Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizari ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Kiswaga Boniventura Destery

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Magu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizari ya Maji na Umwagiliaji

MHE. KISWAGA B. DESTERY: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikushukuru kwakunipa nafasi hii ya kuchangia. Nianze kwanza kwa kutoa shukrani kwa Wizara hii ya Maji kwa maana ya Mawaziri wote na Watendaji Wakuu wa Wizara kwa namna ambavyo wanafanya kazi. Wako watu asubuhi walisema Mawaziri hawa ni wazee, lakini nataka niseme aliyewateua bahati nzuri amefanya nao kazi, hawa ni Mawaziri makini kwelikweli na ni wachapakazi kweli. Ukienda ofisini kwao, ukiwaita jimboni wanakuja haraka kuja kuona shida ulizonazo. Kwa hiyo, kwa kweli nawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee nimpongeze Mheshimiwa Rais. Wakati anaomba kura alifika Magu akasema hapa shida moja ni maji na mimi wakati naomba kura niliwaeleza wanachi kama maji hayatapatikana sirudi 2020. Bahati nzuri wakati anazunguka hivi karibuni kwenda Simiyu alipita Magu akasema nakwenda kumuagiza Waziri wa Maji ili aweze kuja kusaini mkataba haraka na wakandarasi wawe site. Hivi ninavyozungumza mkataba ule tuliusaini hadharani kule Nyasaka ambapo utahudumu kata nne kule mjini Jimbo la Ilemela pamoja na kata tatu Jimbo la Nyamagana lakini mradi huu unaunganisha pia na Lamadi na Misungwi. Magu wakandarasi wako site.Nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa ahadi yake ya kweli na Wanamagu watapata maji, Magu ilikuwa imesahaulika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, yapo maeneo mengi, mradi huu wa Magu Mjini utahudumia wananchi 46,000 lakini Tarafa ya Ndagalu ambayo haina bwawa, haina mto, vijiji 21 wakazi 86,000 wana hali mbaya kutokana na kukosa huduma ya maji. Kwa hiyo, pamoja na kwamba bajeti hii inasemwa haitoshi na mimi nikisema hii inatosha maana yake tarafa hii haitaingizwa. Hata hivyo, niendelee kusema tunapokuwa na shilingi bilioni 600 zikaenda zote shilingi bilioni 600 mwaka huo tunahama hapo, tukiongeza ifike shilingi bilioni 900 halafu hatuna uwezo wa kuwa nazo haitusaidii. Mimi niombe shilingi bilioni 600 hizi ziende zote, wale ambao mmepangiwa miradi tutahama kwenda maeneo mengine. Pamoja na hayo,


tuuongeze huu mfuko wa shilingi 50 kwa kila lita ya mafuta ifike shilingi 100 ili usaidie kuharakisha kutekeleza miradi hii. (Makofi)


Mheshimiwa Naibu Spika, Tarafa ya Ndagalu na Tarafa ya Sanjo wana hali mbaya kama nilivyosema. Hawana mito, hawana mabwawa na bahati mbaya kabisa wanakwenda kuchota maji kilometa 58 wengine, wanaamka saa tisa za usiku. Nazungumza haya kwa sababu Mheshimiwa InjiniaLwenge ameshawahi kufanya kazi kule Mwanza na Magu anaijua vizuri, Ndugu Kalobelo anaijua vizuri Magu. Wanaamka saa tisa na unajua Wasukuma muda ule wa mapema baba mwenye mji anakaa kwenye kimunya anachunga ng’ombe kwa hiyo kuingia kulala ni saa saba, naye amechoka, anafika kwenye kitanda puu, akiamka saa tisa amuangalie mwenzake ili atafute mtoto hayupo yuko kwenye maji. (Kicheko/Makofi)


Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niombe sana tuwahurumie hawa wananchi, ni tatizo kubwa. Kwa hiyo, muone kwamba wazalishaji wakubwa wa uchumi ni akinamama, muda mwingi wanaumalizia kuchota maji kuliko kuzalisha. Niombe, kama tutaongeza Mfuko wa Maji, Tarafa za Ndagalu na Sanjo ziangaliwe kwa umakini wake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna watu hapa bado wanabeza Serikali hii ya Awamu ya Tano na bado wanasema 2020 haitarudi. Nataka niwahakikishie kwamba Serikali hii inarudi kwa kishindo kifua mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, haya maneno yanathibitishwa na Biblia Takatifu. Wakorintho 10:23, inasema, vitu vyote ni halali bali si vitu vyote vifaavyo. Ikaongeza, vitu vyote ni halali bali si vitu vyote vijengavyo. Vyama vyote ni halali lakini chama kinachoweza kujenga ni Serikali ya Chama cha Mapinduzi. Vyama vyote ni halali lakini chama ambacho kinaweza kuwa kizuri ni Chama cha Mapinduzi. (Makofi)


Mheshimiwa Naibu Spika, mnazungumza kwamba mmemezwa demokrasia kwenda kuwaeleza watu mtaenda mkaeleze nini? Kama ni demokrasia, juzi MArehemu Mheshimiwa Dkt. Macha amefariki tukatarajia mtaleta mtu yuleyule (mlemavu), hamkuleta mlemavu, ninyi mna demokrasia gani?

Mlituletea hapa wagombea wawili tukasema waongezeni, mkaleta sita mkawanyima kura hata ninyi, hata Makamu Mwenyekiti mmemnyima kura, hao wote wangejiuzulu wakarudi CCM. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, msiseme kwamba hakuna demokrasia.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba watuvumilie kidogo, tuwe na uvumilivu wa kisiasa ili tuelewane kidogo, ninyi mmezungumza asubuhi hapa.

TAARIFA...

HE. KISWAGA B. DESTERY: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza taarifa siikubali kwa sababu chama kina mamlaka ya kubadilisha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nchi hii Rais Dkt. Magufuli, kama ni upele umepata mkunaji sasa. Unajua ili uwe jemedari lazima upigane vita, huwezi kuwa jemedari bila kupigana vita. Rais Dkt. Magufuli amepigana vita ya ufisadi, rushwa, vyeti hewa na mambo mengi, kwa hiyo, amefanya kazi ambayo alikusudia.

Mheshimiwa Naibu Spika, Rais Dkt. Magufuli wakati ....Yeye atafanya kazi, hatajali chama…

Wale ambao wanatoka vyama vya upinzani tutapata wapi Rais wa namna hii? Kwa hiyo, naomba niwaambie Wabunge wenzangu wajue kwamba dereva mliyenaye atawafikisha salama na CCM itashinda mwaka 2020. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kiswaga, muda wako umekwisha, ahsante sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja lakini tuvumiliane kisiasa, tuwe na ngozi nene.