Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizari ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Athumani Almas Maige

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tabora Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizari ya Maji na Umwagiliaji

MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi pia naomba nikushukuru sana kuniruhusu nichangie bajeti hii ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wabunge wote humu ndani, naomba niwashauri tu kwamba wampe pongezi Mheshimiwa Dkt. Magufuli kwa kazi nzuri anayoifanya na Mawaziri hawa ambao ni vigogo. Siyo kweli kwamba Mawaziri hawafanyi kazi, lakini Wabunge wote imekuwa tunataka maji hata kama tungepewa ng’ombe tugawane hatoshi, kinachotolewa sasa kinatosha sana. Mimi naomba niwashukuru sana Mawaziri ninyi wawili na hasa mpelekeeni salaam Mheshimiwa Dkt. Magufuli kwa miradi mitatu ambayo iko Jimboni kwangu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, mradi ule wa umwagiliaji katika kata ya Shitage, unaenda vizuri lakini naomba muusimamie vizuri umalizike. Vilevile hivi karibuni tumesaini mkataba wa bomba la maji kutoka Ziwa Victoria kuleta maji Uyui na kupeleka Tabora. Mabilioni ya fedha yamewekwa pale, tungepata wapi kama siyo Rais Mheshimiwa Dkt. Magufuli? Pia tume-comission mradi mkubwa wa maji pale Mabama kwa niaba ya Mkoa mzima wa Tabora uliosaidiwa na Japan, mradi mkubwa vijiji 31 katika kata zangu vinapata maji, tungepata wapi mtu kama Mheshimiwaw Dkt. Magufuli? Aidha, uko mradi nimeuona umeanzishwa kutoka Malagarasi kuleta maji Urambo na Kaliua unapita pia mpaka kata zangu za Ndono pale Ilolangulu. Mradi huu mmeutengea shilingi bilioni mbili, naona Mheshimiwa Mama Sitta hakuwa ameiona hiyo lakini naomba muuanze ili tuweze kuufanikisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, yako matatizo katika Wizara hii ambayo kwa kweli mimi sidhani kama yanatokana na wao wenyewe. Tumeona bajeti haitoshi, tunawashauri wakachukue shilingi 50 za mafuta waziweke kwenye mradi wa Mfuko wa Maji ili akina mama hawa wapumzike. Ni kweli akina baba wanawakosa akina mama asubuhi, hii hairuhusiwi. Nashauri tuimarishe suala hili ili watoto waende shule wameoga na akina mama wateke maji maeneo ya karibu. Wabunge wote tumeomba humu ndani ya Bunge Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Naibu Waziri kubalini hilo tupate hela za mfuko. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba mnisikilize vizuri sana Mawaziri, katika Jimbo langu katika kijiji cha Majengo lilijengwa bwawa, wananchi wakafurahi, wakaanza kuvua samaki, wakamwagilia, bwawa likapasuka baada ya miaka miwili; huu ni mwaka wa tano hamjarudi tena kurekebisha bwawa lile. Mheshimiwa Waziri kama husemi vizuri kuhusu bwawa hili na mimi nitatoa shilingi. Bwawa la Majengo katika kata ya Ikongolo mlijenga limefanya kazi vizuri miaka mitatu limepasuka, mwaka wa tano hamjarudi wala hamjasema sababu kuwaambia wananchi kwa nini hamrudi, naomba mrudi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wangu wanakesha wanatafuta maji, nimelipa Serikalini hela nyingi kuwaita Wakala wa Maji na Mabwawa na Wachimba Visima wakapima maji yapo chini, cha kusikitisha, huu ni mwezi wa tano nakutafuta Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri, Halmashauri wameleta ripoti maji yapo chini tena ya kutosha kwenye vijiji viwili vile vya Inonelwa pamoja na Ikongolo ambako ndiyo hakuna maji, maji yapo chini mengi. Mimi Mbunge nimelipia hela zangu, nataka mje mchimbe kwa sababu maji yapo. Namuomba Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Naibu Waziri mnipe majibu kwa nini hamji kuchimba maji ambayo nimegharamia kuyatafuta na yapo chini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, mmeutaja mradi huu wa Shitage mwaka wa tatu huu eti wamefanya mita 170, mradi hauendi. Wananchi wanategemea kumwagilia mpunga tupate mpunga pale kwa nini hauendi? Naomba mtakapokuja tena mniambie kwa nini mradi huu wa Shitage umekwama?

Mheshimiwa Naibu Spika, tunagombania muda hapa, mimi naunga mkono hoja na nakushukuru sana kuniruhusu nichangie hoja hii ya Wizara ya Maji, ahsante sana.