kusema kwamba naunga mkono hoja asilimia mia moja. Niwapongeze wananchi wa Tanzania kwamba katika uchaguzi uliopita Taifa limeibuka na kiongozi. Naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa uongozi wake na niwapongeze wananchi wa Tanzania kwa kumpa zana na silaha ya Urais. Maana ifike mahali tutofautishe kati ya urais na uongozi, vinaweza vikawa vitu viwili tofauti, inapokuwa kitu kimoja mambo yanaweza kwenda kwa kasi na inakuwa hapa kazi tu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana pia Mheshimiwa Kassim Majaliwa, Waziri wetu Mkuu ambaye hakuna shaka anafanya kazi inayoonekana na sisi ambao tumepata bahati ya kumfahamu ni mtu ambaye anafanya kazi kwa umakini sana. Kwa hiyo, sina wasiwasi kabisa kwamba timu ya Baraza la Mawaziri ilivyopangwa kwa umakini Taifa hili linaweza likaiona neema na naona speed inaanza kuwapa wenzetu kiwewe. Wasiwe na kiwewe watulie kwa sababu kazi isipofanyika watu watalalamika kazi haifanyiki, sasa inapofanyika watu wanalalamika, hatuwezi kuwa na Taifa la walalamikaji tunataka Taifa la watu wa kujenga hoja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sina budi kuzungumzia kwamba Taifa letu sasa tunaingia katika awamu muhimu ambayo inatufafanua hata kwa ngazi za ulimwengu. Naomba nimpongeze sana Rais wetu kwamba katika diplomasia yake amefanya kitu ambacho wanadiplomasia wanakienzi sana, ameanzia kutembelea nchi jirani. Katika diplomosia iliyobobea hiyo ndiyo diplomasia kwa sababu unaanza kuwatembelea watu ambao wanaitwa your natural allies, watu ambao una maslahi nao kwa karibu sana. Kwa hiyo, ni jambo la kupongeza kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa bajeti iliyo mbele yetu nimeiangalia, nimeipitia kwa umakini sana, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwamba imekaa vizuri. Tunaposimama hapa kuchangia ni kuboresha hasa kwa upande wangu kuzungumzia mtazamo wa wananchi wa Muleba Kusini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawashukuru sana wananchi wa Muleba Kusini, hali yangu ilikuwa ngumu lakini mnaniona nimerejea mjengoni, ahsanteni sana Muleba Kusini. Waswahili wanasema ukweli ukidhihiri uongo hujitenga. Kwa hiyo, nimesimama hapa kwa mantiki hiyo na nataka kusema kwamba kazi inaendelea na tumeshapata watu wa kutuongoza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, najua Mawaziri wamejipanga chini ya Waziri Mkuu na Mheshimiwa Rais na Mama Samia Suluhu ambaye ni kielelezo tosha kwamba wanawake tunaweza, naye nampongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ninawawakilisha wakulima, wavuvi na wafugaji wa Muleba Kusini. Hali yao siyo nzuri sana, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Nchemba alikuja akaona tuna matatizo ya wafugaji na wakulima. Hapa ninavyozungumza mifugo katika Mkoa wa Kagera iko kwenye hifadhi.
Kwa hiyo, naomba kabisa Mheshimiwa Waziri Mkuu na wewe utuwekee nguvu zako tuweze sasa kuhaulisha hii ardhi ambayo iko kwenye hifadhi ambazo zimepitwa na wakati tuweze kupata mahali pa kuchungia. Ni tatizo kubwa sana kwamba ukitaka kutoa mifugo ile kwenye hifadhi itabidi upeleke kwenye mashamba ya wakulima itazua migogoro ya ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kilimo pia tusisahaulike sisi. Suala la mnyauko bado halijakaa sawasawa na magonjwa yanaibuka kila siku. Kituo chetu cha Utafiti cha Maruku kimesahaulika. Naomba Kituo cha Maruku kwa ajili ya Ukanda wa Mkoa wa Kagera kipewe kipaumbele na Mheshimiwa Waziri Mkuu katika hili utuunge mkono.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pembejeo. Muleba ni wakulima wa maharage, migomba na nafaka mbalimbali lakini hatujawahi kuona vocha hata moja. Kwa hiyo, katika hili tumesahaulika na tunaposahaulika inakuwa njaa. Nakumbuka Mheshimiwa Waziri Mkuu aliyestaafu aliwahi kunipa mahindi nipeleke Muleba, hii sio tabia yetu, lakini tukisahaulika katika uwezeshwaji, mambo yanakuwa magumu sana. Kwa hiyo, suala hili nalo tuliwekee mkazo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikimbilie sasa kuzungumzia suala la miundombinu. Bahati nzuri nchi yetu sasa hivi inaendeshwa na wahandisi na mainjinia naona kila siku wanapangwa katika sehemu mbalimbali. Suala la reli halina mjadala, nchi haiwezi kuendelea bila reli. Nikizungumzia kwa mtazamo wa sehemu yoyote ile, ukienda nchi za Ulaya unakuta reli inafanana na mishipa ya damu, wanasema ni capillary system. Kwa sababu nchi ya kilimo kama haina reli haiwezi kushindana kwenye masoko ya dunia. Ukibeba mizigo, hususan mahindi, kahawa kwa ma-semi trailer huwezi kushindana katika uwanja wa dunia. Kwa hiyo, suala la reli lipewe mkazo, napongeza kwamba limepewa kipaumbele lakini tunazungumzia reli basically kwenda kila mahali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sisi watu wa Mkoa wa Kagera hususan Muleba Kusini, tunaomba kabisa Serikali hii Tukufu, chini ya Jemedari wetu Rais, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli na chini ya Prime Minister, Mheshimiwa Kassim Majaliwa, meli ya Ziwa Victoria imekuwa sasa lazima niseme aibu, imekuwa ni aibu ya Taifa wananchi wanasubiri meli. Wale watu walioangamia kwenye MV Bukoba wakiibuka leo zaidi ya miaka 20 baadaye hatujanunua meli jamani hatutapata mahali pa kukimbilia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapohapo niunganishe usalama katika Ziwa Victoria. Ziwa Victoria sasa hivi, wavuvi wenyewe ndiyo wameweka ulinzi wao shirikishi. Naomba sana Waziri wetu wa Mambo ya Ndani na hapa naomba Waziri Mkuu utuwekee nguvu kwamba ulinzi katika Ziwa Victoria uimarishwe kwa sababu wananchi wametelekezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu muda siyo rafiki nikimbilie sasa suala la miundombinu hasa barabara. Nilishapiga magoti, kila jioni nasali tupate barabara ya kwenda kwenye Hospitali yetu Teule ya kutoka Muleba – Rubya. Hospitali Teule unapita kwenye mlima mkali na miamba, akina mama wanajifungua pale kwa sababu ya mtikisiko kwa ile barabara ilivyokuwa mbovu kwenye Mlima Kanyambogo. Sisi Muleba Kusini tupo tayari kuchapa kazi chini ya Jemedari wetu Rais, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli na timu yake aliyoipanga na Waziri Mkuu lakini sasa msitusahau tuko mbali, lakini nashukuru kwamba Waziri Mkuu umshapita umeona wewe mwenyewe umbali wetu, kwa hiyo bila kuwekewa juhudi maalum mambo yatakuwa magumu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niungane na wale waliozungumzia suala la vijana na ajira. Tusipowawekea vijana wetu utaratibu wa ajira itakuwa vigumu. Sisi watu ambao tumeajiriwa tunapenda kuwaambia vijana wajiajiri, watajiajiri namna gani bila uwezeshwaji? Kwa hiyo, suala la kuwezesha vijana ni muhimu sana na uwezeshaji ni taasisi za Serikali kuweka mazingira wezeshi, siyo kuwa-harass wale vijana kama vyombo vya kuwafuatilia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, kulipa kodi, unamwezesha kijana, unaangalia accounts zake unaona kama kweli amepata faida, siyo kila mfanyabiashara anapata faida. Ifike mahali ijulikane kwamba mfanyabiashara pia anaweza akapata hasara na anapopata hasara itambuliwe. La sivyo vyombo vyetu vinaweza vikafunga small micro enterprises, viwanda vidogo vidogo vya vijana vikafungwa vyote kwa sababu ya harassment tukashindwa kwenda mbele kama Rais alivyosema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hayo ndiyo ya kwangu na naomba niwasihi vijana kwamba dawa za kulevya ni hatari, UKIMWI ni hatari, lakini nasema na viroba ni hatari. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme viroba ni hatari, navikemea Muleba Kusini, navikemea popote pale. Nilikuwa tayari kushindwa uchaguzi kama nikisema eti vijana wanywe viroba ndiyo wanipigie kura, wasinipigie kama ni mambo ya viroba. Kwa hiyo, suala la viroba ni hatari sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika nchi ya Sweden, pombe inauzwa na Serikali, labda niseme maana yake Taifa hii limetusaidia sana. Katika nchi ya Sweden, Shirika la kuuza na kununua pombe Kali ni Shirika la Serikali, hili nalo tujifunze kutoka kwa hao wenzetu ambao wamepiga hatua katika yale ambayo yanatukwaza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa ni wale ambao wanabeza juhudi za Rais, kwa mfano kusema mizigo imepungua bandarini, bandari yetu ya Dar es Salaam lazima tuiboreshe, kama mizigo imepungua ilikuwa hatuna faida nayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, muda sio rafiki …
MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wako umekwisha, naomba ukae.
MHE. PROF. ANNA K. TIBAIJUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja moja kwa moja.