Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Rashid Mohamed Chuachua

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Masasi Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. RASHID M. CHUACHUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kupata fursa hii ya kuchangia hotuba ya Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuipongeza Serikali, Ofisi ya Waziri Mkuu na Waziri Mkuu mwenyewe kwa kazi kubwa na nzuri inayopendeza ya kuandaa hotuba hii ambayo kimsingi inatafsiri kwa kina Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi na Mpango wa Maendeleo wa mwaka mmoja. Hongera sana Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia niseme tu kwamba kazi kubwa inayofanywa na Serikali iliyopo madarakani ni kazi ambayo inapaswa kuungwa mkono na sisi Wabunge. Tuiunge mkono Serikali yetu ili tuweze kusonga mbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nisisahau kusema kwamba wakati tuna harakati za kisiasa, wananchi wangu hawakunituma ili nije kuonekana kwenye tv. Wamenituma nije kufanya kazi kwa sababu wao hawahitaji tv, wanahitaji maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo napenda niiambie Serikali kwamba wakati tunajiondoa kwenye hali ya utegemezi lazima tufahamu kwamba maendeleo haya tunayoyataka ni vita kubwa sana. Hili ni jambo la msingi sana, maendeleo ni vita. Nachukua kauli ya Profesa wangu Mheshimiwa Norman Sigalla King ameandika maendeleo ni vita. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wapo viongozi wengine ni waandamizi, wanazungumza kwamba Serikali ya Chama cha Mapinduzi pamoja na Rais wake wanapofanya kazi kubwa ya kuwawajibisha watumishi ambao kimsingi wanatenda kinyume na taratibu za utumishi wa umma wanakosea, hili ni suala la ajabu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema ni suala la ajabu kwa sababu viongozi hao wanafikia hatua ya kudiriki kuzungumza kwamba wanaowajibishwa ni watu wa mkondo fulani wa kisiasa, ni jambo kubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivi kwa sababu Mheshimiwa Rais tunamuona anavyofanya kazi na Waziri Mkuu akiwa anawawajibisha viongozi ambao kimsingi wengine ni waandamizi katika Chama cha Mapinduzi. Kwa hiyo, lazima tuzungumze mambo ambayo hatuwapotoshi Watanzania. Tukisema hivi maana yake tunataka kuwaaminisha Watanzania kwamba hao wanaoharibu wao ndiyo wamewatuma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba wakati Serikali inakwenda kwenye hatua ya maendeleo ya viwanda, naomba waendee katika hatua hiyo wakijua kwamba maendeleo haya ni vita. Unapokwenda kwenye viwanda unahitaji rasilimali kubwa inayozalishwa nchini iende kwenye processing industry, lakini wakati huo huo tunawakwaza Watanzania wenzetu ambao kimsingi tuliwategemea watusaidie, wao kazi yao ilikuwa ni kusafirisha malighafi, wanakwazika na kitendo cha Tanzania kutaka kwenda kwenye uchumi wa viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapotaka kwenda kwenye uchumi wa viwanda na kuziwezesha sekta zinazotegemea viwanda, wapo Watanzania wenzetu wanaishi hapahapa, wanakwazika na ununuzi wa ndege kwa sababu wana hisa kwenye makampuni mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapotaka kuboresha reli tunawakwaza Watanzania wenzetu kwa sababu wengine wana malori, wanataka bidhaa zisafirishwe kwa malori wapate faida hata kama tunadidimia katika uchumi wetu. Maendeleo ni vita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali ikaze buti kuhakikisha kwamba inasimamia yale ambayo wameyasema na sisi tutawaunga mkono. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maneno haya, niseme tu kwamba wakati tunakwenda kwenye uchumi wa viwanda tunategemea sana kilimo lakini mipango yetu inaonyesha wazi kabisa kwamba mchango wa sekta ya kilimo ni asilimia 25 tu katika Pato la Taifa wakati nguvu kazi iliyopo katika kilimo ni zaidi ya asilimia 74.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ina maana kwamba kiasi kikubwa cha nguvu kazi kipo kwenye kilimo lakini tija ya kilimo bado haiwezi ku-support uchumi wa viwanda. (Makofi)
Naiomba Serikali iliangalie hili na ihakikishe kilimo kinatengewa pesa za kutosha. Wakati wa kuondoa kero kwa wakulima wetu ni sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaishukuru Serikali kwa kauli aliyoitoa Waziri Mkuu, alipotembelea maeneo ya Kusini. Amefanya uamuzi mkubwa wa kufuta baadhi ya makato ambayo yalikuwa ni kero kubwa kwa wakulima. Huu ni uamuzi mkubwa sana. Wakulima wetu wamelalamika kwa miaka mingi na tunaendelea kuitia moyo Serikali kwamba iendelee kuona namna ambavyo inaweza kuondoa kero kwa wakulima wa mazao yote yanayotegemewa kukuza uchumi wa nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo, tunategemea pia Serikali sasa itoe kipaumbele katika suala zima la pembejeo. Katika bajeti iliyopita, Serikali ilitoa voucher za pembejeo kwa takribani voucher milioni tatu. Mkoa wa Mtwara peke yake ulipata voucher 10,000 tu na Jimbo la Wilaya ya Masasi lilipata voucher 3000. Hili ni jambo ambalo linaweza kuwakatisha tamaa wakulima kwa sababu voucher hizi hazikutosha. Naiomba Serikali iongeze mkazo mkubwa sana katika kuhakikisha kwamba voucher zinatoka za kutosha ili wakulima wetu wapate pembejeo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze haraka haraka kwenye suala la elimu. Tunazo changamoto kubwa na Serikali imefanya juhudi kubwa. Mimi naamini kwamba changamoto hizi ni sehemu ya maendeleo. Kwa hiyo, niendelee kuiomba Serikali iendelee kufanya juhudi kubwa, lakini naiomba Serikali hii ya Chama cha Mapinduzi, iweke msisitizo mkubwa sana kwenye suala la Elimu ya Watu Wazima na Elimu nje ya mfumo rasmi. Ukiangalia historia ya elimu ya nchi hii, toka Serikali ya awamu ya kwanza, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Baba wa Taifa, alifanya kazi kubwa katika eneo la Elimu ya Watu Wazima na Elimu nje ya mfumo rasmi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema kwa sababu tunahitaji nguvukazi kwenye Sekta ya Viwanda, hatuwezi kuhakikisha kwamba tunawaelimisha Watanzania wengi kwa wakati mmoja kwa kutegemea waingie madarasani. Pia naiomba Serikali ifahamu kwamba kiwango cha Watanzania kutokujua kusoma na kuandika kinaongezeka na vijana wetu wengi hawana elimu ya kutosha. Kwa hiyo, tunaweza tukawa na viwanda vya kutosha lakini tukaishia kwenye kuwa wabeba mizigo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nawaomba sana, Serikali yangu ihakikishe kwamba inapanua wigo wa elimu ili wale ambao hawana uwezo wa kwenda kwenye sekta rasmi ya elimu waweze pia kupata elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo changamoto kubwa katika ardhi, lakini juhudi za Serikali za kutaka kuwapimia wananchi tunazipongeza ila tunamwomba kwa heshima kubwa Waziri wa Ardhi afike Jimbo la Masasi ili atatue kero za wananchi wa Masasi. Wananchi wa Masasi wana matatizo mengi katika ardhi na bahati nzuri tumezungumza na Waziri, amesema atapanga muda. Naomba baadaye atuambie ni lini atakwenda ili kusudi wananchi waweze kutatuliwa matatizo yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo matatizo katika eneo la afya, lakini pia Serikali imepiga hatua katika kutatua kero za afya kwa wananchi wetu, isipokuwa katika Jimbo la Masasi matatizo bado yapo. Tunaiomba Serikali ihakikishe kwamba katika bajeti ya mwaka huu inatoa pesa za kutosha ili kuhakikisha kwamba wananchi wetu wanapata huduma za afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze tu suala la ulinzi na usalama. Tunaishukuru Serikali kwa juhudi zake, tunashukuru Serikali kwa kuhakikisha kwamba inawajali Askari Polisi. Isipokuwa katika Jimbo la Masasi, kuna tatizo kubwa. Jeshi la Polisi wanaishi katika maeneo ambayo hayana nyumba. Tunaomba Serikali iangalie hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, nizungumze tu kwamba Askari wetu wa Jeshi la Kujenga Taifa, tunaomba wapatiwe Bima ya Afya. Ahsante sana.